2017-08-18 14:26:00

Sayansi ya tiba ya mwanadamu inavyomwilishwa katika Injili ya huduma


Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican ni kielelezo makini cha maisha na utume wa Kanisa katika ukuaji wa sayansi na maendeleo ya tiba ya binadamu inayomwilisha katika Injili ya upendo, hasa kwa watoto wagonjwa na maskini, wanaohitaji huruma, upendo na faraja. Hii ni hospitali inaounda familia ya Mungu inayowajibikiana na kusaidiana; kwa kuwapokea watoto wagonjwa wanao bahatika kuishi na kuhudumiwa katika mazingira ya kifamilia na Jumuiya ya inayojikita katika huduma, faraja na mapendo.

Ni Jumuiya ya wataalam na mabingwa wa sayansi ya tiba ya mwanadamu, inayomwilisha katika utu na heshima ya binadamu; inayopania kuganga na kutibu magonjwa ya watoto, kwa kuzingatia utu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Familia ni hospitali ya kwanza kwa shida na mahangaiko ya binadamu, hapa ni mahali ambapo mgonjwa anapata faraja, imani na matumaini katika mahangaiko yake. Hospitalini hapa, faraja hii inatolewa na madaktari, wafanyakazi na wanafamilia wenyewe.

Hii ni hotuba iliyotolewa hivi karibuni na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa kuwasilisha taarifa ya utendaji wa Hospitali ya Bambino Gesù katika kipindi cha Mwaka 2016- 2017. Ni taarifa inaonesha mafanikio yaliyofikiwa katika huduma, tiba na uchunguzi wa kisayansi wa magonjwa ya watoto wadogo wanaopatiwa tiba hospitalini hapo kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Umekuwa muda pia wa kuweza kuangalia changamoto, magumu na kinzani wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa huduma ya tiba na kinga kwa watoto wagonjwa.

Hospitali hii inashirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Afya nchini Italia, ndiyo maana katika tukio hili waziri wa afya Beatrice Lorenzin, alikuwepo. Lengo ni kuendelea kusimama kidete: kulinda, kutunza na kudumisha afya bora ya umma. Tafiti na takwimu mbali mbali zilizotolewa katika taarifa ya Hospitali ya Bambino Gesù katika kipindi cha Mwaka 2016- 2017 ni muhimu sana katika mchakato wa maboresho ya afya ya watoto ndani na nje ya Italia kwa kutambua kwa unyenyekevu mkubwa kwamba, hakuna mtu ambaye ana hati miliki ya afya na maisha ya binadamu katika ujumla wake.

Kardinali Pietro Parolin ametumia fursa hii kuwahimiza  madaktari, watafiti na wanasayansi wanaojisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa watoto wagonjwa hospitalini hapo, kuendeleza kazi hii kwa: weledi, juhudi, maarifa na nidhamu ya kazi; ukweli na uwazi katika masuala yote ya uongozi na huduma kwa wagonjwa. Wajisadake bila ya kujibakiza kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua kwa unyenyekevu kwamba, hawawezi kutatua changamoto zote za afya na tiba zinazowakabili watoto sehemu mbali mbali za dunia. Wawe na dhamiri safi kwa kutekeleza yale wanayopaswa kutekeleza kwa moyo wa dhati kabisa. Huduma kwa wagonjwa licha ya magumu na changamoto zake, ni sehemu ya mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, huu ni utume wanaoutekeleza kwa niaba ya Mama Kanisa kwa ajili ya watoto wagonjwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Pietro Parolin amependa kuwahakikishia uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu Francisko katika utume wao na kwamba, anathamini sana mchango wanaoutoa kwa ajili ya watoto wagonjwa. Kwa watoto wengi Dr. Mariella Enoc, Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù amekuwa kama mama yao mdogo! Katika takwimu zinazotolewa, daima ikumbukwe kwamba, kuna majina, historia na maisha ya watoto wagonjwa; waliofanyiwa uchunguzi; familia na watu kadhaa waliohudumiwa na kusaidiwa katika shida na mahangaiko yao; watoto ambao wameonja huruma na upendo kutoka katika Hospitali ya Bambino Gesù, leo hii wanaweza kusimulia historia tofauti kabisa!

Kardinali Pietro Parolin anakaza kusema, takwimu hizi zinaonesha dhamana na wajibu wa viongozi wa Hospitali kusimama kidete, ili kuhakikisha kwamba, huduma hii inakuwa ni endelevu, ili kuunganisha na hatimaye, kumwilisha tafiti za kisayansi na Injili ya huruma na upendo inayotolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa katika ujumla wake kwa ajili ya watoto wagonjwa. Utume wa Hospitali ya Bambino Gesù unapaswa kuendeleza sayansi na huduma ya upendo kwa watoto wagonjwa, dhamana inayohitaji tafiti makini na endelevu; mazingira yenye amani na utulivu yanayofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya kifamilia. Hospitali hii, kiwe ni kituo cha ushuhuda wa mshikamano wa huduma ya upendo kwa watoto wagonjwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Pietro Parolin anafafanua kwamba, mwaka 2019, Hospitali ya Bambino Gesù itakuwa inaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1869 na familia ya Salviati. Hii ni historia ya pekee na muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika huduma kwa watoto wagonjwa. Ni wakati muafaka wa kuangalia changamoto za mbeleni zinazojitokeza katika sayansi na tiba ya binadamu kwa imani, matumaini, ujasiri na ushupavu, ili kufanya maboresho makubwa katika huduma zinazotolewa na Hospitali ya Bambino Gesù. Ubora, usalama na ukarimu ni mambo yanayopaswa kuvaliwa njuga kwa siku za usoni. Dhamana hii inapaswa kutekelezwa na Baraza la Uongozi wa Hospitali ya Bambino Gesù; kwa hekima na busara; kwa imani na matumaini sanjari na kutambua kwamba, yale yote wanayowatendea watoto wadogo, wanamtendea Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.