2017-08-18 14:08:00

Papa Francisko alaani vitendo vya kigaidi huko Barcellona


Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na taarifa ya shambulizi la kigaidi lililotokea mjini Barcellona, Hispania na kusababisha zaidi ya watu 13 kupoteza maisha; 90 kujeruhiwa vibaya na kati yao 15 wamelazwa hospitalini wakiwa mahututi. hayo yamebainishwa na Msemaji mkuu wa Vatican Dr. Greg Burke. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua nafasi hii kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliofariki dunia, ili waweze kupata pumziko la milele na majeruhi kuweza kupona haraka na kurejea tena kwenye maisha na shughuli zao za kila siku. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na familia yote ya Mungu nchini Hispania. Baba Mtakatifu katika salam zake za rambi rambi alizomtumia Kardinali Juan Josè Omella Omella wa Jimbo kuu la Barcellona analaani na kushutumu kwa nguvu zote, vitendo vya kinyama vinavyofanywa na magaidi dhidi ya ut una heshima ya binadamu. Anapenda kuchukua nafasi hii kwa ajili ya kuombea amani na utulivu duniani kote!

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, katika ujumbe wake kwa vyombo vya habari linasema, limesikitishwa na kuhuzunishwa sana na shambulizi la kigaidi lililotokea huko Barcellona, Alhamisi, tarehe 17 Agosti 2017. Maaskofu wanapenda kuonesha uwepo na mshikamano wao wa dhati na familia ya Mungu nchini Hispania. Wanapenda kuwatia shime walengwa wa mashambulizi haya ya kigaidi, kwa namna ya pekee, wananchi wa mji wa Barcellona na wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama. Vitendo vyote vya kigaidi vinakwenda kinyume kabisa cha maadili, utu, heshima na Injili ya uhai. Vinatishia haki ya maisha na uhuru wa watu. Kielelezo makini cha ukosefu wa kuvumiliana pamoja na ukatili wa kutisha.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumtolea Mwenyezi Mungu sala na maombi kwa ajili ya watu waliofariki dunia kutokana na shambulizi la kigaidi na kwamba, awajalie afya njema majeruhi pamoja na faraja kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na kitendo hiki cha kigaidi. Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, awakirimie watu wa Hispania: amani moyoni mwao, ili kamwe vitendo hivi visijirudie tena.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.