2017-08-29 14:10:00

Kardinali Parolin: tendeni wema, msilipize kisasi!


Vitendo vya kigaidi ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Jumuiya  ya Kimataifa inapaswa kushikamana katika mchakato wa kupambana na vitendo vya kigaidi, lakini kwa kuzingatia Injili ya upendo inayowasukuma waamini kulipa ubaya kwa kutenda mema, changamoto ambayo inahitaji ujasiri na ushupavu wa Kiinjili, vinginevyo, watu wataishia katika tabia ya kulipizana kisasi na matokeo yake ni maafa makubwa kwa watu na mali zao! Maandiko Matakatifu yanawaasa waamini kushinda ubaya kwa kutenda mema.

Huu ni ufafanuzi uliotolewa, Jumatatu, tarehe 28 Agosti 2017 na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari, huko Veneto kuhusiana na mfululizo wa vitendo vya kigaidi ambavyo vinaendelea kuitikisa Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake. Na hapa kuna mifano mingi ya waamini ambao wamegeuza ubaya kuwa ni chemchemi ya wema na huruma ya Mungu kwa waja wake, kiasi kwamba, wamekirimiwa amani na utulivu wa ndani!

Akizungumzia kuhusu ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji, ambao kwa sasa wanaendelea kuwa ni changamoto kubwa nchini Italia, kutokana na baadhi ya wanasiasa kupinga sera ya kuwapokea na kuwakaribisha wahamiaji na wakimbizi nchini Italia, Kardinali Parolin anasisitiza kwamba, pamoja na ugumu wote wanaokabiliana nao viongozi waliopewa dhamana ya huduma ya uongozi kwa raia wao, jambo la msingi linalopaswa kuzingatiwa ni mshikamano wa upendo na ukarimu; ili kuweza kukabiliana na changamoto hii kwa pamoja. Ni mzigo mkubwa ambao, Italia peke yake haiwezi kuubeba. Lakini, uchoyo na ubinafsi pamoja na baadhi ya wanasiasa kutaka kujitafutia umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko ni mambo ya hatari sana katika mafungamano ya kijamii!

Kardinali Pietro Parolin anaendelea kufafanua kwamba, ukosefu wa fursa za ajira hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ni changamoto kubwa inayogusa: utu, heshima, ustawi na matumaini ya vijana wa kizazi kipya kwa sasa na kwa siku za usoni. Ikumbukwe kwamba, kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu. Kazi humwezesha mtu kutekeleza vyema majukumu yake ndani na nje ya familia. Kumbe, kuna haja ya kuwa na sera makini za uchumi endelevu zitakazowawezesha waajiri kutengeneza fursa za ajira, ili kuwajengea uwezo wafanyakazi wao sanjari na kuwalindia: utu na heshima yao.

Vijana wa kizazi kipya wanashindwa wakati mwingine kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kwa kukosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha hasa pale wanapokosa fursa za ajira na miradi ya kuweza kuwaendeleza kiroho na kimwili. Vijana wakiwa na uhakika wa fursa za kazi, wanaweza kuwa na mwelekeo sahihi kuhusu maisha, usalama na mafungamano ya kijamii. Ukosefu wa fursa za ajira ni kati ya mifumo mipya ya umaskini duniani, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga kwa njia ya mshikamano wa upendo, unaowawezesha waamini kuiona sura ya Mungu kati ya watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali. Hawa wanaweza kuwa ni wakimbizi na wahamiaji; wazee na maskini; wagonjwa na wasiojiweza kutokana na sababu mbali mbali.

Kardinali Parolin, amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kushiriki kikamilifu katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii inatokana na ukweli kwamba, kipindi cha kiangazi kwa mwaka 2017 nchini Italia kimesababisha majanga makubwa kwa maeneo makubwa ya misitu kuungua moto na hivyo kupoteza uoto wa asili. Mito mingi inaendelea kukauka kutokana na kiangazi cha muda mrefu, hali ambayo imesababisha baadhi ya miji mikuu nchini Italia kufikiria kuwa na mgawo wa maji! Watu watambue kwamba, mazingira ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu, kuitunza na kuiendeleza, kwani ni sehemu muhimu sana ya utu, heshima na utimilifu wake. Kuna baadhi ya watu wanashutumiwa kujihusisha na uchomaji wa misitu kwa sababu wanazozifahamu wenyewe, jambo ambalo ni hatari sana kwa maisha, ustawi na maendeleo ya wengi!

Kardinali Pietro Parolin, alikuwa mjini Veneto kuzindua Jarida linalohusu ziara ya Mtakatifu Yohane Paulo II na Papa Mstaafu Benedikto XVI wakati wa likizo za kiangazi huko Kaskazini mwa Italia. Ni jarida linalokusanya maoni ya mashuhuda waliokuwepo pia katika ziara hizi za mapumziko. Amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali ili siku moja Papa Paulo I aweze kutangazwa mwenyeheri na hatumaye Mtakatifu kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.