2017-08-29 15:11:00

Angola uchaguzi umepita! Dumisheni amani na mshikamano wa kitaifa


Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe linaialika familia ya Mungu nchini Angola kusimama kidete katika kulinda, kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa; ili kukuza: amani na utulivu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Wananchi wa Angola wanakumbushwa kwamba, kwa miaka mingi, nchi yao iliogelea katika shida na magumu ya maisha kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe, wasitake tena kurejesha kurasa chungu za historia ya Angola. Wito wa Baraza la Maaskofu unafuatia matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Angola hivi karibuni na kumpatia ushindi wa kishindo Joao Lourenco, aliyekuwa Waziri wa mambo ya ndani ya nchi wakati wa uongozi wa Eduardo Dos Santos wa Angola ambaye amemaliza muda wake wa uongozi, baada ya kuiongoza Angola kwa muda wa miaka 38.

Chama cha MPLA, ambacho kimekumo madarakani tangu mwaka 1975 kimejinyakulia asilimia 64% ya idadi ya kura zote halali zilizopigwa na hivyo kujipatia viti 220 vya wabunge. Chama cha UNITA kimejinyakulia asilimia 24% na vyama vingine vimeambulia asilimia zilizobakia. Hii ni taarifa kama ilivyotolewa na Tume huru ya uchaguzi nchini Angola. Wananchi milioni 9. 3 waliokuwa na haki ya kupiga kura walitekeleza dhamana na wajibu wao Kikatiba. Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, tangu mwanzo lilikazia umuhimu wa kuhakikisha kwamba, mchakato mzima wa uchaguzi unafanyika katika ukweli na uwazi, ili kudumisha demokrasia na ukomavu wa kisiasa miongoni mwa wananchi wa Angola.

Askofu Antònio Francisco Jaca, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe anawataka wananchi wa Angola kuendelea kudumisha misingi ya haki, amani na mshikamano wa kitaifa, ili kugeuza mchakato mzima wa uchaguzi mkuu kuwa ni sehemu ya kusherehekea furaha ya demokrasia na wala si maombolezo kutokana na chuki za kisiasa. Wananchi wajenge na kuimarisha umoja na mafungamano ya kijamii kitaifa kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Baba mmoja na kamwe tofauti za vyama vyao vya kisiasa vinavyokuja na kupita, visiwe ni chanzo cha vurugu na ghasia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.