Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Iweni na huruma kama Baba Yenu wa Mbinguni

Msaada unaoombwa na mwamini ni hatua ya kwanza ya huruma ya Mungu anayekuwa kuwasaidia na kuwakomboa watu wake. - REUTERS

17/08/2017 15:49

Mtakatifu Thomas Acquinas, Mwalimu wa Kanisa anasema, huruma ni ukamilifu wa haki na si kifo chake. Katika Lk. 6:36 tunasoma neno hili ‘Basi iweni na huruma kama Baba yenu alivyo na hurma’ lakini pia tunaambiawa ‘heri walio na huruma, maana watahurumiwa – Mt. 5:7’.Injili ya leo yazungumzia tendo la kushtusha kidogo. Yesu anakutana na mwanamke na ambaye ni mpagani. Mbele ya watu wa kawaida ilikuwa tendo lisilo la kawaida. Na huyu mwanamke anamsalimia Yesu akimpa heshima kubwa ya majina ya kimasiha. Anamwita Yesu Bwana na Mwana wa Daudi. Kwa hakika cheo hiki Mwana wa Daudi chaelezea ukamilifu wa ahadi ya Mungu ya ujio wa mkombozi toka uzao wa Daudi utaokarejesha ufalme wa Mungu kwa watu wake.

Huyu mwanamke alikuwa mpagani. Sasa hatujui alipata kuyajuaje haya yote. Bila shaka mbegu ya imani ilimsukuma. Yule mama anatoa ombi kwa Yesu ili amponye binti yake mgonjwa aliyepagawa na pepo. Kinachoshtusha hapa ni ukimwa wa Yesu kwa ombi hili na baadaye majibu yake kwa ombi hilo. Lile ombi la huyo mama na msisitizo linakuwa kero hata kwa wafuasi wa Yesu. Yesu anapojibu anasema kwanza amekuja kwa ajili ya taifa la Israeli. Yule mama anamsihi na kumwomba awe na huruma kwa wengine. Na hapa imani yake kwa nguvu ya Mungu anayeponya inaonekana. Isieleweke kuwa Yesu hakuja kwa ajili ya wote ila Yesu anasema kwanza kwa taifa la Israeli. Hata hivyo imani ya yule mama inavuka mipaka na binti yake anaponywa. Mtume Paulo katika somo la pili anazungumzia kuhusu upekee na upendeleo wa zawadi ya Mungu kwa taifa la Israeli. Hii lakini haiondoi kwamba na wengine watapata hiyo huruma. Pia katika somo la kwanza twaona jinsi nabii Isaya anavyoongea kuhusu haja ya watu kushika haki ya Mungu na kumrudia Bwana na kumtumikia ili kuipata hiyo huruma.

Tutafakarishwe na mfano huu; mama mmoja alitafuta huruma kwa mtoto wake kutoka kwa mfalme Napoleone.  Mfalme akamjibu yule mama kuwa lile lilikuwa ni kosa lake la pili na hivyo haki inadai auawe.  Mama akaendelea kusema lakini mimi siombi haki itendeke. Naomba apate huruma yako. Mfalme akajibu huyu ni mkosefu na hastahili huruma. Mama akajibu hakika asingestahili huruma, lakini ndiyo hiyo tu namwombea. Mfalme akajibu, basi sawa na apate huruma. Na mama akamwokoa mtoto wake na kifo.

Katika Injili yote ya Mathayo tunaona akiandika kuonesha mambo makubwa yanayoweza kutendeka tukiwa na imani katika Yesu Kristo. Mwinjili Mathayo anawaandikia wakristo wa mwanzo ambao tayari walikuwa wamepokea na kuonesha imani hiyo. Katika Injili ya leo tunamwona Yesu akishangazwa na imani ya yule mama na anamtimizia ombi lake. Sisi hatuna budi kutumia nafasi hiyo na tumwendee daima Yesu katika mahangaiko yetu na shida zetu. Mtakatifu Augustino anasema wazi kuwa, Mungu ametuumba sisi bila hiari yetu, lakini kuupata wokovu yahitaji juhudi binafsi. Tuendelee kuomba mwanga wa Roho Mtakatifu ili tuweze kuuona utukufu wa Mungu uliopo kati yetu na kumwendea Mungu anayeokoa. Tunaamini kuwa neema hii ipo kati yetu kwa hiyo basi wajibu wetu wa kwanza ni kumwendea Mungu kwa mahitaji yetu ya kimwili na kiroho.

Neno la Mungu katika Fil. 3:8-14 litusaidie katika tafakari yetu jumapili hii ya leo. Tunaona kuwa Mtume Paulo anatamani kumjua yeye na uweza wa kufufuka kwake na ushirika wa mateso yake. Mtume Paulo anatamani kufananishwa na kufa kwake. Kwa hakika maneno kama haya au ni ya  kichaa au ni ya mtu mtakatifu. Mtu mwingine angeweza kusema/kuomba kufunguliwa au kuachana na njia ya Kristo. Sitaki kuteseka na kufa. Paulo anasema bila Yesu yote ni mavi, yote ni ubatili. Paulo atualika tuyafahamu mapenzi ya Mungu, lakini siyo ufahamu wa kujua suluhu ya tatizo fulani kama vile kupata jibu la tatizo fulani tu, bali aongelea uzoefu wa ndani unaoumba upya. Anatushirikisha mambo matatu makuu ya kutafakari katika ufahamu huu yaani katika kumjua Kristo; kuijua nguvu ya ufufuko wake, kushiriki ufufuko wake na kumjua Kristo mfufuka anayeshirikisha uweza wake kwao wamwaminio na wanaopenda kuwa naye. Aidha Mtume Paulo anatualika tupige mbio – ninapiga mbio, niifikie tuzo ya juu aliyoniwekea Mungu katika Kristo Yesu.

Mtume Paulo anatambua ukuu huu wa huruma ya Mungu na anamshukuru Yesu kwa mema yote aliyomjalia. Ingawa sisi tulikuwa wadhambi, yeye hakuona dhambi zetu ila alituletea msamaha toka kwa Baba. Anatukomboa toka hali yetu ya zamani. Huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu. Ili sisi tuweze kupata huruma ya Mungu, hatuna budi kutambua mahitaji yetu na maisha tunayoishi kila siku.

Mfano huu utusaidie pia katika tafakari yetu ya leo. Ilitokea siku moja Mfalme wa Urusi alitaka kutoa msamaha kwa mmoja kati ya wafungwa katika gereza kuu la mji. Yeye alitaka kutoa msamaha kwa mfungwa atakayesema wazi kile kilichomsibu mpaka akawa pale gerezani. Kila mfungwa alidai kuwa ameonewa na hakutendewa haki. Maana yake kila aliyeulizwa alisema hakustahili kuwa mahali pale. Mwishoni kabisa akatokea mfungwa mmoja aliyetamka wazi kosa lake na kukubali kuwa kuwepo kwake pale gerezani ilikuwa sawa kabisa. Huyu alikiri kosa lake. Mfalme akaamuru Bwana jela amfungue pingu na kumwacha huru kwa vile alikiri kosa lake. Bwana jela hakuelewa kabisa jambo hilo alilofanya mfalme kwamba aliyetaja waziwazi kosa lake ndiye anayepata msamaha. Mfalme akamwambia kuwa mtu aliyekiri kosa lake yuko katika kujijenga upya. Huyu anaweza kutenganisha jema na baya na hivyo akiwa makini hatakosa tena.

Wengi wetu hatufikii hatua hii ya kukiri na kukubali makosa. Na hii inagharimu sana maisha yetu na mahusiano kati yetu sisi na kati yetu na Mungu. Pia wengi wetu hatufikii upeo wa juu wa kujua na kukiri ukuu wa Mungu, hatujui mahitaji yetu vizuri na pia hatujui mahitaji ya wenzetu. Hali hii inatufanya tushindwe kutoa maombi sahihi kwa ajili yetu na pia kwa ajili ya wenzetu. Ombi la yule mama kwa Yesu juu ya binti yake linatutafakarisha sana. Ina maana kwamba yeye hakuwa na mahitaji binafsi? La hasha. Alichofanya ni ushuhuda tosha na fundisho kubwa katika imani yetu. Tunaalikwa kumwendea Yesu daima kwa ajili ya mahitaji yetu binafsi, ndugu zetu na majirani na kwa ajili ya taifa zima la Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.

17/08/2017 15:49