Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwalinda na kuwasaidia wahamiaji!

Biashara haramu ya binadamu ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu! - AP

06/09/2017 14:05

Padre Michael Czerny, Katibu mkuu msaidizi, Idara ya wahamiaji na wakimbizi, Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu ya binadamu akichangia katika kikao cha Umoja wa Mataifa kinachojadili kuhusu “Mkataba wa Kimataifa juu ya usalama wa Wahamiaji 2018” mjini Vienna, Austria kuanzia tarehe 4-5 Septemba 2017 amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za wahamiaji na wakimbizi duniani!

Mkutano wa Vienna ulikuwa unajadili kuhusu: kutoroshwa kwa wakimbizi, biashara haramu ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo; utambulisho, ulinzi na usalama sanjari na huduma kwa waathirika wa biashara haramu ya binadamu! Padre Michael Czerny amewasilisha mapendekezo na vipaumbele vinavyotolewa na Mama Kanisa mintarafu changamoto kubwa ya wakimbizi na wahamiaji duniani, wanaoendelea kuteseka hata katika mifumo mipya ya utumwa mamboleo. Hawa ni watu ambao wamegeuka kuwa kama bidhaa inayoweza kuuzwa na kununuliwa sokoni!

Kumekuwepo na mafanikio makubwa katika Jumuiya ya Kimataifa kuhusu watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa na wahamiaji, lakini maisha yao yako hatarini, wanapokuwa katika mchakato wa kutafuta hifadhi na usalama wa maisha, kiasi kwamba, wengi wao wanajikuta wametumbukia katika mikono ya makundi ya kihalifu kimataifa. Ikumbukwe kwamba, uhamiaji ni dhana inayojengeka katika matumaini makubwa ya kupata hifadhi, usalama, ustawi na maendeleo endelevu. Lakini kwa bahati mbaya, si kila mtu anaweza kufanikisha ndoto hii kwa njia halali na matokeo yake, watu hawa wanajikuta wakiwa wametumbukia katika mikono ya wafanyabiashara haramu ya binadamu, wanaowanyanyasa na kuwadhulumu, utu na heshima yao kama binadamu!

Kutokana na changamoto ya ulinzi na usalama kwa wakimbizi na wahamiaji, ujumbe wa Vatican unaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwa na mfumo bora wa sheria na njia halali ambazo zinaweza kutumiwa na wakimbizi na wahamiaji ili kuweza kupata hifadhi na usalama wa maisha yao, ili wasitumbukie katika mitego ya wafanyabiashara haramu ya binadamu! Umaskini, ukosefu wa fursa za ajira, elimu duni na dhuluma; vita, ubaguzi na nyanyaso mbali mbali ni kati ya mambo yanayowatumbukiza watu wengi katika biashara haramu ya binadamu inayokuzwa kutokana na utalii wa ngono, hitaji la nguvu kazi sanjari na uchu wa mali na fedha!

Taarifa za biashara haramu ya binadamu kwa mwaka 2016 zinaonesha kwamba, kumekuwepo na ongezeko kubwa la watu wanaosafirishwa kama bidhaa na kwamba, asilimia 51% ya waathirika ni wanawake, asilimia 21% ni wanawaume, asilimia 20% ni wasichana na wavulana ni asilimia 8%. Watu kati ya milioni 21 hadi 46 wametumbukizwa katika kazi za suluba, biashara ya ngono pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, sera na mifumo mbali mbali ya uchumi inajikita katika kukabiliana na tatizo la biashara haramu ya binadamu. Vyombo vya ulinzi na usalama: kitaifa na kimataifa havina budi kushirikiana ili kutokomeza biashara hii haramu na wahusika kufikishwa mbele ya sheria. Kuna haja pia ya kuwaelimisha watu watakawasaidia wakimbizi na wahamiaji kupata haki zao msingi.

Padre Michael Czerny anakaza kusema, huduma makini kwa waathirika wa biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo, hawana budi kupatiwa ushauri nasaha na huduma msingi zitakazowawezesha kurejea tena kwenye jumuiya zao. Uponyaji wa ndani unahitajika sana. Hii ni biashara inayohitaji ushirikiano wa wadau katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu, bila kusahau mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa pamoja na taasisi zake. “Mkataba wa Kimataifa juu ya usalama wa Wahamiaji 2018” ni njia inayotaka kuboresha dhana ya wakimbizi na wahamiaji kwa kutumia njia halali. Ujumbe wa Vatican unatarajia pia kushiriki katika mkutano wa Umoja wa Mataifa unaotarajiwa kutoa Mpango Mkakati wa Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu, utakaofanyika mjini New York kuanzia tarehe 27- 28 Septemba, 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

06/09/2017 14:05