Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Kardinali Parolin: Amani ya kudumu inajikita katika haki na sheria!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, amani ya kudumu inasimikwa katika haki, sheria na kanuni msingi zinazoongooza Jumuiya ya Kimataifa. - AP

23/08/2017 09:57

Ili kuweza kuwa na amani ya kudumu, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika haki, sheria na kanuni msingi. Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumanne, tarehe 22 Agosti 2017 wakati alipokutana na kuzungumza na Bwana Sergiey Lavrov, Waziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa nchini Russia. Kardinali Parolin ametumia nafasi hii kuishuruku Serikali ya Russia kwa mwaliko na mapokezi makubwa ambayo wamemkirimia na kwamba, lengo la safari hii ya kikazi ni kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Russia na Vatican zinaridhishwa na uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya nchi hizi mbili: kwanza kabisa kwa uwakilishi wa pande hizi mbili. Kumekuwepo pia na ushirikiano katika masuala ya kitamaduni, kisayansi na katika masuala ya tiba ya mwanadamu na kwamba, wameamua kuendeleza na kudumisha mahusiano haya hata kwa siku za usoni. Vatican na Russia zimetiliana sahihi mkataba wa kurahisisha utoaji wa hati za kusafiria kwa wanadiplomasia wa pande hizi mbili.

Kardinali Parolin akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wake na Waziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa wa Russia anasema, wamezungumzia pia kuhusu maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Russia: matatizo na changamoto ambazo zinapaswa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Kwa mfano upatikanaji wa vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini Russia kwa Mapadre na Watawa ambao si wananchi wa Russia bado kuna ugumu wa kuweza kuvipata. Wamezungumzia haja ya kurejesha baadhi ya nyumba za Ibada zilizokuwa zinamilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, ili kuliwezesha Kanisa kutoa huduma za kichungaji kwa waamini wa Kanisa Katoliki wanaoishi nchini Russia. Haya ni mambo nyeti yaliyogusiwa na viongozi hawa wawili na kwamba, wanaangalia kwa pamoja jinsi ya kuyatekeleza kwa dhati.

Kardinali Parolin anakaza kusema, kuhusiana na masuala ya kimataifa, wamejadili kwa kina na mapana hatima ya Wakristo huko Mashariki ya Kati, vita na ghasia nchini Ukraine zinazoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Katika mazingira kama haya, Vatican inapenda kujielekeza zaidi katika huduma kwa waathirika; kwa kusimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ili kupata amani ya kudumu, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika haki, sheria na kanuni msingi. Majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi; kwa kuzingatia utu na heshima ya binadamu ni mambo msingi yanayopaswa kudumishwa na wote.

Vatican kwa upande wake, itaendelea kutofungamana na upande wowote ule wa kisiasa, ili kukazia kwa namna ya pekee: haki ya kimataifa na umuhimu wa kusimama kidete, kulinda na kudumisha amani duniani sanjari na kuanza mchakato wa kurejesha mahusiano na mafungamano bora miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa. Kumekuwepo na majadiliano ya kina na mapana kuhusiana na hatima ya maisha ya Wakristo huko Mashariki ya kati,  vita, ghasia na mipasuko ya kisiasa Barani Afrika na katika baadhi ya maeneo duniani ingawa, Russia imesimamia upande wake, lakini hata Vatican anasema Kardinali Pietro Parolin, imeonesha msimamo wake unaojikita katika haki msingi za binadamu; uhuru wa kuabudu, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi. Haya ni kati ya masuala tete ambayo yameendelea kufanyiwa kazi kati ya Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican katika mazungumzo yake na Rais Vladimir Puttin wa Russia, Jumatano, tarehe 23 Agosti 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

23/08/2017 09:57