2017-08-28 09:03:00

Kardinali Parolin; jitahidini kumwona Mwenyezi Mungu kati ya maskini


Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema hawana budi kujibidisha kutambua uwepo wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa maskini na hivyo kuwa tayari kujibu kilio chao kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Wakimbizi na wahamiaji ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa, inayohitaji jibu makini linalofumbatwa katika: ukarimu, kwa kuzingatia haki msingi za binadamu; kwa kuhamasisha na kuwashirikisha wakimbizi na wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani. Falsafa ya ujenzi wa kuta za utengano haina tija wala mashiko katika mchakato wa mshikamano wa kimataifa.

Elimu makini na endelevu ni kati ya changamoto zinazopaswa kuvaliwa njuga na Mama Kanisa ili kuweza kuwajengea uwezo vijana wa kizazi kipya, kukabiliana na changamoto za maisha katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kuna haja kwa wanasiasa kujikita katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili ili kusaidia mchakato wa kuipyaisha jamii hususan katika masuala ya kisiasa. Utandawazi wa mshikamano ni muhimu sana katika kukabiliana na changamoto za ukosefu wa haki na amani ili hatimaye, kukoleza maendeleo endelevu ya binadamu.

Hakuna nchi ambayo inaweza kujidai kwamba, inaweza kujitosheleza yenyewe kwani Jumuiya ya Kimataifa inategemeana na kukamilishana na kwamba, Marekani na Umoja wa Ulaya wana dhamana na wajibu mkubwa wa kulinda na kudumisha haki na amani duniani! Huu ni muhtasari wa mawazo makuu yaliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi, tarehe 26 Agosti 2017 katika hotuba yake kwenye kilele cha Mkutano wa urafiki kati ya watu nchini Italia unaofanyika kila mwaka na ambao sasa umeingia katika awamu yake ya XXXVIII.

Hii imekuwa ni fursa makini ya kutafakari na kupembua mambo msingi yanayorutubishwa katika maisha ya kila siku, ambayo wakati mwingine, hayapewi uzito unaostahili. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa ufunguzi wa mkutano huu, aliwataka wajumbe kuondokana na Ugonjwa wa Ukosefu wa Kinga za Maisha ya Kiroho Mwili kwa kufanya mambo kwa mazoea!

Kardinali Parolin anafafanua kwamba, Mama Kanisa mwezi Oktoba, 2018 ataadhimisha  Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Hii ni nafasi ya pekee kwa Maaskofu, kuwasikiliza vijana kwa makini ili hatimaye, Kanisa liweze kuibua mbinu mkakati wa utume kwa vijana wa kizazi kipya, kwa kuwekeza zaidi katika elimu makini na endelevu. Ni dhamana na wajibu wa Kanisa kuhakikisha kwamba, hata vijana wa kizazi kipya wanarithishwa imani, maadili na utu wema, kwa kumwachia Mwenyezi Mungu kuchukua nafasi ya kwanza katika maisha ya vijana, ili waweze pia kuongozwa na Roho Mtakatifu.

Jambo la msingi ambalo jamii inapaswa kujiuliza ni urithi gani ambao inataka kuwarithisha na kuwaachia vijana wa kizazi kipya kama amana na utajiri kwa siku za usoni? Vijana wajengewe uwezo wa kuunda familia na jamii inayojikita katika uhuru wa watoto wa Mungu unaowajibisha. Vijana wajengewe dhamiri nyofu ili kutambua mema wanayopaswa kuzingatia na mabaya kuwekwa pembeni. Vijana wanayo kiu ya haki, amani, ustawi na maendeleo! Wanapaswa kusaidiwa ili wasitumbukizwe katika ghasia, fujo na mipasuko ya kijamii. Vijana wawe ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo na mshikamano.

Kardinali Pietro Parolin anaendelea kufafanua kwamba, katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kuna haja ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano unaofumbatwa katika kanuni ya auni; kwa kuwajibika kila mmoja kadiri ya nafasi na dhamana yake. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutambua kwamba, inategemeana na kukamilishana katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Matatizo na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo zina athari zake katika maisha ya watu kitaifa na kimataifa. Mfano mzuri ni myumbo wa uchumi ambao umekuwa na athari zake kitaifa na kimataifa. Kwa bahati mbaya sana, kuna baadhi ya wanasiasa wanaotaka kujipatia umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko kwa kuwahamasisha watu kujitenga

Kumbe, kuna haja kwa wanasiasa wakristo kutekeleza dhamana na wajibu wao utakaosaidia kumwilisha tunu msingi za Kiinjili mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa, kama sehemu ya mchakato wa kupyaisha jamii mamboleo. Wanasiasa wawe ni mashuhuda wa Injili ya upendo inayomwilishwa katika haki, amani, demokrasia, ili kujenga na kudumisha amani jamii na utulivu, mambo msingi katika kukoleza maendeleo endelevu ya binadamu!

Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanayo dhamana anasema Kardinali Parolin ya kujenga na kudumisha dunia iliyo bora zaidi. Marekani na Umoja wa Ulaya wanayo dhamana na wajibu mkubwa wa kujenga na kudumisha haki na amani duniani. Jitihada zinapaswa kufanyika ili kuboresha demokrasia katika hatua mbali mbali, ili kudumisha amani na usalama; ustawi na maendeleo ya wengi. Utandawazi unapaswa kudhibitiwa na kuratibiwa katika mambo msingi kwa kuzingatia mafao ya wengi ili kuweza kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Bwana Emilia Guarnieri Rais wa “Mfuko wa Mkutano wa Urafiki Kati ya Watu nchini Italia” katika hotuba yake ya kushukuru na kufunga Mkutano wa urafiki kati ya watu nchini Italia, Jumapili, tarehe 27 Agosti 2017 ametangaza kwamba, mkutano wa XXXIX utafanyika mjini Rimini kuanzia tarehe 19- 25 Agosti 2018 kwa kuongozwa na maneno la Don Giussani “Nguvu zinazoongoza historia ndizo pia zinazomfanya binadamu kuwa na furaha”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.