Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Imani ya Kanisa inasimikwa katika ushuhuda makini wa Mitume wa Yesu

Imani ya Kanisa kuhusu Yesu Mwana wa Mungu aliye hai imesimikwa katika mwamba thabiti wa ushuhuda na mafundisho ya Mitume wa Yesu. - AP

26/08/2017 07:00

Nasadiki kwa Bwana mmoja Yesu Kristo, Mwana wa pekee wa Mungu. Aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, Mwanga kwa Mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli. Aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Aliyepaa mbinguni, atakują tena kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Hii ndiyo siri ambayo Yesu aliwaonya mitume wake wasiitangaze mapema, lakini leo sisi tunaona fahari kuitangaza na kuiungama kama sehemu ya Kanuni ya Imani inayosimikwa katika msingi wa Mitume wa Yesu na kwa namna ya pekee kwake Petro Mtakatifu aliyepewa ufunguo wa maadili na imani kwa ajili ya Kanisa la Kristo.

Petro ni mwamba, ambaye juu yake, Kristo amejenga Kanisa lake. Hata leo hii, Kristo Yesu anataka kulijenga Kanisa lake katika sakafu ya moyo wako unaosheheni imani thabiti kwamba, Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu aliye hai! Waswahili husema eti kazi yako ndilo jina lako. Ushuhuda wa maisha ya Yesu, mahubiri yake juu ya Ufalme wa Mungu pamoja na miujiza aliyowatendea watu: kiroho na kimwili; ni matukio yanayowapatia watu mbali mbali fununu juu ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Lakini, leo hii swali la msingi ambalo linaulizwa na Kristo Yesu ni: Je, watu wanasema mimi ni nani? Wewe unasema Kristo ni nani kwako? Ni swali nyeti na tete linalohitaji majibu makini yanayofumbatwa katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo yenye mvuto na mashiko!

Baada ya kuadhimisha Fumbo la Maisha ya Kristo: kwa kusherehekea Siku kuu ya Noeli; kwa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake; kupaa kwake mbinguni, ambako ameketi mkono wa kuume wa Baba yake wa milele, atakują tena kuwahukumu wazima na wafu na kwamba, Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Jumapili ya XXI ya Mwaka wa Kanisa, Kristo Yesu anaibuka na swali msingi, Je, watu wanasema kuwa mimi ni nani? Hili ni swali linalopaswa kujibiwa na watu ambao sasa wanamfahamu kwa kiasi kikubwa kuwa kweli Yesu ni nani?

Katika pita pita yangu, nikamuulizia kijana ikiwa kama kweli alikuwa anamfahamu Yesu kuwa ni nani? Akasema, kwa vijana wa kizazi kipya, Kristo Yesu anaweza kufananishwa na wachezaji mashuhuri wa Mpira wa miguu, ambao wakiingia uwanjani wanatandaza kabumbu, kiasi cha kuwafanya watu kukosa usingizi! Kumbe, kwa vijana wa kizazi kipya, Yesu ni mshambuliaji hatari sana katika maisha ya watu: kiroho na kimwili. Ni mchezaji mashuhuri aliyekuwa na umati mkubwa wa mashabiki. Ni mchezaji aliyebarikiwa sana kwa kuhubiri, kuponya, kuwalisha na kuwanywesha watu wakati wa shida. Ni mshambuliaji aliyekuwa na jicho la pekee la kuweza kuona mwanya na kuutumia kikamilifu.

Majibu haya ya vijana wa kizazi kipya yana ukweli ndani yake, lakini, nilitaka kujiridhisha kwa kuwauliza wanasiasa waliobobea na wanaharakati, ambao sehemu kubwa ya maisha yao wanaitumia kwenye majukwaa na hata pengine mahabusu! Wao wanasema, Kristo Yesu ni Nabii mashuhuri sana! Ni mwana harakati; ni mwana mapinduzi ambaye alipenda kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwatetea wanyonge na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii! Alikuwa ni sauti ya wanyonge na mtetezi mkubwa wa haki msingi za binadamu. Alikazia kwa namna ya pekee: haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati; mambo yanayovaliwa njuga na wanasiasa, wanaharakati na wana mapinduzi sehemu mbali mbali za dunia. Ni Nabii aliyesimamia mchakato wa ujenzi wa haki jamii. Hata hapa kuna chembe ya ukweli kuhusu Yesu!

Kwa wasomi na wanazuoni ambao pengine hawaoni tena sababu ya kwenda Kanisani, wanadiriki kusema, Kristo Yesu alikuwa ni kati ya wanafalsafa waliobobea kwa nyakati zake katika kufikiri na kutenda. Alikuwa na mawazo tete hata wakati mwingine wafuasi walishindwa kumfuasa hasa pale alipokuwa anazungumzia kuhusu: Fumbo la Msalaba, Ekaristi Takatifu na Hekalu ambalo angeweza kulivunja na kulijenga kwa siku tatu! Jambo ambalo haliwezi kumwingia mtu wa kawaida kabisa! Yote haya ni majibu yaliyotolewa na watu wa kawaida ambao hawakuwa na nafasi ya kutembea na Kristo katika maisha yao, kwa ukaribu zaidi.

Yesu anawauliza Mitume, Je, Yeye ni nani kwao! Ikumbukwe kwamba, hawa ni wale aliowateuwa kumsindikiza katika maisha na utume wake; watu waliobahatika kufunuliwa siri za mbinguni; mashuhuda wa matendo makuu ya Mungu katika maisha ya watu; mambo yaliyotendwa na Kristo Yesu, kwa kuwaondolea watu dhambi zao; kuwaganga na kuwaponya magonjwa na shida zao mbali mbali. Yesu akadhihirisha kuwa ni mchungaji mwema, kimbilio la maskini na wanyonge, shuhuda wa ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu wote. Yesu alikuwa ni bandari ya matumaini kwa wale waliokata tamaa.

Petro mtume kwa niaba ya mitume wengine wote anakiri muhtasari wa Kanuni ya Imani: ”Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai” na Yesu anamwambia Petro”Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu”. Hii ndiyo siri ambayo, leo Mama Kanisa anaona fahari kuitangaza na kuiadhimisha. Yesu ni Mwana wa Mungu aliye hai: Ni Mungu kati pamoja na watu wake. Hii ndiyo ile imani iliyoshuhudiwa hata na Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali waliomtolea Yesu zawadi ya: Uvumba au ubani unaonesha Umungu wa Kristo; Dhahabu ni kielelezo cha Ufalme wa Kristo na Manemane ni ufunuo wa Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo. Hili ndilo chimbuko la imani ya Kanisa inayosimikwa kwenye msingi wa Mitume wa Yesu.

Hadi kufikia hapa, ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, utakuwa sasa na uhakika wa kujibu swali la msingi lililoulizwa na Kristo Yesu kuwa wewe unasema kuwa Yesu ni nani katika maisha yako? Leo, tujitaabishe tena kurudia Kanuni ya Imani, ili tuweze kuimwilisha katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa wale watu wanaotuzunguka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

26/08/2017 07:00