2017-08-21 10:40:00

Hija ya Papa Francisko nchini Chile, 2018: Amani yangu nawapa!


Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki pamoja na Serikali ya Chile na kwamba, anatarajiwa kufanya hija ya kitume nchini humo kuanzia tarehe 15 hadi tarehe 18 Januari 2018. Kauli mbiu inayoongoza hija hii ya kitume ni “Amani yangu nawapa”. Hii ni sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Yohane 14:27. Baraza la Maaskofu Katoliki Chile linasema, huu ndio ushuhuda wanaoufanyia kazi kama kielelezo na utambulisho wa waamini nchini Chile kama sehemu ya mchakato wa kutafuta, kujenga nakudumisha amani miongoni mwa familia ya Mungu nchini Chile.

Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Chile, anapenda kuhimiza ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kidugu miongoni mwa wananchi wa Chile katika ujumla wao. Nembo ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Chile inakazia mambo makuu matatu: Msalaba, Sahihi ya Baba Mtakatifu Francisko na Ramani ya Chile. Nembo hii inapambwa kwa rangi ya bendera ya Chile na Vatican, ikiwa na maneno “Chile 2018”. Nembo hii ni matunda ya kazi ya mikono na ushirikiano wa watu mbali mbali nchini Chile, wanaotamani kuona hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko inagusa sakafu ya maisha ya wananchi wote wa Chile katika ujumla wao kwa kujikita katika amani, chachu ya maendeleo endelevu ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.