2017-08-30 15:35:00

Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira, 2017


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatano tareheĀ  30 Agosti 2017 amekumbusha kwamba, tarehe 1 Septemba 2017, itakuwa ni Siku ya Kuombea Utunzaji Bora mazingira, iliyoanzishwa, kunako mwaka 2016, ili kusaidia kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika maadhimisho ya Siku hii, ameshirikiana na Patriaki Bartolomeo wa Kwanza kuandika Ujumbe unaowahamasisha waamini kujizatiti katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Wanakazia umuhimu wa kuwajibika na kuheshimu kazi ya uumbaji ambayo binadamu amekabidhiwa kuilinda, kuitunza na kuiendeleza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Viongozi wa Kanisa wanawataka wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa na watu wenye ushawishi mkubwa katika medani za kimataifa kusikiliza kilio cha dunia na kilio cha maskini, ambao wanateseka sana kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi!

Na Padre Richard. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.