Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Jitoeni sadaka kusimamia, kutangaza na kushuhudia ukweli!

Yesu anawaalika wafuasi wake kujikana wenyewe, kuubeba vyema Msalaba na kuanza kumfuasa! - AFP

30/08/2017 18:22

Katika jamii inayopambwa na huria ya kimaadili ukweli hutoweka. Huu ndiyo ulimwengu tunaoishi leo hii ambapo mwanadamu amejipatia mamlaka ya juu kabisa ya kuamua lililo jema au ovu kadiri aonavyo yeye na kadiri ya vionjo vyake. Ndipo katika ulimwengu huu sisi Wakristo tunaitwa kila siku kwa ajili ya kumshuhudia Kristo anayetufunulia Neno la Mungu ambalo ni msingi wa ukweli wote. Ushuhuda wetu huu unatudai kutenda tukikinzana na upepo. Maelekeo na matamanio ya kiulimwengu ni rahisi kutuhadaa na kufikiri kwamba hiyo ndiyo namna sahihi ya kutenda kumbe sivyo. Hiyo ndiyo sadaka tunayoalikwa kuitoa katika Dominika hii kwa kujikatalia utu huo wa dhambi, utu huo bandia na kumfuata Kristo katika ukweli.

Injili ya Dominika hii kwa upande mmoja inatuwekea Kristo mbele yetu kama mwakilishi wa njia ya ukweli na kwa upande mwingine inawaweka wakuu wa makuhani na waandishi kama wapinzani wa ukweli huo. Neno la Kristo ambalo linajipambanua katika nafsi yake lilinua kuufunua ukweli ambao ulifubaishwa na dhambi lakini kinyume chake unakutana na ukinzani wa matendo ya binadamu ambaye amekwisha kulowea katika njia ya upotofu. Njia hii ya upotofu inatupatia utambulisho bandia ambao ndiyo tunaojikinai kuwa ni utambulisho wetu rasmi. Katikati ya upinzani huo tunapata mwaliko wa kusonga mbele na kuusimamia ukweli.

Ukinzani huu unajionesha leo hii katika jamii mamboleo ambayo imemtukuza mwanadamu katika kiwango cha juu. Ukweli juu ya mwanadamu umepindishwa. Neno la Kristo halipati nafasi katika jamii hii kwani linaonekana kuingilia mipaka ya mtu huru ambaye anapaswa kuachwa kujiamulia mambo yake katika uhuru wote. Hali ya dhambi imegandamana nasi kiasi cha kushindwa kuiona hali yetu halisi ambayo tunapaswa kuwa nayo. Kristo anatuambia kwa hakika kwamba tusipoachana na huo utambulisho wetu wa bandia tutapotea. Ni mwaliko wa kugutuka na kuiacha hiyo nafsi ambayo si utambulisho wetu na kujivika hali yetu halisi, hali ambayo inaambatana na msalaba, yaani njia ya mateso, kukataliwa na hata wakati mwingine kuteswa.

Kibinadamu huwa tunavutika kuitetea njia ya upotevu kwani inatupatia raha za kimwili zinazohisika. Katika njia hiyo mwanadamu anajikinai kuupata ulimwengu wote; kumiliki mali, kuwa na madaraka na kufanya maisha ya starehe na anasa. Lakini Kristo anatuonya kwa kutukumbusha kuwa hayo yote yatatusaidia nini kama tutaipoteza nafsi yetu milele? Katika hali hiyo ya kibinadamu tunamwona mtume Petro anausahau ujasiri wake tuliouona Dominika iliyopita kwa kumkiri Kristo kuwa ni Masiha. Anaacha kuongozwa na Roho Mtakatifu na kuruhusu mawazo ya kimwili kumtawala. Anaona ugumu kumwona Masiha huyu aliyemkiri juma lililopita kuwa ni Masiha Mteseka. Kwao walielewa masiha kama shujaa, jemedari ambaye hawezi kutikiswa na nguvu za kidunia. Ni vipi tena tuambiwe kuwa anateseka? Hii ilikuwa kikwazo kikubwa.

Hapa tunaiona kazi ya shetani inayomvuta mmoja kutolipatia nafasi neno la Mungu na kwa upande mwigine tunaiona kazi ya Mungu ambayo inapopewa nafasi inamuongoza mmoja kuyaona matendo makuu ya Mungu na kuyakiri mbele ya watu. Katika muono huo wa shetani au wa kidunia Petro anajitutumua na kuonesha kuwa alichokikiri juzi hakiwezi kuharibiwa. Ni kana kwamba anataka kuonesha tutapambana ili hadhi yako ya kimasiha isivurugwe na hawa wanaonuia kuivuruga. Tunaweza kujiuliza: Je, halikuwa jambo la hekima kwa Petro kumtetea Bwana? Je, hatupaswi kumpigania Bwana?

Kwa haraka inaonekana ni sahihi lakini kwa undani Petro ambaye pia aliwawakilisha wenzake walipohakikishiwa kuwa kweli Kristo ndiye Masiha (rejea uthibitisho wa Kristo kwa jibu la Petro Dominika iliyopita) walishaanza kujaa tamaa za kibinadamu za madaraka katika jamii baada ya ushindi wa huyu Masiha. Hawakuiona wala kuifahamu kazi ya Mungu itakayotendeka katika Masiha huyu na kuwapatia ukombozi wa kiroho. Hivyo utetezi wake ulikuwa ni kazi ya shetani na si mawazo ya kimungu. Hapa tayari mwanadamu alishajinyakulia nafasi ya Mungu na kuona kuwa yeye anao uwezo wa kupambana na kumtetea Mungu, kwamba nguvu na uwezo wake vipo juu ya Mungu. Kwa hakika ni kihoja kidogo. Juma moja lililopita Petro alikiri uwepo wa Mungu katika Kristo na kumkiri kuwa ni Mwana wa Mungu na juma hili mara moja anaonesha mashaka katika uwezo huo wa Mungu na kujikinai kuweza kumtetea ili asiingie katika njia ya mateso.

Katika somo la kwanza Nabii Yeremia anamwakilisha mwanadamu anayekumbana na mateso kwa sababu ya kuusimamia ukweli. Anaonesha kukata tamaa na hata kuona pengine Mungu amemhadaa. Anatamani kuacha kulitangaza Neno hilo la ukweli lakini kwa kuwa Mungu yupo pamoja naye bado anaendelea kusikia msukumo wa ndani ambao unamtaka kuendelea kulisimamia Neno la Mungu. Bado anautambua uwezo wa Mungu ulivyo mkuu na jinsi ambavyo Mungu ni kimbilio lake. Msukumo huo wa ndani si jambo lililomjia kwa nasibu tu bali linathibitisha muunganiko wake na Mungu. Hapa tunaona umuhimu wa paji la imani katika kuipokea kazi ya Mungu. Si suala la kulala ndani au kutojishughulisha na mambo ya ukweli na haki ndipo utajikuta unaongozwa kuusimamia ukweli. Mmoja anapaswa kujitajirisha na mambo ya kimbingu kusudi anapokumbana na changamoto wakati wa ushuhuda wa ukweli aendelee kubaki katika uthabiti.

Katika jamii yetu inayotuzunguka tunakutana na fursa chache sana za kujitajirisha na mambo haya ya kimbingu. Mitandao ya kijamii na njia nyingine za kimawasiliano vinatuondoa kabisa katika muktadha huo wa kimbingu. Mazingira haya hutuwekea mbele yetu raha na starehe za kidunia, mitindo na mifumo ya kidunia ambavyo vinamuondoa Mungu na kupingana na ukweli kuwa ndiyo mwelekeo wetu sahihi. Hivyo, mwaliko wa kujikana nafsi unaonekana pia katika namna nyingine ya kujibandua katika mazingira kinzani kwa Neno la Mungu. Hili ni jambo ambalo kwa hakika linatuhitaji kujitoa sadaka sana hasa leo hii. Tunaona ni rahisi sana na hata wakati mwingine kupoteza muda mrefu sana tumejiloweka katika mazingiza hayo lakini miguu yetu inapata uzito, macho yetu huingia ukungu, na hata akili zetu zinafubaishwa tunapopaswa kujiunganisha na Mungu kwa njia ya sala au katika kulisikiliza neno lake.

Mtume Paulo anatuhamasisha akisema: itoeni miili kama sadaka hai, takatifu na ya kumpendeza Mungu na kumalizia kuwa “msiifatishe namna ya Dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu”. Ni neno zuri linalotuhitimishia tafakari yetu kwa Dominika hii. Ni dokezo kuwa daima tulitafute Neno la Mungu na kujiweka tayari kuyatimiza mapenzi yake. Kristo anatualika kuuvua utu wetu wa kale, utu wa dhambi na kujivika utu wa utakatifu, ndiyo nafsi yake Yeye ambaye chakula chake ni kutimiza mapenzi ya Baba yake.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.

30/08/2017 18:22