2017-08-24 11:15:00

Kardinali Parolin akutana na kuzungumza na Rais Putin wa Russia


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatano tarehe 23 Agosti 2017 amekutana na kuzungumza na Rais Vladimir Putin wa Russia katika Ikulu ndogo iliyoko mjini Sochi. Mazungumzo haya yamefanyika katika hali ya amani, utulivu na kusikilizana kwa dhati. Wamejadili kwa kina na mapana masuala na changamoto mamboleo zinazoiandamana Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu. Ameishukuru Serikali ya Russia kwa mapokezi mazito pamoja na kuwasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Kwa upande wake, Rais Putin amekumbushia safari zake mbili za kikazi, zilizomwezesha kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican katika miaka ya hivi karibuni. Kardinali Parolin anaridhishwa na uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Vatican na Russia. Mkataba uliotiwa sahihi kuhusu  wanadiplomasia wa Vatican na Russia kusafiri katika nchi hizi mbili pasi na ulazima wa kuwa na hati ya kusafiria, iliyotiwa mkwaju kati ya Vatican na Serikali ya Russia hapo tarehe 23 Agosti 2017 ni hatua ambayo imepongezwa sana.

Rais Vladimir Putin amepongeza mazungumzo haya kati yake na Kardinali Parolin kwamba, yanasimikwa katika uaminifu, ukweli na uwazi na kwamba, huu ni mwanzo mzuri katika kujenga na kuimarisha uhusiano kati ya Serikali ya Russia na Vatican. Amewapongeza viongozi wa Makanisa kwa kuanzisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene ya moja kwa moja kati yao. Kwa sasa Serikali ya Russia na Kanisa la Kiorthodox linaendelea kutekeleza mambo msingi yaliyofikiwa kati ya Rais Putin na Baba Mtakatifu Francisko katika mazungumzo yao.

Majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa haya mawili, kwa sasa yanachukua uzito wa pekee kabisa na kwamba, ni matumaini ya Serikali ya Russia kwamba, majadiliano haya ya kiekumene yataendelezwa na kudumishwa, ili kuimarisha umoja, ushirikiano na mafungamano ya Makanisa haya mawili. Mkutano kati ya Patriaki Cyril na Baba Mtakatifu Francisko huko Havana, Cuba, ulisaidia kuimarisha msingi wa majadiliano ya kati ya Makanisa haya mawili. Rais Putin, kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Russia amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko aliyetoa kibali cha masalia ya Mtakatifu Nicholaus wa Bari, kwenda kutembezwa nchini Russia na hivyo kuwawezesha waamini zaidi milioni 2.3 kusali na kutoa heshima zao.

Kunako mwaka 2018, Vatican na Russia zitafanya onesho la sanaa kwa pamoja katika Jumba la Makumbusho la Tretyakov, la Moscow, nchini Russia. Rais Putin, ametumia fursa kwa niaba ya wapenda sanaa, kuishukuru Vatican kwa kupenda kukuza na kudumisha urithi wa maisha ya kiroho. Mwishoni mwa mazungumzo yao; Kardinali Pietro Parolin na Rais Vladimir Putin wamebadilishana zawadi kama alama ya kumbu kumbu ya tukio hili la kihistoria. Kardinali Pietro Parolin kuanzia tarehe 20 hadi tarehe 24 Agosti 2017 amekuwa na ziara ya kikazi nchini Russia ambayo imesaidia kuimarisha mchakato wa mahusiano ya kidiplomasia sanjari na uekumene wa sala, maisha ya kiroho, ushuhuda wa damu na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.