2017-08-24 12:16:00

Jubilei ya Miaka 25 ya Parokia ya Kiabakari, sasa inataka kuthubutu!


Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Kiabakari sanjari na uzinduzi wa ukarabati wa Hekalu la Huruma ya Mungu ni tukio ambalo lilipambwa kwa ustadi mkubwa wa maandalizi ya maisha ya kiroho kwa njia ya semina na mafungo. Itakumbukwa kwamba, Parokia ya Kiabakari ni sehemu ya matunda ya juhudi na mchakato wa uinjilishaji Jimboni Musoma, katika kipindi cha Miaka 60 iliyopita kama ulivyofafanuliwa kwa kina na mapana na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma katika Barua yake ya Kichungaji inayoongozwa na kauli mbiu “Upendo kwa utume”.

Waamini wamejiandaa kikamilifu, ili kukamilisha ile hija ya maisha ya kiroho iliyoanzishwa na Roho Mtakatifu miaka 25 iliyopita, akawaongoza, akawategemeza na hatimaye, kumwilisha ndoto ya ujenzi wa Hekalu la Huruma ya Mungu, mahali ambapo waamini wanaweza kutakaswa, kushukuru na kuadhimisha matendo makuu katika maisha yao, daima wakiwa tayari kumwimbia Mwenyezi Mungu huruma yale ambayo inadumu milele! Kauli mbiu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Kiabakari yalikuwa ni “Tutakase na tutakatifuze; tukushukuru na kukuadhimisha”.

Askofu Michael Msonganzila, tarehe 19 Agosti 2017 ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini 200. Hili ni tukio ambalo lilitanguliwa na mafungo ya maisha ya kiroho, kwa kupokea Sakramenti ya Upatanisho, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu. Ilikuwa ni nafasi muhimu sana kwa familia ya Mungu, Parokia ya Kiabakari kujitakasa ili iweze kutakatifuzwa. Askofu Michael Msonganzila anasema, kwa hakika, Mapaji ya Roho Mtakatifu yanaonekana katika uhalisia wa maisha ya waamini.

Jumapili, tarehe 20 Agosti, 2017 ilikuwa ni “Siku ya kushukuru na kuadhimisha” (1992 – 2017) kilele cha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Kiabakari sanjari na uzinduzi wa ukarabati wa Hekalu la Huruma ya Mungu. Ukarabati huu, unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 44, ili kuweza kupyaisha na kurejesha ile sura ya Hekalu la Huruma ya Mungu iliyokuwepo miaka 20 iliyopita, lakini kwa wakati huu, ikiwa imeboreka zaidi. Katika kilele hiki, familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Parokia ya Kiabakari ilichangia fedha taslimu kiasi cha shilingi 534, 150, 000 pamoja na mifuko 10 ya saruji. Askofu Msonganzila kwa kuguswa na huruma pamoja na ukarimu wa Mungu kwa watu wa Musoma, amechangia mifuko 100 ya saruji pamoja na kuungwa mkono na waamini kwa mifuko mingine 54. Hii ni sawa na asilimia 10 ya gharama zote za ukarabati hadi kufikia siku hiyo!

Padre Wojciech Adam Koscielniak, Paroko wa Parokia ya Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma katika risala yake kwa Askofu Michael Msonganzila anasema dhima ya kichungaji iliyowaongoza kwa miaka 25 iliyopita ilikuwa ni kumwandalia Mwenyezi Mungu Aliye Mwingi wa Huruma mahali ambapo Huruma yake, itaweza kumpenyeza mwanadamu, kumgusa na kumbadilisha kiroho, kimwili na kiakili. Wakajenga Hekalu la Huruma ya Mungu, Kituo cha Afya, Shule ya awali na Shule ya msingi. Wakawakaribisha Watawa wa Shirika la Watumishi Wadogo wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa kwa familia ya Mungu, Parokiani Kiabakari na hatimaye, wakaweka Lango la Huruma kwa watu wote waitafutayo Huruma ya Mungu na Rehema zake. Jubilei ni tukio la kumshukuru Mungu aliyefanikisha historia, maisha na utume wa Parokia ya Kiabakari kwa kuwatumia wanadamu wadhaifu na wenye mipaka na mapungufu mbalimbali.

Ndiyo maana, Jubilei pia ni kipindi cha kuomba toba, msamaha na neema ya kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi; kwa kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Roho Mtakatifu. Wanataka kusonga mbele na kumwomba Mwenyezi Mungu mwenye Huruma Kituo cha Hija hiki kitangazwe siku moja kuwa Kituo cha Kitaifa cha Hija ya Huruma ya Mungu na kiendelee kulitumikia Taifa la Mungu nchini Tanzania na Afrika Mashariki katika ujumla wake. Wanataka kuthubutu kuboresha huduma za kiroho na za kichungaji zinazotolewa Parokiani na vigangoni - hasa katika utume wa ndoa, familia takatifu na katika JNNK na vyama vya kitume. Wanataka kuthubutu kulea miito mbalimbali katika Parokia yao, hususan miito ya upadre, utawa, ukatekista na ndoa takatifu na kwamba wanataka kuthubutu kuboresha huduma ya afya itolewayo hapo Kiabakari. Wanataka kuthubutu kuzaa Parokia mpya ya Muganza; kuitegemeza Parokia kwa moyo wa ukarimu na sadaka, ili kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kuboresha mazingira, nyumba ya wote pamoja na kuwahudumia akina mama wanaolea familia zao binafsi.

Askofu Michael Msonganzila alipata bahati pia ya kubariki na kutoa zawadi ya baiskeli nane kwa ajili ya huduma kwa makatekista vijijini. Alibariki gari ya shughuli za huduma za kichungaji Parokiani Kibakari, ukiwa ni msaada kutoka kwa MIVA, Poland. Jubilei hii ilipambwa pia na uwepo wa Bendi ya Watoto wenye ulemavu wa ngozi kutoka katika Kituo cha Kulelea Watoto Walemavu cha Bikira Maria Mama wa Msaada wa Daima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.