2017-08-18 15:53:00

Mshikamano wa Makanisa katika kukabiliana na changamoto mamboleo


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuanzia tarehe 20- 24 Agosti, 2017 anatarajia kufanya safari ya kikazi nchini Russia, kama msaidizi wa karibu sana wa Baba Mtakatifu Francisko ambaye anataka kushuhudia na kutangaza Injili ya amani, matumaini na kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu katika umoja, upendo na mshikamano wa dhati! Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujielekeza zaidi katika mchakato wa majadiliano ya kisiasa, kidini na kiekumene katika ukweli na uwazi, ili kujenga na kudumisha mazingira ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Ni safari inayopania kuonesha mshikamano na uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu Francisko katika mahangaiko ya watu wa Mungu katika nchi za Ulaya Mashariki.

Askofu mkuu Ilarione Volokolamsk, Rais wa Idara ya uhusiano na ushirikiano wa Kimataifa wa Kanisa la Kiorthodox la Russia katika mahojiano maalum na  Jarida la “Il Sole 24 Ore” linalochapishwa nchini Italia anasema, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na maboresho makubwa ya mahusiano kati ya Kanisa la Kiorthodox na Russsia pamoja na Kanisa Katoliki; kama inavyojionesha pia uhusiano wa kimataifa kati ya Russia na Vatican katika ujumla wake. Kumekuwepo na ushirikiano wa karibu katika medani mbali mbali za maisha kati ya pande hizi mbili. Hii inatokana na mwendelezo wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene ambayo yamewasaidia kutambua kwamba, kuna mambo mengi ambayo yanawaunganisha pamoja kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi, ikilinganishwa na mambo machacahe yanayowagawa na kutaka kuwasambaratisha.

Askofu mkuu Ilarione anakaza kusema, kuna haja kwa Makanisa kuendeleza majadiliano ya kiekumene ili kujenga na kudumisha uekumene wa sala na maisha ya kiroho; uekumene wa damu na huduma, kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kwa namna ya pekee, ni kwa Makanisa kuendelea kujizatiti katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, hasa kutokana na dhuluma, nyanyaso na mauaji ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia.

Wakristo wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya kiroho, kanuni maadili na utu wema, dhidi ya mmong’onyoko wa maadili unaoendelea kusambaa kwa kasi kubwa duniani kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari inayoifanya dunia kuwa kama “Kijiji”. Kuna mwelekeo wa ukanimungu unaotaka kumng’oa Mwenyezi Mungu kutoka katika maisha na vipaumbele vya watu, jambo ambalo ni hatari sana kwani wanataka kuifanya dini kuwa ni jambo la binafsi na wala si kito cha thamani sana katika maisha ya watu. Huu ndio mwelekeo potofu unaovaliwa njuga kwa wakati huu katika Nchi za Ulaya.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alikutana na Patriaki Cyril wa Moscow na Russia nzima tarehe 12 Februari 2016 mjini Avana, Cuba. Ulikuwa ni wakati wa kuzungumzia masuala mbali mbali ya ushirikiano na hatimaye, viongozi hawa wawili wakaweka sahihi katika tamko la pamoja la ushirikiano kati ya Makanisa haya mawili. Ushirikiano wa Makanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni muhimu sana katika kuvunjilia mbali migogoro ya kidini na hali ya kutoaminiana ambayo imekuwepo kwenye historia na maisha ya Makanisa haya mawili. Majadiliano ya kiekumene hayana budi kudumishwa katika sala na maisha ya kiroho, kwa kuwahusisha waamini wa kawaida, kwani haya ni majadiliano katika uhalisia wa maisha ya watu!

Ibada ya pamoja kati ya waamini wa Kanisa la Kiorthodox na Kanisa Katoliki wakati wa kutembeza masalia ya Mtakatifu Nicholaus wa Bari  imeelezwa kuwa ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika sala, maisha ya kiroho ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha utakatifu wa watu wa Mungu wenye kiu ya kuona Kanisa limeungana chini ya Kristo Yesu, Mchungaji mkuu. Hii ni dhana inayopaswa kukuzwa na kuendelezwa na waamini wa Makanisa yote!

Askofu mkuu Ilarione anakaza kusema, Ibada ya kuheshimu masalia ya Mtakatifu Nicholaus wa Bari imehudhuriwa na watu zaidi ya milioni moja na hawa si wanataalimungu, bali ni waamini wa kawaida wanaoguswa na maisha na utume wa Mtakatifu Nicholaus wa Bari. Hata hivyo, wanataalimungu wanapaswa kuendelea na huduma yao, ili kuondoa mambo yanayokinzana katika imani na ushuhuda wa  Kikristo, ili siku moja, Wakristo wote waweze kuwa chini ya Kristo mchungaji mkuu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.