2017-08-29 14:33:00

Onesho la Kimataifa la EXPO 2017 Astana Kufungwa 10 Septemba 2017


Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kuanzia tarehe 30 Agosti hadi tarehe 4 Septemba 2017 atakuwa mjini Astana, Kazakhstan ili kushiriki katika tukio la kufunga Onesho la Kimataifa la EXPO 2017 Astana hapo tarehe 10 Septemba 2017 lililokuwa kinaongozwa na kauli mbiu “Nishati ya baadaye”. Kardinali Turkson anashiriki kama Kamishina wa Onesho hili ambalo limezishirikisha nchi nyingi, ikiwemo pia Vatican. Itakumbukwa kwamba, Vatican imekuwa ikishiriki maonesho kama haya tangu mwaka 1815 kwa kuwa na banda lake binafsi ambalo kwa mwaka 2017 linaongozwa na kauli mbiu “ Nishati kwa mafao ya wengi: utunzaji wa nyumba ya wote”.

Kauli mbiu hii inafumbata matumaini na matarajio ya Jumuiya ya Kimataifa mintarafu nishati rafiki, kwa ajili ya: mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Jukwaa hili limekamilika kwa ushiriki wa Kanisa mahalia! Lengo ni kutoa kipaumbele cha pekee kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu pamoja na kujitahidi kuboresha mazingira nyumba ya wote, kwa kuwa na matumizi bora na endelevu ya rasilimali asilia. Kardinali Turkson katika ziara hii ya kikazi anafuatana na Askofu mkuu Francis Assisi Chullikatt, Balozi wa Vatican nchini Kazakhstan, Kirghizistan na Tagikistan pamoja na viongozi wa Kanisa mahalia.

Tarehe 31 Agosti 2017 Kardinali Turkson atashiriki katika mkutano wa majadiliano ya kidini ulioandaliwa kwa msaada wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, Ubalozi wa Vatican pamoja na Serikali ya Kazakhstan. Viongozi wa dini mbali mbali kutoka ndani na nje ya Kazakhstan wanatarajiwa kushiriki. Tarehe 1Septemba 2017, Siku ya Kimataifa ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira, ujumbe wa Vatican utafafanua kwa kina na mapana maudhui yaliyomo kwenye Banda la Vatican ambalo limetengenezwa kwa mfumo wa kidigitali kwa kuwashirikisha wasanii, wanazuoni na wataalam wa maisha ya kiroho wanaojadili kwa kina na mapana kuhusu: Upendo wa Mungu kama chanzo cha kazi ya uumbaji. 

Nishati kama nyenzo msingi iliyowekwa mikononi mwa binadamu ni nyenzo ambayo haijatumika barabara kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi; nishati inapaswa kutumiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; mwishoni ni nguvu ya maisha ya kiroho inayooneshwa kwa nguvu ya sala; maana ya maisha na majadiliano ya kidini. Siku ya Taifa la Vatican itakuwa ni tarehe 2 Septemba 2017. Hii ni siku ambayo ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya EXPO 2017 Astana utasomwa. Tarehe 3 Septemba, 2017 kutafanyika mkutano utakao ongozwa na kauli mbiu “Nishati kwa mafao ya wengi: utunzaji wa nyumba ya wote”. Ni mkutano utakaowashirikisha “vigogo” kutoka Umoja wa Mataifa, Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa pamoja na Makampuni ya Kimataifa yanayotengeneza nishati rafiki kwa maendeleo ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.