2017-08-28 14:00:00

Papa Francisko: Wabunge Wakatoliki jengeni madaraja ya majadiliano


Mtandao wa Wabunge Wakatoliki Kimataifa unawashirikisha wabunge kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaotaka kushuhudia tunu msingi za Kiinjili katika maisha na utume wao kama wanasiasa, hali inayodhihirisha pia Ukatoliki wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 27 Agosti 2017 mara baada ya Sala ya Mchana alikutana na kuzungumza na wajumbe hawa wa mkutano wa kimataifa, waliokuwa wameongozana na Kardinali Christoph Schonborn, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Vienna, Austria pamoja na Bwana Christiaan Alting Von Gesau, Rais wa Mtandao huu.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, amewashukuru wajumbe wa mkutano huu ambao kwa mara ya kwanza, wengi wao ni wale wanaotoka Barani Afrika. Licha ya mada nyeti na tete zinazotawala katika mkutano huu, lakini wanatoa kipaumbele cha kwanza kuhusu uelewa wa binadamu kadiri ya mafundisho ya Kanisa. Amewataka wajumbe hawa wanaporejea katika nchi zao, wajitahidi kujenga na kudumisha madaraja yanayowakutanisha watu, ili kuwashirikisha matunda ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, jambo msingi katika mchakato wa maamuzi katika hatua mbali mbali, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu anawataka wabunge hawa kufahamu kwa kina Mafundisho Jamii ya Kanisa ili waweze kusaidia mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika utu na haki. Sheria zisaidie kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu katika nyanja mbali mbali za kisiasa; daima kwa kusimama kidete kulinda na kuwatetea maskini na wanyonge ndani ya jamii; wajizatiti kulinda na kudumisha ekolojia ya binadamu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Wajitahidi kumwona Kristo mteseka kati ya watu wanaowahudumia, daima wakijizatiti kusimamia ukweli, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wawe ni mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.