2017-08-28 08:43:00

Papa Francisko asikitishwa na nyanyaso za kidini na maafa Barani Asia


Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 27 Agosti 2017, aliyaelekeza mawazo yake Kusini mwa Bara la Asia, hasa huko nchini Bangaladesh, Nepal na India ambazo zimekumbwa na mafuriko makubwa pamoja na maporomoko ya ardhi ambayo hadi kufikia Jumapili, zaidi ya watu 1200 walikuwa wamefariki dunia na watu zaidi ya milioni 5.7 wanahitaji msaada wa dharura.

Baba Mtakatifu anawaombea marehemu wote pumziko la milele na wale wote walioathirika faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Taarifa zinaonesha kwamba, watu zaidi ya 300, 000 wanahitaji msaada wa makazi ya muda nchini Bangaladesh. Hofu ya mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza imetanda kwa wakati huu huko Bangaladesh. Huko Nepal, hali ni mbaya zaidi kwani kuna zaidi ya watu 100, 000 wako hatarini kumezwa na maji kutokana na mafuriko makubwa.

Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na taarifa za dhuluma na nyanyaso dhidi ya wananchi wa Rohingya. Anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu hawa. Amewasihi waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaokoa wananchi hawa; awajalie kupata wasamaria wema watakaosimama kidete kulinda na kutetea haki zao msingi. Rohingya ni wananchi kutoka Myanimar na wengi wao ni waamini wa dini ya Kiislam. Taarifa kutoka kwenye vyombo vya habari kimataifa zinazonesha kwamba, wananchi wengi wameuwawa na nyumba zao kuchomwa moto na vikosi vya ulinzi na usalama nchini Myanimar.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.