Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Imani ya Mtume Petro imemwezesha kupata ufunguo wa imani na maadili

Mtakatifu Petro kutokana na imani yake thabiti kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai, alipewa ufunguo wa imani na maadili, licha ya mapungufu yake ya kibinadamu!

22/08/2017 13:47

Baada ya kumuumba mwanadamu Mwenyezi Mungu alimwambia: “Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu wa nchi” (Mw 1:28). Mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kiumbe huyu ametunukiwa namna ya ajabu zaidi ya viumbe vyote, amepewa akili na utashi na kama mzaburi anavyo mwinua anamtaja kama yeye alifanywa mdogo kidogo tu kuliko Mungu (Zab 8:5). Hiyo ni namna ya ajabu anayofanywa mwanadamu na zaidi anashirikishwa kazi za kimungu.

Injili ya Dominika hii inatuonesha jinsi ambavyo mwanadamu anashirikishwa kazi ya Mungu. Mtume Petro anapewa funguo za ufalme wa mbinguni kusudi kuweza kufungua au kufungia lolote. Ni mamlaka ya kimbingu ambayo yanakasimiwa kwa mwanadamu. Huu ni ufunuo wa mamlaka anayopewa Baba Mtakatifu kama Halifa wa Mtume Petro katika kuisimamia imani na maadili ya Kanisa. Mtume Petro anapewa madaraka hayo baada ya kuikiri imani: “Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai”. Kristo anampatia Petro sifa ya kuwa mwamba, mahali ambapo anaisimika imani ya Kanisa. Petro anakuwa mwamba, yaani mahali ambapo misingi ya kiimani itakuwepo, mahali ambapo wanadamu wanapaswa kuchota ukweli wote wa kiimani na kimaadili.

Tukio hili la kupewa funguo linaonekana pia katika somo la kwanza. Katika sehemu hii tunamwona mmoja anayenyang’anywa madaraka. Huyu ni Shebna, mtunza wa hazina ya hekalu anayeambiwa kwamba: “nitakusukuma na kukutoa katika mahali pako”. Ananyang’anywa kazi yake kwa sababu ya kukosa uaminifu. Nafasi yake anapatiwa Eliakimu mwana wa Hilkia. Anapewa funguo za hazina bila shaka ni kutokana na uaminifu wake na hivyo anategemewa kuitunza vyema hazina hiyo. Huyo ni mfano wa Mtume Petro anayepewa funguo za hazina ya mbinguni kusudi kwa uongozi wake aweze kuwapatia watu wote kinachostahili kutoka katika hazina hiyo.

Lakini tukiangalia namna inavyojulikana imani ya Petro tunaona la kujifunza. Mtume Petro haipati imani yake kwa sababu na maneno na namna watu wanavyosema. Kristo anaanza kuuliza “watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?” Ni hali kutafuta jinsi ambavyo jamii inampokea. Namna ambavyo watu wanamtambulisha pengine kutokana na miujiza, mafundisho au uponyaji wake. Bila shaka haya yote yatakuwa yameanza kuwa fikirisha watu na kumpatia unasaba fulani: “Yohane Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii”. Mtume Petro hategemei majibu hayo bali anatamka jibu lake mahususi ambalo kwalo linamfanya kuwa jiwe au mwamba wa kujenga ambao juu yake itajengwa imani.

Jibu madhubuti la kiimani la Mtume Petro linaelezwa kuwa limepata chanzo chake kutokana na ufunuo wa Kimungu. Kristo anamwambia kwamba: “mwili na damu havikufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni”. Hili ni dokezo muhimu katika majawabu mbalimbali ya kiimani. Kumtamka Kristo kuwa ni Masiha, Mwana wa Mungu aliye hai si suala la ueledi au ujuzi au uchunguzi wa kiakili bali ni matokeo ya kazi ya Mungu ndani mwako. Ni onyo la kutobaki katika wingi wa madaftari na tafiti nyingi ili kuipata elimu juu ya Mungu. Taalimungu kama tunavyofundishwa na hati ya Mtaguso mkuu wa pili wa Vatikano “Dei Verbum” inapaswa kupata chanzo chake katika Ufunuo wa Mungu. Tutakapobakia katika hatua ya kidunia tu matokeo yake ni kuipambanua imani kijuu juu tu na kutokuipatia fursa kupenya ndani ya mioyo ya watu na kuzaa matunda mema.

Katika ulimwengu wetu wa leo wa maendeleo ya sayansi na teknolojia mambo ya kiimani yanakosa mvuto na mashiko. Vitu Vingi vinatiliwa mkazo kutafuta kupata mvuto kupitia tafiti mbalimbali za kisayansi. Majibu kwa maswali mengi ya kiimani na kimaadili yanakosa nafasi na hivyo si ajabu kuona hata maelekezo kutoka kiti cha kitume huwekewa ukinzani. Kwa bahati mbaya namna hii ya kuyachukulia masuala ya kiimani na kimaadili yananyemelea hata ndani ya anga za Kanisa. Wakati mwingine tunadiriki hata kuutupilia mbali au kuufumbia macho ujumbe wa Injili unaonuia kuueneza upendo wa Mungu na kupanga hoja mbalimbali za kisayansi na kitaaluma huku tukidhani tunaitetea imani.

Mtume Paulo anatuambia kwamba: “Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani!” Mtume Petro hakuhitaji kwenda kukaa chini na kutafakari au kufanya utafiti ndipo atoe jawabu kuwa Kristo ni nani. Yeye alimruhusu Roho wa Mungu kumuongoza na hekima hiyo ya kimungu ikamfunulia kwamba Kristo ni Mwana wa Mungu aliye hai. Elimu hii ilihitaji tu utayari wa mmoja kuruhusu kuongozwa na Mungu na kujazwa Elimu hiyo ya kimungu. Hii haimaanishi kwamba tunadharau uchunguzi na tafiti mbalimbali, la hasha! Bali himizo ni kuupa ufunuo wa Mungu kipao mbele.

Tutambue kwamba kazi zote tuzitendazo hapa duniani ni kazi za Mungu. Tangu uumbaji mwanadamu amekasimiwa kazi za kimungu. Kwa kuwa ni kazi za Mungu basi tunapaswa daima kuyatafuta mapenzi ya Mungu katika kila tulitendalo. Kwa nini Mungu amenipatia nafasi hii? Mungu ananitaka nitende nini au nitoe nini mahali hapa na wakati huu? Tuepuke kuongozwa na mazoea au tamaduni za mahali. Maneno au uzoefu wa mahali unaweza kuwa kinyume na Neno la Mungu. Tutakapomsikiliza yeye kwa kuitii sauti yake kwa hakika tutatimiza vema na kwa uaminifu wajibu anaotukasimu.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.

22/08/2017 13:47