Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Katekesi siku ya Jumatano

Wito wa kweli unapata chimbuko lake kwa kukutana na Kristo Yesu!

Papa Francisko anasema, wito wa kweli unapata chimbuko lake kwa mwamini kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yake kama ilivyokuwa kwa mitume wake wa mwanzo mwanzo!

30/08/2017 15:11

Kumbu kumbu ya wito wa mtu inasaidia kupyaisha matumaini kama ilivyokuwa kwa Mwinjili Yohane ambaye ana kumbu kumbu hai ya yale mambo yaliyotokea katika ujana wake, Yesu alipowachagua na kuwaita kwenda kuona mahali alipokuwa anaishi na tangu wakati huo, wakawa wafuasi wa Mwanakondoo wa Mungu. Itakumbukwa kwamba, Mwinjili Yohane alikuwa amemchagua Yohane Mbatizaji kuwa ni kiongozi wake wa maisha ya kiroho na kwamba, tukio hili lilitendeka huko Bethania, ng’ambo ya Mto Yordani, alikokuwako Yohane Mbatizaji, akibatiza Ubatizo wa Toba na Maondoleo ya dhambi.

Hii ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 30 Agosti 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Yohane Mbatizaji alipomwona Yesu akitembea, akawaambia wafuasi wake wawili “Tazama Mwanakondoo wa Mungu”. Wale wanafunzi wawili wakamsikia akinena, wakamfuata Yesu na alipogeuka akawaona na kuwauliza “Mnatafuta nini?” Kristo Yesu katika Injili anaoneshwa kuwa mtaalam anayeweza kugusa hata katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Wakati ule, Yesu alikutana na vijana wadadisi, waliokuwa wanatafuta maana halisi ya maisha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, vijana waliopoteza kipaji cha udadisi na ubunifu, hao ni vijana “wanaokula pensheni ya uzeeni katika ujana wao hatari sana”. Hawa ni vijana waliozeeka hata kabla ya wakati! Kristo Yesu katika maisha na utume wake, daima alipenda kutembea ili kukutana na watu, ili kuwasha moto wa mapendo ndani ya mioyo yao, ili kuzima kiu ya upendo wa dhati! Baba Mtakatifu anapenda kuwauliza vijana wa kizazi kipya hata leo hii, wanatafuta nini katika maisha? Wanatafuta nini katika sakafu ya maisha yao?

Wito wa Yohane na Andrea unapata chimbuko lake kwa kukutana na Kristo Yesu katika safari ya maisha yao na kuanza kujenga naye upendo na urafiki wa dhati, kiasi hata cha kujisikia kuwa wako nyumbani pamoja na Kristo Yesu, kiasi cha kuanza kuwa ni wamissionari, hali ambayo inaleta mvuto hata kwa akina Simoni Petro na Yakobo. Hao walipashwa Habari Njema ya kuonana na Masiha, maana yake Kristo. Hawa nao wakawa ni wamisionari waliobahatika kuonana na Kristo Yesu; tukio ambalo limeacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wao; ni mwanga ulioangazia ujana wa maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna njia mbali mbali zinazoweza kumsaidia mtu kugundua wito wake, lakini njia ya kwanza kabisa ni ile furaha ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha. Wito wa kweli wa maisha ya ndoa, maisha ya kuwekwa wakfu na upadre unapata chimbuko lake kwa kukutana na Kristo Yesu anayewakirimia waja wake furaha na matumaini mapya; anawasindikiza na kuwaongoza katika shida, magumu na changamoto za maisha na kwamba, huu ndio utimilifu wa furaha ya maisha.

Yesu anawataka watu wanaojisadaka ili kumfuasa katika miito mbali mbali na wala si watu wanamfuasa huku wakiwa na manung’uniko moyoni mwao. Anataka kuwaonjesha furaha ya kweli katika maisha, tayari kushiriki katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa furaha ya Injili. Yesu anawataka wahubiri ambao furaha ya Injili inabubujika kutoka ndani mwao, tayari kuwarithisha wengine ile furaha na imani kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Hawa ni watu wanaopendwa na Yesu kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria.

Hata katika safari ya wito, kuna wakati wa raha na magumu; kuna kushuka na kupanda anasema Baba Mtakatifu Francisko, lakini daima ni watu ambao wanasheheni matumaini na kuendelea kuota ndoto pamoja na Mwenyezi Mungu. Waamini wanapaswa kutambua chanzo cha miito yao, yaani Kristo Yesu, moto wa upendo, chemchemi ya mradi unaopaswa kuimarishwa kwa njia ya moto wa matumaini! Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanasaidia kuwasha moto wa mapendo kwa watu wanaohitaji furaha ya kweli na amani ya kudumu inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anawataka waamini kamwe wasiwe na woga wa kumsikiliza Roho Mtakatifu anayewasaidia kufanya maamuzi magumu katika safari ya maisha yao, daima wajitahidi kuthubutu kumfuasa Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

30/08/2017 15:11