2017-09-05 07:28:00

Iweni mashuhuda wa kweli wa Fumbo la Msalaba!


Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XXII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa, inatoa changamoto kubwa kwa wale wanaotaka kumfuasa Kristo, kwanza kabisa kujikana wao wenyewe, yaani kuuvua utu wa kale uliochakaa kama jani la mgomba na kuanza kujivika utu mpya unaofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani, tayari kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Kuchukua vyema Msalaba wako, yaani kutambua ukuu wa Msalaba ambao ni kielelezo cha ufunuo wa huruma, upendo na hekima ya Mungu kwa binadamu, tayari kumfuasa Kristo ili kumtangaza na kumshuhudia katika uhalisia wa maisha yenye mvuto na mashiko.

Shida na magumu ni sehemu ya maisha na utume wa Unabii kama zinavyoshuhudiwa na Nabii Yeremia aliyeteseka kiasi hata cha kupata kishawishi cha kutaka “kubwaga manyanga na kutokomea mbali” lakini anakumbuka kwamba, utume wake ni sawa na moto unaowaka ndani mwake, hauwezi kuzimika kwa kuyakimbia majukumu! Mama Kanisa anawataka watoto wake, kuwa kweli ni sadaka safi inayompendeza Mwenyezi Mungu na tayari kumjifunza Kristo Yesu kwa kufuata nyayo za Njia yake ya Msalaba, ili kushiriki katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu!

Nabii Yeremia katika somo la kwanza anasikitika kusema kwamba, kila mara asemapo anapiga kelele na kulia kwa uchungu kutokana na dhuluma na uharibifu, kwa kuwa Neno la Mungu limefanywa kuwa shutuma kwake na dhihaka mchana kutwa! Nabii Yeremia anaonesha uchungu mkubwa unaobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wake. Anatabiri adhabu na mateso makubwa kwa Wayahudi kwa kutomsikiliza Mungu na kutii Amri na Maagizo yake, lakini, mambo yote haya yanachelewa kutekelezwa na Mwenyezi Mungu, aliye mwingi wa huruma na mapendo.

Matokeo yake Nabii Yeremia anaumia sana moyoni mwake! Alitaka Mwenyezi Mungu awashikishe adabu, awaoneshe cha mtema kuni na kile kilichomnyoa kanga manyoya! Hiki kinakuwa ni kishawishi cha kutaka kutelekeza utume wake kwa kubwaga manyanga! Anakutana na watu wenye shingo ngumu, watu ambao hawaambiliki, lakini anapokumbuka wema, huruma na upendo wa Mungu kwake, anapiga moyo konde na kusonga mbele kwa imani na matumaini kwani anatambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye nguvu na ngao ya maisha yake na kwamba, Neno la Mungu limekuwa ndani mwake kama moto unaowaka!

Katika Somo la Pili, Paulo Mtume, anawaalika waamini kutoa miili yao ili iweze kuwa ni dhabihu: safi, hai na yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu. Hii ni ibada inayowapyaisha ili kumpenda zaidi Mwenyezi Mungu kwa kumpatia kipaumbele cha kwanza katika maisha yao kwa kumpenda na kujitahidi kuishi kwa ukamilifu. Kwa maneno mengine, waamini wanahimizwa kuufia utu wao wa kale!

Yesu katika Injili ya leo anatoa masharti kwa wale wote wanaotaka kumfuasa ili kuwa kweli wafuasi wake, tayari kutangaza na kushuhudia ukuu wa Fumbo la Msalaba kwa njia ya maisha yao! Kwanza kabisa, hawana budi kujikana, kuchukua Msalaba wao vyema na kuanza kumfuasa katika maisha na utume wa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha yao, kielelezo makini cha imani yenye mvuto na mashiko kwa watu! Yesu anawataka wafuasi wake kuubeba vyema Msalaba ambao ni kielelezo cha huruma, upendo na wema wa Mungu kwa binadamu. Ni ishara ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu na muhtasari wa Fumbo la Pasaka. Ni kielelezo cha sala, neema na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Mkombozi wa ulimwengu. Ndiyo maana Kanisa linaona fahari ya kutangaza na kushuhudia ukuu na utakatifu wa Fumbo la Msalaba na kwamba, hakuna upendo wa kweli usiofumbatwa katika mateso!

Hii ndiyo changamoto ya maisha na utume wa Kinabii kwa Wakristo wote kwani kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo! Wakleri wanayo dhamana na wajibu wa pekee zaidi katika maisha na utume wa Kinabii. Ni wajibu wa wafuasi wote wa Kristo kusimama kidete kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kiinjili, Kiutu na Kimaadili. Wawe thabiti katika kukemea tabia ya rushwa na ufisadi saratani inayoisambaratisha jamii; wawe na ujasiri wa kukemea na kupambana na uchu wa mali na madaraka; kwa kuonesha mfano bora wa maisha; kwa kusimamia haki msingi za binadamu; utu na heshima ya binadamu; maendeleo, ustawi na mafao ya wengi. Wafuasi wa Kristo wajizatiti kupambana vyema na utamaduni wa kifo kwa kusimamia Injili ya uhai, familia na amani duniani.

Yesu anawataka wafuasi wake kujikana wenyewe kwa kutambua uwepo wa dhambi na madhara yake katika maisha na utume wao; wawe tayari kuubeba Msalaba wao na kuanza kumfuasa Kristo kwa ari na moyo mkuu! Kujikana ndilo wazo kuu linalobeba uzito wa pekee katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XXII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa. Kujikana ni mchakato unaofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani. Ni mchakato unaopania kupyaisha maisha kutoka katika undani wa mtu mwenyewe kwa kuuvua utu wake wa kale na kuanza kujivika utu mpya, ili kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka.

Huu ni mwaliko wa kujitahidi kuondokana na mapungufu ya kibinadamu pamoja na vilema vyake kama vile: uchoyo, ubinafsi na tabia ya kujitafuta kama kielelezo cha utimilifu wa maisha! Kujikana kuwawezeshe Wakristo kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa. Kujikana ni kuambata tunu msingi za maisha ya Kiinjili, kiutu na kijamii kwa kuheshimu na kuthamini utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kujikana ni kumpatia Mungu nafasi na ukuu wake katika maisha, ili kuambata na kukumbatia upendo wake usiokuwa na kifani. Leo, tuwe na ujasiri wa kujikana, kuubeba Msalaba na kumfuasa Kristo Yesu, tayari kumtangaza na kumshuhudia mbele ya watu wa Mataifa. Yesu mwenyewe amemkomboa mwanadamu kwa njia ya Fumbo la Msalaba, yaani mateso, kifo na ufufuko wake. Tujitahidi kuuvua utu wa kale na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.