2017-08-18 14:55:00

Watu 13 wafariki dunia baada ya kuangukiwa na mti kabla ya Ibada


Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam za rambi rambi kwa Askofu Antonio Josè Cavaco Carrilho wa Jimbo Katoliki la Kisiwa cha Madeira, nchini Ureno kutokana na maafa yaliyowasibu waamini 13 kufariki dunia na wengine 49 kuangukiwa na mti mkubwa wakati wanajiandaa kwa maandamano katika Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho, hapo tarehe 15 Agosti 2017. Baba Mtakatifu katika salam za rambi rambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anapenda kuwahakikishia wale wote waloguswa na kutikiswa na msiba huu uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake.

Baba Mtakatifu anawaombea waliofariki dunia pumziko la amani huko mbinguni, majeruhi waweze kupona haraka na kurejea tena katika shughuli zao za kila siku! Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Ureno limesikitishwa sana na tukio hili ambalo limewakumba waamini wakati wanajiandaa kufanya maandamano kwa ajili ya kusrehekea Siku kuu ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni. Wanapenda kuonesha mshikamano wao wa dhati na familia ya Mungu kisiwani hapo. Kwa muda wa siku tatu, kuanzia tarehe 15 Agosti 2017, familia ya Mungu nchini Ureno imekuwa ikitolea sala na sadaka yake kwa ajili ya kuwaombea waliopatwa msiba katika tukio hili la kushangaza sana.

Mti huu ambao una zaidi ya miaka mia mbili, uliwahi kuonesha dalili za kuanguka, lakini ukadhibitiwa! Tarehe 15 Agosti 2017 ukaanguka kwa mwendo kasi wa ajabu, kiasi hata cha kusababisha maafa makubwa kwa watu waliokuwa wanajiandaa kwa ajili ya maandamano ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni. Mashuhuda wanasema, lilikuwa ni tukio la kufumba na kufumbua macho, tayari watu kadhaa wakawa wamepoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa! Rais Marcelo Rebelo de Sousa ametembelea eneo la tukio ili kuwafariji waliofikwa na maafa haya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.