2017-08-28 15:52:00

Nchi ya Tanzania itatoa uraia kwa wakimbizi wa Burundi waliofika tangu 1972


Wakimbizi wa Burundi ambao wameishi Tanzania zaidi ya miaka 45 watapokea uraia wa Tanzania. Hayo yametokana na mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya ndani ya Tanzania Mwigulu Nchembe na mwakilishi wa Tume  ya Umoja wa Mataifa kwa ulinzi wa wakimbizi Volker Türk. Serikali ya Tanzania kwa ushirikino na Umoja wa Mataifa wa kwa ajili ya wakimbizi (UNHCR) imefikia hatua ya mwisho katika mchakato wa kawaida kwa ajili ya wakimbizi wa Burundi waliofika nchini tangu mwaka 11972. Msemaji wa Umoja wa Mataifa kwa wakimbizi Teresa Ongata  anasema, kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la kusaidia wakimbizi zinaonesha kuwa katika kanda za nchi ya Tanzania, wapo wakimbizi 243,565, pamoja na hayo wapo zaidi ya wakimbizi 162,000 kutoka Burundi waliokimbia nchi yao tangu 1972.

Wiki mbili zilizopita Shirika la kusaidia wakimbizi, iliongea na Serikali ya Tanzania na kukubaliana kuwa wakimbizi wa Burundi wanapaswa kurudi katika nchi yao kwa hiari,wengine ambao wamekaa nchini humo zidi ya miaka 45 waweze kupatiwa uraia. Na Mwezi uliopita Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli aliwaalika wakimbizi wa Burundi warudi makwao kwa hiari. Mara baada ya kuongea na  Rais wa Burundi Pierre Mkurunziza huko Ngara katika Mkoa wa Kagera, alisema ni maisha mapya sasa kwa watu wa nchi ya Burundi kuanza kufikiria kurudi makwao kwa hiari  ili kujenga uchumi katika nchi yao, wakati huo huo pia kuweza kuendeleza uhusiano mwema kati ya nchi hizo mbili.Taarifa pia zinasema kuwa zaidi ya wakimbizi 5,000 kutoka Burundi ambao wako katika maeneo tofauti ya mkoa wa Kigoma wameonesha utashi wao wa kurudi makwao kwa hiari na kwa  miezi ya hivi karibuni wakimbizi 150,000 wamekwisha  rudi makwao.

Hata hivyo kuhusiana na suala la wakimbizi na matatizo ya chakula,Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP, limelazimika kupunguza mgao wa chakula kwa wakimbizi laki 3 na elfu 20 wanaoishi katika kambi za Mtendeli, Nduta na Nyarugusu mkoani Kigoma kaskazini magharibi mwa Tanzania. WFP inasema imelazimika kufanya hivyo kwa sababu ya upungufu wa fedha. Hiyo ni kwasababu inahitaji kwa haraka jumla ya Dola za Marekani milioni 23.6 kuanzia sasa hadi Desemba, 2017 ili kuweza kumudu kuendelea kutoa mgao unaokidhi mahitaji ya chakula na lishe kwa wakimbizi wanaoishi nchini Tanzania. Michael Dunford, mwakilishi wa shirika la WFP nchini Tanzania,amesema shirika hilo haliwezi kuwahudumia ipasavyo wakimbizi hao hadi pale watakapopata fedha. Ikumbukwe raia wengi wa Burundi waliokimbilia nchini Tanzania katika makambi hayo walikimbia nchi yao kutokana na vurugu zilizotokea baada ya rais Pierre Nkurunziza kuwania urais kwa muhula wa tatu. Mgogoro huo umesababisha vifo vya watu zaidi ya 1,000 na maelfu kukimbilia nje ya nchi.

Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.