2017-09-07 12:16:00

Baba Mtakatifu Francisko "atinga timu" nchini Colombia!


Baba Mtakatifu Francisko amewasili nchini Colombia, Jumatano jioni, tarehe 6 Septemba 2017 na kupokelewa na bahari ya watu waliongozwa na viongozi wa Serikali na Kanisa nchini Colombia. Rais Juan Manuel Santos Calderon kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Colombia, alimkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kwa mikono miwili, huku akisindikizwa na shamrashamra ya wananchi wa Colombia ambao walionekana kujipanga kwenye barabara kuu kuelekea kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Colombia, umbali wa kilometa 15 kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bogotà.  

Baba Mtakatifu akiwa uwanja wa ndege amepewa shada la maua na mtoto Clara Rojas, mtoto wa mbunge ambaye alitekwa nyara kunako mwaka 2002 na Kikosi cha Mapinduzi ya Kijeshi “FARC” na baadaye kuachiliwa huru! Katika patashika hii nguo kuchanika, Mtoto Clara akazaliwa huko msituni, kumbe, mtoto huyu ni alama ya amani na matumaini kwa wananchi wengi wa Colombia

Baba Mtakatifu alipowasili kwenye makao makuu ya Ubalozi wa Vatican amewashukuru na kuwapongeza wote waliojitokeza kumpokea. Amewataka wananchi wa Colombia kuendelea kujikita katika mchakato wa amani na upatanisho kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Baba Mtakatifu anawataka wananchi wa Colombia kutokubali wajanja wachache kuwapoka furaha na matumaini yaliyo mbele yao! Vijana hawa ni wale ambao wanatoka katika maeneo ya watu maskini sana kutoka Colombia na wengi wao wamesaidiwa kutoka kwenye matumizi haramu ya dawa za kulevya.

Rais Juan Manuel Santos Calderon akizungumza na waandishi wa habari elfu tatu kutoka ndani na nje ya Colombia wanaofuatilia tukio hili, amemshukuru sana Baba Mtakatifu Francisko kwa kusaidia mchakato wa amani na upatanisho nchini Colombia. Hii ni mara ya tano wanakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko na daima tema kuu imekuwa ni amani na upatanisho wa kitaifa! Amewatia shime kusonga mbele hata pale ambapo vizingiti vilijitokeza na kutaka kukwamisha mchakato huo. Ameonesha: furaha, shukrani na matumaini makubwa kwa wananchi wa Colombia kwa siku za usoni.

Ijumaa, tarehe 8 Septemba 2017 huko Villavicencio, Kusini mwa mji wa Bogotà ni siku maalum sana, kwani kunafanyika Ibada ya Upatanisho wa Kitaifa katika Uwanja wa Las Malocas. Baba Mtakatifu Francisko atapata nafasi ya kukutana na kusalimiana na kusikiliza shuhuda za waathirika wa vita nchini Colombia, vita ambayo imedumu kwa takribani miaka 50. Atafanya tafakari ya kina kwenye Msalaba wa Upatanisho wa Kitaifa. Rais Juan Manuel Santos Calderon anakaza kusema, waathirika wa vita ya wenyewe kwa wenye wamepewa kipaumbele cha kwanza katika mchakato mzima wa upatanisho wa kitaifa! Familia ya Mungu nchini Colombia imesheheni furaha na matumaini makubwa kwa ujio wa Baba Mtakatifu Francisko ambaye anataka kuwahamasisha kupiga hatua ya kwanza katika mchakato wa upatanisho baada ya miaka mingi ya vita, ghasia na mipasuko ya kijamii!

Sasa Colombia inataka kuandika ukurasa mpya wa matumaini na maendeleo endelevu! Baba Mtakatifu Francisko amekuja kwa wakati muafaka katika kusaidia mchakato wa amani, upatanisho na kwamba, sasa ni wajibu wa wananchi wa Colombia kusimama kidete kulinda na kudumisha amani na upatanisho ambao wameutolea jasho sana! Huu ni wakati wa ujenzi wa amani nchini Colombia! Wananchi wa kawaida wanasema, kwa hakika Baba Mtakatifu Francisko ni chemchemi ya: furaha, huruma, upendo na amani kwa wananchi wa Colombia. Jambo la msingi wanasema wananchi ni wanasiasa kujizatiti sasa kujenga na kudumisha amani, upatanisho na msamaha unaobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo za watu! Yaliyopita si ndwele, sasa wagange yaliyopo na yale yajayo mbele yao kama ndugu na wala si kama maadui wanaoangaliana “kwa jicho la makengeza”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.