2017-08-24 11:33:00

Patriaki Cyril wa Russia asema, Makanisa yamefungua ukurasa mpya!


Wakristo wa Makanisa ya Kiorthodox na Kikatoliki, wanapaswa kushikakama katika uekumene wa huduma makini kwa maskini na wale wote wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali sanjari na kujenga amani duniani. Hii ndiyo safari ya kiekumene inayopaswa kutekelezwa na Makanisa haya mawili, ili kujenga na kudumisha umoja na amani. Huu ndio ujumbe mzito uliotolewa na Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Russia nzima, alipokutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumanne, tarehe 22 Agosti 2017.

Kardinali Parolin amewasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa Patriaki Cyril ambaye ameyapokea kwa moyo wa shukrani. Hali tete, nyanyaso na dhuluma dhidi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati na mateso na mahangaiko ya familia ya Mungu nchini Ukraine ni kati ya mada kubwa zilizogusiwa na viongozi hawa wawili walipokutana kwenye monasteri ya Danlov, huko Moscow. Wanasema, kuna haja kwa Makanisa kushikamana kwa dhati ili kuwasaidia na kuwahudumia Wakristo huko Mashariki ya kati.

Mchakato huu, hauna budi kusimikwa katika harakati za kujenga na kudumisha umoja wa Makanisa katika ngazi ya hali ya juu kabisa. Uekumene wa huduma kwa Wakristo huko Mashariki ya Kati unao mchango mkubwa katika kujenga na kudumisha umoja wa Wakristo duniani anasema Patriaki Cyril. Umoja huu unaweza pia kuvaliwa njuga na Makanisa hata katika mazingira tete ya vita, ghasia na mipasuko ya kijamii huko nchini Ukraine. Katika mazingira kama haya, dhamana, wajibu na utume wa Makanisa ni kujitahidi kujenga amani na utulivu kati ya watu. Ikumbukwe kwamba, vita na ghasia si mambo yanayodumu nyakati zote, iko siku itakoma na ghasia kutulia! Makanisa yasaidie mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano wa dhati.

Patriaki Cyril na Kardinali Pietro Parolin wanasema, mazungumzo haya ni mwanzo mpya wa mahusiano kati ya Kanisa la Kiorthodox na Kanisa Katoliki. Mwanzo wa safari hii yenye matumaini ni mkutano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Cyril huko Havana, Cuba, mwezi Februari 2016 na hatimaye, viongozi hawa wawili wakatia mkwaju kwenye kile kinachojulikana kama “Tamko la Havana, Cuba” linaoonesha ushirikiano wa kiekumene kati ya Makanisa haya mawili.

Umoja huu umeendelea kuimarishwa kwa hija ya masalia ya Mtakatifu Nicholaus wa Bari mjini Moscow na huko San Peterburg, jambo ambalo limewawezesha wakristo wengi kutoa heshima na kuonesha ibada yao kwa Mtakatifu Nicholaus wa Bari. Patriaki Cyril anasema, kwa hakika hili limekuwa ni tukio la kihistoria kati ya Makanisa haya mawili. Kardinali Parolin anakaza kusema, huu ni uekumene wa utakatifu wa maisha, unaowawezesha waamini kuungana kwani watakatifu hawa wako karibu sana na Mwenyezi Mungu, hivyo kwa njia ya sala na maombezi yao wanawasaidia waamini katika shida na magumu ya maisha yao, daima wakiendelea kujizatiti ili siku moja waweze kuadhimisha pamoja Fumbo la Ekaristi Takatifu. Viongozi wakuu wa Makanisa haya wanaendelea kuonesha utashi wa kutaka kushirikiana kwa karibu zaidi, ili kuimarisha na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika uhalisia wa maisha ya watu. Makanisa yote mawili yanajiweka chini ya ulinzi na tunza ya Roho Mtakatifu ili aweze kuyaongoza kadiri ya matakwa yake. Kardinali Pietro Parolin amewasilisha pia zawadi ya Baba Mtakatifu kwa Patriaki Cyril ambaye pia amemzawadia Baba Mtakatifu kitabu cha “Uhuru na Uwajibikaji”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.