2017-08-19 14:51:00

Jubilei ya Miaka 25 ya Parokia ya Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma


Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma katika kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, Miaka 100 ya Upadre Tanzania na miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Jimbo Katoliki la Musoma ameandika Barua ya Kichungaji inayoongozwa na kauli mbiu “Upendo kwa Utume” na humo anapembua historia ya Jimbo Katoliki la Musoma. Parokia ya Kyabakari tarehe 20 Agosti 2017 inaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake ni matunda na juhudi za ukuaji wa Kanisa Mahalia Jimbo Katoliki la Musoma.

Uinjilishaji katika Jimbo letu la Musoma unayo historia nzuri na inayotia moyo. Shirika la kwanza kueneza injili ndani ya mipaka ya Jimbo letu la Musoma ni la wamisionari wa Afrika - White Fathers. Hawa walifika kwa mara ya kwanza mwaka 1897 katika eneo la Nyakatende wakitokea Kagunguli, Ukerewe. Katika ujio wao huu mambo hayakuwaendea vizuri kwani walishambuliwa sana na ugonjwa wa malaria. Ugonjwa huu ulisababisha kifo cha mwenzao, Padre. Joseph van Thuet, na kwa sababu hii walilazimika kurudi Kagunguli. Mwaka 1909 waliamua kurudi tena. Katika awamu hii walipata misukosuko mingine mingi ikiwemo kukataliwa. Hata hivyo mwaka 1911 walipewa eneo Nyegina na hapo walianza  rasmi kujenga kanisa.  Ni katika mwaka huo huo mkristo wa kwanza alibatizwa.

Kwa sababu hii tunauhesabu mwaka 1911 kuwa ndio mwaka ambao Ukristo umepokelewa katika mipaka ya Jimbo la Musoma. Mwaka 2011 tuliadhimisha kwa shukrani Jubilei ya Miaka 100 ya kuuishi Ukristo katika Jimbo letu. Wamisionari wa Afrika walifanya kazi ya uinjilishaji hadi tarehe 11 Aprili 1946 ilipoundwa Vikarieti ya Musoma - Maswa. Vikarieti hii ilikabidhiwa kwa wamisionari wa Shirika la Maryknoll. Ni katika uongozi wa wamisionari hawa Musoma ilifanywa kuwa "Prifektura" ya Kitume tarehe 24 Juni 1950 na hatimaye kupewa hadhi ya kuwa Jimbo tarehe 05 Julai 1957.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Padre Wojciech Adam Koscielniak, Paroko wa Parokia ya Kiabakari Jimbo Katoliki la Musoma, muasisi wa Parokia na Kituo cha Hija cha Kiabakari Jimbo Katoliki Musoma, chemchemi ya huruma ya Mungu ndani na nje ya Tanzania anasimulia historia ya Parokia ya Kiabakari iliyopewa msukumo wa pekee na Hayati Askofu Justin Samba wa Jimbo Katoliki la Musoma kwa wakati ule, aliyebariki jiwe la msingi la ujenzi wa Makao makuu ya Parokia kunako tarehe 26 Januari 1991 na kuzinduliwa rasmi na Askofu mkuu Agostino Marchetto, Balozi wa Vatican nchini Tanzania kwa wakati huo.

Padre Wojciech Adam Koscielniak anasema, kilele cha maadhimisho haya ni Jumamosi, tarehe 19 Agosti 2017. Hii ni Siku maalum ya kuimarisha imani, matumaini na mapendo ya familia ya Mungu Parokia ya Kiabakari kwa kumtolea sifa na shukurani Roho Mtakatifu aliyewezesha kumwilisha ndoto ya kuwa na Kituo cha Huruma ya Mungu Jimbo Katoliki Musoma katika kipindi cha miaka 25 na matunda yake yanaonekana sasa. Hii ni Siku ya waamini 200 kupata Sakramenti ya Kipaimara ambayo imetolewa na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma. Katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa mapaji ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Haya ni mapaji yanayoonekana na kutumika katika uhalisia wa maisha ya watu kila siku!

Tarehe 20 Agosti 2017 ni kilele cha maadhimisho haya yanayofumbatwa kama alama ya shukrani na mwanzo wa ukarabati mkubwa wa Kanisa la Parokia ya Kiabakari ambalo pia ni Kanisa la Kituo cha Hija Jimbo Katoliki Musoma. Ukarabati huu unatarajiwa kukamilika hapo tarehe 31 Desemba 2017, Siku Maalum ya Kufunga uhamasishaji wa Sakramenti ya Ndoa, Parokia ya Kiabakari na Mwaka wa Uimarishaji wa Familia Katoliki, Parokia ya Kiabakari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.