2017-08-21 08:33:00

Papa Francisko: Epukeni ugonjwa wa ukosefu wa kinga za kiroho mwilini


Mkutano wa urafiki kati ya watu nchini Italia unaofanyika kila mwaka na ambao sasa umeingia katika awamu yake ya XXXVIII ni fursa makini ya kutafakari na kupembua mambo msingi yanayorutubishwa katika maisha ya kila siku, ambayo wakati mwingine, hayapewi uzito unaostahili. Hii inatokana na hali halisi inayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo, kiasi kwamba, anaonekana kuwa na haraka kupita kiasi cha kutaka kila dakika kugeuza karatasi ya maisha yake. Kumbe, kila mwaka wajumbe wa mkutano wa urafiki wa watu wanapata nafasi ya kukaa na kutafakari mambo msingi yanayojenga utu na heshima ya binadamu, ambayo kamwe hayawezi kubezwa!

Huu ni mwaliko wa kujizatiti katika kukuza na kudumisha urithi ambao watu wameupata kutoka kwa wazazi wao; mambo ambayo wanayathamini na hawana budi kuyadumisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni fursa inayomsukuma kila mjumbe kufanya rejea katika historia ya maisha yake binafsi, ili kuiendeleza kama amana na urithi mkubwa, vinginevyo moto huu wa hazina na urithi mkubwa kutoka kwa wazazi utaendelea kupoteza nguvu na hatimaye, kuzimika kabisa! Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu Francesco Lambiasi wa Jimbo Katoliki Rimini, nchini Italia kama sehemu ya maadhimisho ya Mkutano wa Urafiki kati ya Watu nchini Italia.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huu anakaza kusema, kati ya hatari za jamii mamboleo ni tabia ya kuwa na kumbukumbu ndogo na kutothamini hazina ya mambo msingi yaliyopita kwa kudhani kwamba, hayana nafasi tena katika ulimwengu mamboleo na maendeleo ya sayansi na teknolojia! Lakini, madhara yake ni makubwa sana kwa jamii hususan katika mchakato mzima wa elimu unaowanyima vijana wa kizazi kipya nafasi ya kuwa na matumaini ya kumbu kumbu endelevu katika maisha yao kwa siku za usoni! Haiwezekani kuchukua msimamo thabiti pasi na rejea ya historia iliyowafikisha katika hatua hii ya maisha. Kama Wakristo wanasikitika kupoteza amana na utajiri wa Mapokeo yao.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, huu ndio ule wakati uliokubaliwa wa Kanisa kutoka kifua mbele, likitambua kwamba, ndani mwake linabeba Mapokeo, amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume wake. Linasukumwa na kuongozwa na mwanga wa Roho Mtakatifu ili kukutana na watu wanaotafuta maana ya maisha. Kuna nyayo za uwepo endelevu wa Mwenyezi Mungu katika maisha na historia ya mwanadamu, kuanzia tangu mwanzo kabisa wa historia ya uumbaji, kwani viumbe vyake vyote vinatangaza na kutukuza kazi hii kubwa katika ulimwengu. Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, ameamua kushiriki katika historia ya maisha ya mwanadamu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili na kukaa kati ya watu wake. Mwenyezi Mungu si kumbu kumbu iliyopitwa na wakati, bali ni uwepo endelevu unaopaswa kupokelewa kwa heshima na taadhima, kama kielelezo cha upendo kutoka kwa watu wapendanao!

Baba Mtakatifu Francisko anawaangalisha Wakristo kuwa macho na makini sana na ugonjwa wa “UKIRO” yaani, “Ukosefu wa Kinga ya Maisha ya Kiroho mwilini” inayowafanya kusahau kumbu kumbu ya historia ya uhusiano binafsi na Mwenyezi Mungu, aliyewapenda upeo, akawanunua kwa Damu Azizi ya Mwanaye mpendwa Yesu Kristo, ili kuwafanya kuwa watu wake. Inasikitisha sana pale, mwamini anapofuta kumbu kumbu hii msingi, kwani anakosa uhakika wa usalama wa maisha yake na matokeo yake hofu, wasi wasi na mashaka vinatawala kuwakosesha ile hamu ya kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, pale mwamini anapoacha bandari salama ya maisha yake ya kiroho inayo muunganisha na Baba yake wa mbinguni, anakuwa ni chambo rahisi sana cha kuweza kumezwa na malimwengu na hatimaye, kugeuzwa kuwa ni mtumwa wa maisha ya kufikirika, yanayomfanya mwamini kuelea katika ombwe, hali ya kukata tamaa na majonzi makubwa yanayomsukuma kutafuta njia ya kujaza utupu na ukavu wa maisha ya kiroho.

Baba Mtakatifu anasema, ili kuweza kuepuka ugonjwa wa “Ukosefu wa Kinga ya Maisha ya Kiroho mwilini”, kuna haja ya kujikita katika upendo unaofumbatwa katika Kristo Yesu, anayewahakikishia uwezo wa kupambana na changamoto mamboleo za maisha zinazohitaji majibu makini, daima kwa kuendelea kuambatana na Roho Mtakatifu, ili aweze kuwaongoza pale anapotaka mwenyewe! Upendo wa Kristo Yesu unaendelea kuwafikia waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwa njia ya maisha na utume wa Kanisa, Watakatifu na Mashuhuda wa imani, amana ya Kanisa hata katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Yote haya anasema Baba Mtakatifu ni matukio yanayotangaza uwepo wa Emmanuel, yaani Mungu pamoja na watu wake, changamoto na mwaliko wa kukuza na kudumisha upendo huu kama ilivyokuwa siku ile ya kwanza mwamini alipokutana na Mwenyezi Mungu katika hija ya historia ya maisha yake! Kristo Yesu kwa mara ya kwanza alikutana na hatimaye, akawaita Mitume wake pale Galilaya, changamoto kwa waamini kurejea tena na tena mwanzoni kabisa mwa neema ya Mungu iliyoanzisha mchakato wa hija ya maisha, pale Yesu alipopita katika historia ya maisha ya kila mwamini, akamwangalia kwa jicho la huruma na upendo na hatimaye, akamwita amfuate! Mwanzo huu wa maisha ya Kikristo ni amana inayopaswa kuendelezwa na kudumisha.

Mama Kanisa anawahamasisha watoto wake kizazi baada ya kizazi kutunza ndani mwao amana na urithi wao wa imani na kwamwe wasikate tamaa wanapokutana na matatizo na changamoto za maisha. Waamini anasema Baba Mtakatifu Francisko wawe na ujasiri wa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutafuta na kudumisha kile: kilicho kweli, chema na kizuri ambacho wamerithi kutoka kwa wazazi na walezi wao, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Ndiyo maana Baba Mtakatifu anawahamasisha wajumbe na waandaaji wa Mkutano wa urafiki kati ya watu nchini Italia kuwa makini kusoma alama za nyakati ili kuzima kiu ya uwepo wa Mungu katika maisha yao, tayari kuzima kiu ya maana ya maisha ya mwanadamu. Watu waweze kuona shuhuda za Injili ya matumaini yasiyoweza kumdanganya mtu awaye yote! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawapatia wajumbe wote wa mkutano huu baraka zake za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.