2017-08-24 12:37:00

Parokia ya Kiabakari na mchakato wa kumwilisha huruma ya Mungu


Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Kiabakari sanjari na uzinduzi wa ukarabati wa Hekalu la Huruma ya Mungu ni tukio ambalo lilipambwa kwa ustadi mkubwa wa maandalizi ya maisha ya kiroho kwa njia ya semina na mafungo. Itakumbukwa kwamba, Parokia ya Kiabakari ni sehemu ya matunda ya juhudi na mchakato wa uinjilishaji Jimboni Musoma, katika kipindi cha Miaka 60 iliyopita kama ulivyofafanuliwa kwa kina na mapana na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma katika Barua yake ya Kichungaji inayoongozwa na kauli mbiu “Upendo kwa utume”.

Waamini wamejiandaa kikamilifu, ili kukamilisha ile hija ya maisha ya kiroho iliyoanzishwa na Roho Mtakatifu miaka 25 iliyopita, akawaongoza, akawategemeza na hatimaye, kumwilisha ndoto ya ujenzi wa Hekalu la Huruma ya Mungu, mahali ambapo waamini wanaweza kutakaswa, kushukuru na kuadhimisha matendo makuu katika maisha yao, daima wakiwa tayari kumwimbia Mwenyezi Mungu huruma yale ambayo inadumu milele! Kauli mbiu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Kiabakari yalikuwa ni “Tutakase na tutakatifuze; tukushukuru na kukuadhimisha”.

Askofu Michael Msonganzila, tarehe 19 Agosti 2017 ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini 200. Hili ni tukio ambalo lilitanguliwa na mafungo ya maisha ya kiroho, kwa kupokea Sakramenti ya Upatanisho, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu. Ilikuwa ni nafasi muhimu sana kwa familia ya Mungu, Parokia ya Kiabakari kujitakasa ili iweze kutakatifuzwa. Askofu Michael Msonganzila anasema, kwa hakika, Mapaji ya Roho Mtakatifu yanaonekana katika uhalisia wa maisha ya waamini.

Jumapili, tarehe 20 Agosti, 2017 ilikuwa ni “Siku ya kushukuru na kuadhimisha” (1992 – 2017) kilele cha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Kiabakari sanjari na uzinduzi wa ukarabati wa Hekalu la Huruma ya Mungu. Ukarabati huu, unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 44, ili kuweza kupyaisha na kurejesha ile sura ya Hekalu la Huruma ya Mungu iliyokuwepo miaka 20 iliyopita, lakini kwa wakati huu, ikiwa imeboreka zaidi. Katika kilele hiki, familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Parokia ya Kiabakari ilichangia fedha taslimu kiasi cha shilingi 534, 150, 000 pamoja na mifuko 10 ya saruji.

Askofu Msonganzila kwa kuguswa na huruma pamoja na ukarimu wa Mungu kwa watu wa Musoma, amechangia mifuko 100 ya saruji pamoja na kuungwa mkono na waamini kwa mifuko mingine 54. Hii ni sawa na asilimia 10 ya gharama zote za ukarabati hadi kufikia siku hiyo! Padre Wojciech Adam Koscielniak, Paroko wa Parokia ya Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma katika risala yake kwa Askofu Michael Msonganzila anasema dhima ya kichungaji iliyowaongoza kwa miaka 25 iliyopita ilikuwa ni kumwandalia Mwenyezi Mungu Aliye Mwingi wa Huruma mahali ambapo Huruma yake, itaweza kumpenyeza mwanadamu, kumgusa na kumbadilisha kiroho, kimwili na kiakili. Wakajenga Hekalu la Huruma ya Mungu, Kituo cha Afya, Shule ya awali na Shule ya msingi. Wakawakaribisha Watawa wa Shirika la Watumishi Wadogo wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa kwa familia ya Mungu, Parokiani Kiabakari na hatimaye, wakaweka Lango la Huruma kwa watu wote waitafutayo Huruma ya Mungu na Rehema zake. Jubilei ni tukio la kumshukuru Mungu aliyefanikisha historia, maisha na utume wa Parokia ya Kiabakari kwa kuwatumia wanadamu wadhaifu na wenye mipaka na mapungufu mbalimbali.

Ndiyo maana, Jubilei pia ni kipindi cha kuomba toba, msamaha na neema ya kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi; kwa kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Roho Mtakatifu. Wanataka kusonga mbele na kumwomba Mwenyezi Mungu mwenye Huruma Kituo cha Hija hiki kitangazwe siku moja kuwa Kituo cha Kitaifa cha Hija ya Huruma ya Mungu na kiendelee kulitumikia Taifa la Mungu nchini Tanzania na Afrika Mashariki katika ujumla wake. Wanataka kuthubutu kuboresha huduma za kiroho na za kichungaji zinazotolewa Parokiani na vigangoni - hasa katika utume wa ndoa, familia takatifu na katika JNNK na vyama vya kitume. Wanataka kuthubutu kulea miito mbalimbali katika Parokia yao, hususan miito ya upadre, utawa, ukatekista na ndoa takatifu na kwamba wanataka kuthubutu kuboresha huduma ya afya itolewayo hapo Kiabakari. Wanataka kuthubutu kuzaa Parokia mpya ya Muganza; kuitegemeza Parokia kwa moyo wa ukarimu na sadaka, ili kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kuboresha mazingira, nyumba ya wote pamoja na kuwahudumia akina mama wanaolea familia zao binafsi.

Askofu Michael Msonganzila alipata bahati pia ya kubariki na kutoa zawadi ya baiskeli nane kwa ajili ya huduma kwa makatekista vijijini. Alibariki gari ya shughuli za huduma za kichungaji Parokiani Kibakari, ukiwa ni msaada kutoka kwa MIVA, Poland. Jubilei hii ilipambwa pia na uwepo wa Bendi ya Watoto wenye ulemavu wa ngozi kutoka katika Kituo cha Kulelea Watoto Walemavu cha Bikira Maria Mama wa Msaada wa Daima.

Ifuatayo ni risala kutoka kwa Padre Wojciech Adam Koscielniak, Paroko wa Parokia ya Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma, iliyosomwa kama sehemu ya utangulizi kwa ajili ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Kiabakari sanjari na uzinduzi wa ukarabati wa Hekalu la Huruma ya Mungu. Kwa niaba ya wanaparokia wote wa Kiabakari, marafiki zetu kote duniani na wageni waalikwa wote waliokusanyika mahali hapa patakatifu siku hii ya leo, natoa shukrani zetu za dhati kwako kwa kukubali kuongoza Ibada hii Takatifu ya Misa ya kumshukuru Mungu Aliye Mwingi wa Huruma na kumwadhimisha kwa Maongozi yake ya Ajabu kwa robo karne iliyopita tangu kuzaliwa kwa Parokia hii ya Kiabakari hadi leo. Asante sana, Baba!

Tarehe 26 Januari 1992, miaka 25 iliyopita, Mtangulizi wako, Hayati Askofu Justin Samba aliadhimisha Misa ya Kipaimara mahali hapa ndani ya kanisa la zamani la kigango cha Kiabakari na kuweka jiwe la msingi la makao makuu  ya Parokia tarajiwa ya Kiabakari. Tarehe 28 Julai mwaka huo wa 1992 Mhashamu Askofu Mkuu Agostino Marchetto alibariki makao makuu ya Parokia na Hayati Mhashamu Baba Askofu Justin Samba alitangaza kuzaliwa kwa Parokia ndogo ya Kiabakari.

Tarehe 3 Julai 1997, miaka 25 iliyopita, Hayati Mhashamu Baba Askofu Mkuu Anthony Mayala alitabaruku kanisa la kiparokia la Mwenye Heri Petro George Frassati na Mtakatifu Gemma Galgani, na Hayati Mhashamu Baba Askofu Justin Samba alitangaza kuzaliwa kwa Parokia kamili ya Parokia na kumteua Paroko wake wa kwanza. Tarehe 17 Agosti 2001 mbele ya Mhashamu Baba Askofu Mkuu Luigi Pezzuto, Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania wakati ule, Hayati Mhashamu Baba Askofu Justin Samba alipandisha hadhi ya kanisa hili la kiparokia na kulitangaza kuwa Kituo cha Kijimbo cha Hija cha Huruma ya Mungu.

Dhima ya kichungaji iliyotuongoza kwa miaka 25 yote iliyopita ilikuwa ni kumwandalia Mwenyezi Mungu Aliye Mwingi wa Huruma mahali ambapo Huruma yake itaweza kumpenyeza mwanadamu, kumgusa na kumbadilisha kiroho, kimwili na kiakili. Tulijenga Hekalu la Huruma ya Mungu, tukajenga Kituo cha Afya, tukajenga shule ya awali na shule ya msingi. Tukakaribisha Watawa wa Shirika la Watumishi Wadogo wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Tukaweka Lango la Huruma kwa watu wote waitafutayo Huruma ya Mungu na Rehema zake.

Leo tumekusanyika hapa ili tuweze kumshukuru Mungu Mwenyezi Mwenye Huruma isiyo na mipaka kwa neema na baraka zote tulizopokea katika miaka yote hiyo 25. Tumekusanyika ili tumwadhimishe kwa nafsi zetu zote maana “kwake hakuna lisilowezekana’ na ndiye Mungu pekee aliyefanikisha historia ya Parokia yetu kwa kuwatumia wanadamu wadhaifu na wenye mipaka na mapungufu mbalimbali. Tukitazama muhtasari wa historia ya Parokia yetu mliyogawiwa nyote katika karatasi yenye picha za hatua kuu za kukua kwa Parokia ya Kiabakari, hatuna budi kukubali kwamba ni Mungu pekee aliyewezesha yote haya myaonayo kuwepo. Ndiyo maana tupo hapa leo ili kwa pamoja tuweze kumwambia - Baba wa Huruma, asante! Pamoja na hayo, tukikumbuka maneno ya Mtakatifu Paulo, Mtume wa Mataifa - “Maana ni kweli, wewe washukuru vema, bali yule mwingine hajengwi.” (1 Kor 14:17) - hatutaki kubaki katika tendo la shukrani na ibada ya kumwadhimisha Bwana.

Tunatazama mbele kwa matumaini, tukijua kwamba Bwana alituongoza kwa miaka yote 25 katika taabu na raha, magonjwa na afya na kutufikisha salama hadi hapa tulipo. Na kwa sababu hiyo, tunataka kusonga mbele na kuendelea kujenga Parokia yetu kadiri ya Mapenzi na Maongozi Matakatifu ya Mungu mwenye Huruma  isiyo na mipaka. Tunashukuru leo lakini shukrani yetu inaambatana na tendo la ukarimu la kuunga mkono kazi za kimaendeleo, hususan ukarabati wa Kanisa letu hili la kiparokia lipate kurudi kwenye hali iliyokuwa nayo siku ya kutabarukiwa kwake, na hata kuiboresha hali zaidi na zaidi. Hatutaki kubaki kutazama nyuma na kupongezana tu kwa mafanikio ya miaka 25 iliyopita. Hapana! Tunataka kusonga mbele na kumwomba Mungu mwenye Huruma Kituo cha Hija hiki kitangazwe siku moja kuwa Kituo cha Kitaifa cha Hija cha Huruma ya Mungu na kiendelee kulitumikia Taifa la Mungu la Tanzania na la Afrika Mashariki.

Tunataka kuthubutu kuboresha huduma za kiroho na za kichungaji zinazotolewa Parokiani na vigangoni - hasa katika utume wa ndoa, familia takatifu na katika JNNK na vyama vya kitume. Tunataka kuthubutu kulea miito mbalimbali katika Parokia yetu, hususan miito ya upadre, utawa, ukatekista na ndoa takatifu. Tunataka kuthubutu kuboresha huduma ya afya itolewayo hapa Kiabakari - kukamilisha chumba cha upasuaji na mitambo yake, kujenga mortuary, kuanzisha idara zitakazolenga moja kwa moja matatatizo ya kiafya yanayosumbua wananchi wetu zaidi - physiotherapy, cardiology, magonjwa ya akina mama n.k. Tunakaribia kukamilisha mchakato wa kununua gari la wagonjwa kwa ajili ya Kituo cha afya.

Tunataka pia kuthubutu kuboresha taasisi zetu za kielimu Parokiani - kukamilisha viwanja vya michezo, kukamilisha darasa la kompyuta, kununua mabasi ya shule na kadhalika. Katika miaka 25 ijayo tunataka kuthubutu kuzaa Parokia mpya ya Muganza katika siku za usoni Mungu akipenda kwa kutenga vigango vitatu vilivyoko kusini mwa Parokia yetu - Nyamikoma, Mwibagi na Nyakiswa.  Tunataka kutegemeza Parokia yetu kwa ukarimu mkubwa na kuifikisha katika hali ya kujitegemea na hata kutegemeza Parokia nyingine maskini zaidi kwa kubuni na kusimamia miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kuanzisha vitega uchumi mbalimbali. Tunataka kuthubutu kumlinda na kumhudumia mwanadamu kiroho, kimwili na kiakili na kutunza na kuboresha mazingira tunamoishi - vyanzo vya maji, misitu, hali ya hewa, kilimo na ufugaji kadiri ya mabadiliko ya tabia nchi - kwa semina, kozi, warsha na elimu endelea ya wananchi na kwa namna ya pekee ya akina mama wanaolea familia zao peke yao (single mothers).

Ndiyo maana siku hii ya kuadhimisha pamoja nawe, Baba, Jubilei ya Miaka 25 ya kusafiri pamoja katika njia za Bwana kama Familia yake ya wanaparokia ya Kiabakari, twasimama mbele zake Bwana na mbele yako, Mpendwa Baba Askofu, na kutamka kwa madhubuti na kwa uhakika maneno ya Mfalme Daudi katika Zaburi ya 37: "Umtumaini Bwana ukatende mema, Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu. Nawe utajifurahisha kwa Bwana, Naye atakupa haja za moyo wako. Umkabidhi Bwana njia yako, Pia umtumaini, naye atafanya.” (Ps 37:3-5) Mikononi mwako, Mhashamu Baba Askofu, tunaweka njia zetu zote, njozi zetu zote, mipango yetu yote na malengo yetu yote. Tunaomba uviunganishe na sadaka ya Bwana altareni. ili Yeye afanye atakavyo kadiri ya haja za mioyo yetu na kadiri ya Maongozi yake Matakatifu. Tunakuomba sasa, Mpendwa Baba, utuongoze katika Ibada hii Takatifu ya shukrani na ya matumaini. Asante.

Risala ya Wanakipaimara wa Parokia ya Kiabakari  kwa Mhashamu Baba Askofu Michael Msonganzila, Askofu wa Jimbo la Musoma.

Hekalu la Huruma ya Mungu, Parokia ya Kiabakari, 19 Agosti 2017

Mhashamu Baba Askofu,

Tumsifu Yesu Kristo!

Sinodi Musoma! Imani na Matendo!

Mpendwa Baba Askofu, awali ya yote tunakupa pole kwa kufiwa na Mama yako Mzazi Mpendwa Mama Tecla! Pole sana sana, Mpendwa Baba! Tuko pamoja nawe katika majonzi na katika sala za kumuombea Mama yetu Mzazi ili Mungu mwenye Huruma nyingi ampokee katika Makao yake ya Milele mbinguni! Aidha, tunakupa pole, Mpendwa Baba kwa uchovu wa shughuli na safari mbalimbali za kichungaji, zikiwemo shughuli za kuongoza mchakato mzima wa utekelezaji wa matamko na maazimio ya Sinodi ya Jimbo letu la Musoma pamoja na Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 60 ya Jimbo letu la Musoma.

Tunakupongeza kwa dhati kwa wazo la kuitisha Sinodi ya Jimbo la Musoma, tunakupongeza kwa mafanikio ya Sinodi na tunakuombea wewe binafsi pamoja na Jimbo zima mafanikio makubwa katika utekelezaji wa maazimio na matamko ya Sinodi na ya Jubilei ya Jimbo la Musoma. Sisi tunakuahidi ushirikiano wa dhati. Tuko pamoja nawe, mpendwa Baba! Tunafahamu kuwa unayo majukumu ya kitume mengi sana; ni kazi ngumu sana inayohitaji moyo mkuu wa kujituma na uvumilivu mwingi, lakini kazi yote hiyo umeimudu kwa ujasiri mkubwa na kwa namna ya pekee kwa maongozi ya Roho Mtakatifu. Pamoja na majukumu makubwa ya kitume uliyo nayo, Mhashamu Baba Askofu, hata hivyo umekubali kwa moyo wa upendo wa dhati ombi letu la kufika kwetu Kiabakari kuongoza maadhimisho ya leo ya Sherehe ya Pentekoste mpya katika Parokia yetu  na kutuimarisha kwa Sakramenti ya Kipaimara na kuungana na wanaparokia wote katika Adhimisho la Jubilei ya Miaka 25 ya Parokia yetu ya Kiabakari. Asante sana, mpendwa Baba!

Mpendwa Baba, tunakushukuru sana kwa kutuimarisha sisi wanakipaimara kwa karama za Roho Mtakatifu na kutupa jukumu la kulijenga Kanisa kama wakristo wazima, mashahidi wa Bwana katika ulimwengu wa kisasa, Mitume wa Huruma yake na wafuasi waaminifu wa Bwana wanaojenga maisha yao ya kikristo ya kila siku juu ya mwamba wa sala na maisha ya kisakramenti na matendo ya upendo na huruma. Leo kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara umetutuma rasmi tuungane na waamini wenzetu kutoa ushuhuda wa imani yetu hai na kuwafanya wengine kuwa wanafunzi wa Bwana na kushirikiana kutekeleza maazimio na matamko ya Sinodi ya Jimbo letu la Musoma. Baba, tunakuhakikisha kwamba tutafanya hivyo na tuko pamoja nawe na wanajimbo  wenzetu wote.

Mhashamu Baba Askofu, Hatupendi kuongea mengi na kukuongezea uchovu zaidi, bali tunapenda tukuhakikishe kwamba tunakuombea kila siku katika Kituo hiki cha Kijimbo cha Hija, hasa kila Ijumaa tunapokuwa na mafungo yetu na siku ya Bwana tunapokuwa wote kama familia ya Watoto wa Mungu nyumbani mwa Bwana humu na kukutaja katika Kanuni ya Misa na kukulinda kwa upendo na sala zetu.

Tunakuomba sasa, Mpendwa Baba, kama alama ya upendo wetu na shukrani za dhati kwako kwa huduma takatifu uliyoitoa leo, upokee shukrani yetu ya Kipaimara kiasi cha shilingi za Kitanzania ….! Aidha, kwa niaba ya wanaparokia wote wa Kiabakari tunaomba upokee salamu zetu za rambirambi kiasi cha Tshs 300,000/= kwa ajili ya msiba mkubwa wa Mama yetu Mpendwa Tecla.  Tunawashukuru pia walimu wetu kwa kutuandaa vema kwa siku takatifu hii ya leo; tunawaomba pia wapokee zawadi ndogo kutoka kwetu. Sisi, wanakipaimara wa Kiabakari, twasema sote – Mpendwa Baba, asante sana na Mungu akubariki daima! Karibu tena Kiabakari, nyumbani kwa Mungu Aliye Mwingi wa Huruma!

Wanakipaimara wa Kiabakari wa Darasa la 2017.

Kwa niaba ya Wanaparokia wote wa Kiabakari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.