Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Amani

Nigeria ni wakati wa toba na wongofu wa ndani; msamaha na upatanisho

Maaskofu wa Jimbo kuu la Owerri, Nigeria wanasema hiki ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani; msamaha, haki, amani na upatanisho wa kweli! - REUTERS

28/08/2017 09:19

Baraza la Maaskofu Katoliki linalounda Jimbo kuu la Owerri nchini Nigeria limetoa tamko la kichungaji linalomshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa maamuzi yake ya busara ya kichungaji, ili kuweza kupata suluhu ya kudumu mintarafu mpasuko wa kichungaji na kimaadili uliolikumba Jimbo Katoliki la Ahiara kwa kukataa kumpokea Askofu Peter Okpaleke aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa mchungaji mkuu wa Jimbo hilo. Maaskofu wanawaalika wakleri na waamini wote katika ujumla wao, kutekeleza agizo la Baba Mtakatifu pasi na masharti yoyote kama kielelezo chao cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kwa muda wa miaka 5, historia, maisha na utume wa Jimbo Katoliki la Ahiara umegubikwa kwa majonzi makubwa yanayotaka kulimega Kanisa. Baba Mtakatifu alimtaka kila Padre kuandika barua ya kuonesha utii kwa Askofu na kuomba msamaha, vinginevyo, wangekumbana na adhabu ya kufungiwa huduma ya Kipadre. Wakleri watumie fursa hii kujiandaa na hatimaye, kumkaribisha na kumpokea Askofu Peter Okpaleke ili aweze kutekeleza dhamana na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Umefika wakati kwa Kanisa nchini Nigeria, kuipatia kisogo kashfa hii inayoendelea kulichafua na kulidhalilisha Kanisa. Maaskofu wanasema, huu ni wakati wa toba na wongofu wa ndani, msamaha na upatanisho.

Baraza la Maaskofu Katoliki Jimbo kuu la Owerri nchini Nigeria linafafanua kwa kusema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu; uliofuatiwa na Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fàtima ni matukio ya neema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake na mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Maaskofu wanawaalika waamini kujikita katika fadhila ya unyenyekevu kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Baraza la Maaskofu Katoliki Jimbo kuu la Owerri linakaza kusema,katika kipindi cha miaka miwili yaani: tangu mwaka 2015 hadi mwaka 2017, kumekuwepo na malumbano ya kisiasa yenye harufu ya ukabila usiokuwa na mashiko wala tija kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Nigeria. Vitendo vya kigaidi vinaendelea kuhatarisha maisha, umoja na mafungamano ya kitaifa, kiasi kwamba, leo hii wananchi wana hofu na wasi wasi mkubwa kuhusu ulinzi na usalama wa maisha na mali zao.

Rushwa na ufisadi wa mali ya umma ni saratani inayoendelea kupekenyua tunu msingi za maisha ya kisiasa, kijamii, kiutu na kimaadili. Kuna umati mkubwa wa vijana wasiokuwa na fursa za ajira, hatari sana kwa usalama wa taifa. Hali ngumu ya maisha kwa wafanyakazi ni mambo yanayoendelea kusababisha majonzi makubwa kwa familia ya Mungu nchini Nigeria. Wanamwombea Rais Muhammadu Buhari afya njema pamoja na kumtaka yeye na Serikali yake, wanasiasa na wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Nigeria katika ujumla wao; kwa kusaidia kuyapatia suluhu matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi wa Nigeria kwa wakati huu. Kunaha haja ya kujenga uzalendo ili Nigeria iweze tena kucharuka katika ustawi na maendeleo endelevu. Kuna haja ya kondokana na ubinafsi, uchu wa mali na madaraka, mambo yanayosababisha vita, ghasia na mpasuko wa kisiasa na kijamii, kwa kuungana na kushikamana kama taifa moja! Madhara ya vita na ghasia ni makubwa sana nchini Nigeria, kumbe, umefika wakati kwa wanasiasa kuondokana na tabia ya ubinafsi na kuambata: huruma, majadiliano, toba, wongofu wa ndani; msamaha na upatanisho wa kitaifa. 

Kwa njia hii, Nigeria inaweza kupyaishwa tena kwa kudumisha umoja na mshikamano wa dhati! Huu ni muda wa kuachana na siasa za chuki na matusi; dharau na kejeli na kuanza kuambata mchakato wa kujenga na kudumisha haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa. Baraza la Maaskofu Katoliki Jimbo kuu la Owerri nchini Nigeria linawataka waamini kufunga, kusali na kufanya toba kama njia ya kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa ajili ya familia ya Mungu nchini Nigeria. Jumatatu, tarehe 28 Agosti 2017 wameitenga maalum kwa ajili maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kujenga kwa Kanisa kuu la Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni, Jimbo Katoliki Owerri. Hii ni nafasi kwa ajili ya kuiombea familia ya Mungu nchini Nigeria katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 

28/08/2017 09:19