2017-08-19 10:52:00

Wokovu ni zawadi ya Mungu kwa binadamu wote inayopatikana kwa imani


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Kanisa ni chombo na Sakramenti ya wokovu ndiyo maana linajibidisha katika utekelezaji wa utume wake wa kimisionari, ili watu waweze kuufahamu ukweli na kwa njia ya ukweli huu, waweze kupata wokovu ambao kimsingi ni zawadi ya Mungu kwa watu wote pasi na ubaguzi. Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XX ya Mwaka A wa Kanisa inakazia sana kuhusu imani ambayo ni fadhila ya Kimungu inayomwezesha mwamini kujiambatanisha na Mwenyezi Mungu katika maisha yake yote: wakati wa raha na shida; wakati wa kukata tamaa na kutembea katika giza. Imani inarutubishwa kwa matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani kama anavyoshuhudia yule Mwanamke Mkananayo!

Baba Mtakatifu Francisko anatukumbusha kwamba, Yesu Kristo ni uso na ufunuo wa huruma ya Baba wa milele. Huruma ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani ya ndani na ni sharti muhimu sana katika wokovu wa binadamu. Huruma ni sheria ambayo imejikita katika sakafu ya moyo wa mwanadamu, inayomsukuma kutenda mema. Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu. Anajisikia kuwajibika kwani anatamani kila mtu awe na afya njema, mwenye furaha na amani tele kama alivyotamani yule Mwanamke Mkananayo kwa mtoto wake aliyekuwa amepagawa! Anasema, iweni na huruma kama Baba yenu wa mbinguni alivyo na huruma!

“Bwana unisaidie”! Ni kilio cha mwanamke Mkananayo anayeonja huruma ya Mungu kwa njia ya Kristo Yesu anayekuja kumsaidia kuondoa udhaifu wa binti yake aliyekuwa amepagawa! Akamsaidia kuonja uwepo wake endelevu. Leo hii ninapenda kuyabinafsisha maneno ya Baba Mtakatifu Francisko anayetutaka kufungua macho yetu ili tuweze kuona machungu ya ulimwengu, majeraha ya ndugu zetu wanaonyimwa hadhi yao, tutambue kwamba tunahimizwa kusikia kilio chao cha kuomba msaada. Tuwaendelee na kuwasaidia; tubomoe vizuizi vinavyotutenganaisha kwa kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene; ili kujenga na kudumisha: misingi ya haki, amani, upendo, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi!

Liturujia ya Neno la Mungu inatufunulia kwa namna ya pekee kabisa kuhusu zawadi ya wokovu inayotolewa kwa watu wote pasi na ubaguzi wala upendeleo! Jambo la msingi ni kuwa na imani thabiti inayoweza kuvuta huruma ya Mungu katika maisha yako. Mwenyezi Mungu alifanya Agano la Kale na Waisraeli, lakini mataifa yote yanaweza kujenga urafiki na Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza Amri, Sheria na Maagizo yake kwa uaminifu mkubwa. Dini isiwe ni chanzo cha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; utengano, ubaguzi na nyanyaso; bali dini iwe ni chemchemi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Lakini, historia inaonesha kwamba, kwa nyakati mbali mbali, dini zimekuwa ni chanzo cha vita, vurugu na mipasuko ya kijamii kutokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani. Ndiyo maana Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanakazia mchakato wa majadiliano ya kidini. Kwa njia ya imani, toba na wongofu wa ndani watu wote duniani wanaweza kupata zawadi ya wokovu. Kanisa Katoliki halikatai yote yaliyo kweli na matakatifu katika dini mbali mbali duniani. Kanisa linaheshimu kwa sifa timamu namna yao ya kutenda, kuishi, sheria na mafundisho yanayolenga kudumisha ukweli. Lakini, Kanisa litaendelea kutangaza na kushuhudia kwamba, Yesu Kristo ni: njia, ukweli na uzima. Linataka kudumisha: ushirikiano, ushuhuda na mafungamano, ili kuimarisha haki jamii; tunu msingi za kimaadili na utu wema; haki msingi za binadamu; uhuru wa kuabudu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ninayasema yote haya nikijitahidi kufafanua mafundisho ya Kristo Yesu katika Injili ya leo kuhusu mahojiano mbashara kati ya Mwanamke Mkananayo na Kristo Yesu ambaye amewapatanisha Wayahudi na watu wa Mataifa kwa njia ya Msalaba wake na hivyo kuwaunganisha tena. Hapa tunagusia uhusiano tete kati ya Wayahudi na ”wapagani”, hao ndio watu wa Mataifa. Leo, Yesu analeta mageuzi makubwa katika dhana ya wokovu wa binadamu, ambayo kimsingi ni zawadi ya Mungu kwa watu wote, ikiwa kama watakuwa na imani tnabiti, waaminifu kwa Amri na Maagizo yake. Haitoshi kufahamu Amri za Mungu, lakini, Yesu anakazia imani inayomwezesha hata”Mbwa kula makombo yanayoanguka mezani pa Bwana wake”.

Hapa Mbwa anaweza kuwa ni ”mtu wa kuja, Kyasaka, Mnyamugi, Mnyamahanga, mshenzi au mpagani” mtu asiye wa kabila langu, wala asiyetoka katika mkoa au nchi yangu. Kanisa linakemea na kulaani: chuki na udhalimu dhidi ya watu na ukatili dhidi ya Wayahudi. Kanisa linadumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, kwani linataka wokovu kwa watu wote wa Mataifa. Kwa njia ya muujiza wa Yesu kwa Mwanamke Mkananayo tunaweza kukiri na Petro mtume kwamba, kwa hakika Mwenyezi Mungu hana upendeleo bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na Yeye na kwamba, Kristo Yesu ni Bwana wa wote.

Huu ndio pia ufafanuzi unaotolewa pia na Mtume Paulo katika somo la pili kwa kukazia kwamba, watu wote wanahamasishwa kuchuchumilia wokovu. Waisraeli walipata bahati na upendeleo wa kuwa ni taifa teule la Mungu; wakatumika kama daraja ya utekelezaji wa kazi ya ukombozi; lakini kwa bahati mbaya wakajisahau na kubweteka, kiasi cha kushindwa kutambua kazi na utume wa Kristo Yesu. Lakini wale waliomkubali na kumpokea wamefanyika kuwa ni watoto wateule wa Mungu. Katika somo la kwanza tumekumbushwa kwamba, nyumba ya Mungu ni nyumba ya sala na sadaka kwa watu wote wa Mataifa.

Tuendelee kujizatiti katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa imani tendaji! Tujitahidi kuvuta huruma ya Mungu kwa kamba ya: Sala, Tafakari, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Mwanamke Mkananayo alionesha upendo na huruma kwa binti yake aliyekuwa amepagawa, kiasi cha kujishusha ili kuomba huruma ya Yesu hata kama alijitambua kwamba, alikuwa ni mtu wa Mataifa. Ni mwanamke aliyekuwa na imani thabiti katika uwepo, uweza na nguvu ya Yesu anayetenda miujiza, ili wote waweze kupata furaha, amani, utulivu na hatimaye wokovu! Tuendeleze majadiliano ya kidni na kiekumene kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.