2017-09-06 11:51:00

Semina ya Kimataifa kuhusu vijana kuanza kutimua vumbi 11-15 Septemba


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, Kanisa linataka kuandamana na kushibana na vijana bega kwa bega ili kuwasikiliza kwa makini, kuwafunda kutoka katika undani wao na kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayofanyika mwezi Oktoba 2018 mjini Vatican kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” ni nafasi ya pekee kwa Maaskofu kuwasikiliza vijana kwa makini ili hatimaye, Kanisa liweze kuibua mbinu mkakati wa utume kwa vijana wa kizazi kipya!

Kardinali Lorenzo Baldisseri anasema, kuanzia tarehe 11-15 Septemba 2017 kutafanyika semina ya kimataifa mjini Roma itakayowahusisha vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu vijana. Hii ni nafasi kwa vijana kuweza kupembua kwa kina na mapana mada mbali mbali zinazohusu maisha yao ili hatimaye, kuweza kuwachagua vijana watakaowawakilisha katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana, mwezi Oktoba, 2018. Hii ni semina elekezi itakayo wasilisha maoni ya vijana baada ya kupembuliwa kwa kina katika makundi kadiri ya lugha za wajumbe.

Kardinali Baldisseri anakaza kusema, tema zinazojadiliwa kimsingi ni: vijana na utambulisho wao; miradi inayoweza kutekelezwa na vijana; vijana na teknolojia; vijana na maisha ya kiroho. Hata wale “vijana wa zamani” wanaopenda kushiriki wanakaribishwa sana. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukazia sana utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ili kuwajengea matumaini ya kuweza kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Vijana kati ya umri wa miaka 16 hadi 29 wanahamasishwa kushirikisha maoni yao kwa njia ya mtandao, ili kwamba, baada ya maoni yao kuchambuliwa, Sekretarieti kuu ya Sinodi iweze kuandaa “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya Kutendea Kazi”.

Semina hii ya kimataifa inawashirikisha wataalam wa utume wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Sekretarieti kuu ya Sinodi inaendelea kukusanya maoni kutoka kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki duniani, Makanisa ya Mashariki pamoja na majibu yaliyotolewa na vijana kwenye mtandao wa Sinodi ya Vijana. Vyama vya kitume kwa ajili ya vijana vinahamasishwa pia kutoa maoni kuhusu utekelezaji wa utume wa vijana katika parokia zao. Vijana watawakilishwa kama wasikilizaji ambao pia wanaweza kuchangia maoni yao wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu.

Sinodi hii itawashirikisha pia vijana kutoka katika dini na madhehebu mbali mbali, ili kwa pamoja waweze kuwa na mbinu mkakati wa utambulisho wa vijana. Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kutembea na kuandamana na vijana wa kizazi kipya, bega kwa bega; kwa kuwasikiliza kwa makini; ili kuwaandaa vijana hawa kuweza kutekeleza dhamana na utume wao ndani na nje ya Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni matumaini ya Mama Kanisa kwamba, vijana wako tayari kusikiliza ushauri wa wahenga, ili waweze kutoka kufua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.