2017-08-18 15:26:00

Mwenyeheri Oscar Romero, shuhuda wa Injili ya matumaini kwa maskini


Tangu mwanzo alipouwawa kikatili Askofu mkuu Oscar Armulfo Romero wakati akiadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, tarehe 24 Machi 1980, maskini na akina “yakhe pangu pakavu tia mchuzi” waliona ndani mwake cheche za utakatifu wa maisha kiasi cha kumwita “Mtakatifu Romero wa Amerika ya Kusini” na “Shuhuda wa Injili ya Matumaini” inayofumbatwa katika kiu ya haki na amani huko Amerika ya Kusini. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Richardo Ezzati Andrello, mjumbe wa Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kilele cha maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kufunga Jubilei ya Miaka 100 tangu alipozaliwa Mwenyeheri Oscar Armulfo Romero. Sherehe hizi zimekwenda sanjari na Siku kuu ya Kupalizwa Bikira Maria Mbinguni mwili na roho, yaani hapo tarehe 15 Agosti 2017.

Mwenyeheri Oscar Armulfo Romero ni shuhuda wa Injili ya Matumaini kwa maskini kutoka Amerika ya Kusini; kwa Kanisa pamoja na wale wote wanaoendelea kujizatiti katika kupigania haki, amani na upatanisho kati ya watu wa Mataifa. Watu wote wanaonyanyaswa, wanaodhulumiwa na kuteswa; watu wasiothaminiwa wala kuheshimiwa utu wao kama binadamu, wanajisikia kwamba, Mwenyeheri Oscar Armulfo Romero ni msimamizi na mwombezi wao. Kifodini cha Askofu mkuu Romero kimeendelea kusikika katika maisha ya watu kutokana na baadhi ya watu kutomfahamu vyema na wengine kumshutumu kwa maneno ya uwongo, ili kutaka kumchafulia jina na sifa njema kwa masilahi ya kisiasa.

Katika mapambano ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Matumaini, aliwahi kusema Baba Mtakatifu Francisko, Khalifa wa Mtakatifu Petro yuko pamoja nao hadi kieleweke. Kardinali Richardo Ezzati Andrello ameitaka familia ya Mungu nchini El Salvador kujizatiti katika mchakato wa kutafuta, kukuza na kudumisha misingi ya haki; amani, ustawi na maendeleo ya wote na kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwapatia baraka zake za kitume na kuwataka kuendelea kumuenzi Mwenyeheri Oscar Romero kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyeheri Oscar Armulfo Romero alikuwa ni shuhuda wa Injili ya Kristo; mtetezi wa Kanisa, utu na heshima ya binadamu. Alikuwa ni chombo cha huruma, upendo, haki, upatanisho na amani ya kweli; mambo aliyotaka kuona yanamwilishwa nchini El Salvador. Ni matumaini ya Kardinali Richardo Ezzati Andrello kwamba kifodini cha Mwenyeheri Oscar Romero kitaendelea kuzaa matunda ya umoja na mshikamano wa Kanisa; haki, amani, maridhiano na mafungamano ya kitaifa nchini El Salvador, kama sehemu ya mchakato ya ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki.

Huu ni mwaliko wa kuendelea kuwa na wongofu wa kichungaji ulioibuliwa na Mwenyeheri Oscar Romero wa kuwa na ujasiri wa kuangalia matukio na historia ya ulimwengu kwa jicho la maskini. Kwa hakika, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mwenyeheri Oscar Romero kunako mwaka 1917 yalipambwa kwa uwepo wa bahari ya maskini na watu wa kawaida, walioona na kutambua cheche za utakatifu wa maisha na utume wa Askofu mkuu Oscar Romero. Ni watu ambao kwa muda wa siku tatu wamefanya maandamano na hija kubwa kwa kutembea kwa miguu tangu tarehe 11hadi tarehe 15 Agosti kuelekea kwenye mji wa Ciudad Barrios, mahali alipozaliwa Mwenyeheri Oscar Romero. Jitihada ziko mbioni ili kubadilisha jina la mji huu, ambao hapo baadaye utaitwa kuwa ni “Ciudad Romero”. Waamini na watu wenye mapenzi mema wametembea umbali wa kilometa 160 na kati ya hizo kilometa 98 wametembea kwa mguu.

Kwa upande wake Kardinali Gregorio Rosa Chavez, Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la  San Salvador amesema, kuanzia sasa kila mwaka ifikapo tarehe 15 Agosti kutafanyika “Matembezi ya Romero” yatakayowawezesha watu wa Mungu nchini El Salvador, kuwakumbuka wafiadini wao, wanaowasindikiza katika safari ya kukutana na Mwenyezi Mungu. Huyu ni kati ya mashuhuda wa maisha ya kiroho wa Mwenyeheri Oscar Romero. Alikuwepo wakati wa maandamano, akitanguliwa na Msalaba pamoja na Sanamu ya Bikira Maria, Mama wa amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.