Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Amani

Askofu Kussala: Familia ya Mungu Sudan ya Kusini ina kiu ya amani!

Familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini ina kiu ya amani ya kudumu. - AFP

25/08/2017 12:03

Vita ya wenyewe kwa wenyewe, ghasia na mpasuko wa kisiasa na kijamii; kushindwa kutekelezwa kwa Mkataba wa Amani Sudan ya Kusini, baa la njaa na ukame wa kutisha ni kati ya mambo yanayoendelea kuwaandama wananchi wa Sudan ya Kusini. Hii ni vita inayofumbatwa katika ukabila usiokuwa na mashiko wala mvuto kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Sudan ya Kusini. Ubinafsi na uchoyo wa baadhi ya viongozi kutaka kujitajirisha wao wenyewe na familia zao, walakini ambako bado kuna umati mkubwa wa familia ya Mungu nchini Sudan inayohitaji maendeleo endelevu ni jambo linalotia uchungu mkubwa kwa wapenda maendeleo wengi.

Inasikitisha kuona kwamba, viongozi wamesahau kwamba, uongozi ni huduma na wala si kichaka cha kutimizia tamaa ya utajiri wa haraka haraka. Haya ni masikitiko makubwa ambayo yameoneshwa na Askofu Edward Hiiboro Kussala, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan. Anakaza kusema, utajiri na rasilimali za nchi ambazo ndicho chanzo kikuu cha ghasia, kinzani na vita unapaswa kutumiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Sudan ya Kusini na wala si kwa ajili ya watu wachache ndani ya jamii.

Baba Mtakatifu Francisko na viongozi wengine wa Makanisa, walionesha utashi wa kutembelea Sudan ya Kusini katika kipindi cha Mwaka 2017, lakini zoezi hili limehairishwa hadi hapo itakapotangazwa tena! Lakini, familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini, imeonja wema na ukarimu wa kibaba ulionesha na Baba Mtakatifu Francisko kwa kugharimia miradi mbali mbali inayopania kuwajengea watu matumaini mapya! Bado wanaendelea kusali ili kwamba, siku moja, Baba Mtakatifu Francisko kwa mapenzi yake Mwenyezi Mungu ataweza kutembelea Sudan ya Kusini, ili kuwatia shime ndugu zake katika Kristo!

Askofu Edward Hiiboro Kussala anasikitika kusema kwamba, madhara ya vita yanajionesha na kuwagusa wananchi wote wa Sudan ya Kusini, hata kama ni kwa viwango tofauti. Watu hawana uhakika wa usalama wa chakula, dawa na mahitaji msingi. Msimamo wa Kanisa Katoliki nchini Sudan ya Kusini ni kuendeleza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Kanisa ni sauti ya kinabii inayotekeleza dhamana na utume wake kwa kuzingatia nguvu ya kimaadili.

Viongozi wa Serikali na wapinzani, daima wako tayari kusikiliza ushauri unaotolewa na viongozi wa Kanisa, lakini kwa bahati mbaya, ni wagumu sana kuweza kumwilisha ushauri huu katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vya watu! Kanisa litaendelea kuwa ni chombo na shuhuda wa amani, kwa kuwaalika wananchi wote wa Sudan ya Kusini kujikita katika majadiliano ili amani, usalama, ustawi na maendeleo ya wengi viweze kuanza kushika mkondo wake. Kanisa linawataka vijana kutokubali kutumiwa na wajanja wachache kuvuruga amani na usalama wa raia. Kanisa linaendelea kutoa huduma za kijamii hasa katika sekta ya afya, chakula na mahitaji msingi, kwani wakati wa vita na ghasia, Serikali inaonekana kana kwamba, imekwenda likizo.

Askofu Edward Hiiboro Kussala anasema, umefika wakati wa kusitisha mapigano na kuanza kujikita katika majadiliano kwa ajili ya ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Sudan ya Kusini. Wafadhili wamechoka sasa kuendelea kuwahudumia watu wasiotaka kupatana, tayari kuanza kuandika ukurasa mpya wa historia na maisha yao! Kanisa litaendelea kuwa ni kimbilio la wanyonge na maskini; litaendelea kuacha milango ya majengo na taasisi zake kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu kwa matumaini kwamba, iko siku amani itaweza kurejea tena nchini Sudan ya Kusini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

25/08/2017 12:03