Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Imani thabiti inaokoa! Jaribu uonje ukuu wa Mungu!

Kila mtu mwenye imani thabiti anaweza kupata rehema na baraka kutoka kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai! - RV

17/08/2017 15:18

Mungu aliteua taifa la Israeli kuwa njia ya kuufikia wokovu wa wanadamu wote. Taifa hili liliandaliwa kwa makusudi kabisa ili kupitia kwake Mwanadamu aweze kuiona njia ya wokovu. Matendo mbalimbali ya Mungu kwa ajili ya kuwafadhilia watu hawa yalilenga katika kuwaandaa na kuutambaua upendo wa Mungu kwa watu wake. Tangu enzi za Waamuzi, Wafalme na Manabii Mwenyezi Mungu ametembea nao na kuwaokoa katika kadhia nyingi walizokumbana nazo. Wakati mwingine walipokaidi hakusita kuwahukumu kwa haki. Kilele cha upendo huu wa Mungu na pale alipomtuma Mwana wake wa pekee ili kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu. Kristo, Mwana wa Mungu anazaliwa katika jamii hii ya Wayahudi na anautimiza utume wake wote kati kati yao.

Lakini Kristo hakuzaliwa kwa ajili Wayahudi tu, wakati wa kuzaliwa kwake Malaika waliimba “Atukuzwe Mungu juu mbinguni na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia” (Lk 2:14). Ujio wake unaipatia dunia yote, yaani unaugusa ubinadamu wote kwa kuleta amani. Pamoja na hilo utume wake ulijikita katika jamii ya Wayahudi ili kupitia watu hawa waliondaliwa tangu awali basi ulimwengu wote uweze kuuonja wokovu wa Mungu. Injili ya Dominika hii inaonesha kwa namna fulani mbinu hiyo aliyonuia Kristo, yaani kulitumia Taifa la Israeli kama nyenzo kwa ukombozi wa wanadamu wote.

Mazingira na mazungumzo ya Kristo na mama mkananayo yanaweza yasieleweke vizuri na pengine kuwa kikwazo kwa wengine kuupokea utume wa Kristo. Kristo anasema: “sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli” anakwenda mbali na kutamka maneno yanayokera akisema “si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa”. Kwa juu juu inaweza kuonesha ubaguzi na dharau kubwa anayoionesha Yesu na pengine kupelekea kukwazika kwa wengi. Kama Yeye ametumwa kwa ukombozi wa wanadamu wote ni vipi ajibakize tu kwa waisraeli tena kwa kutamka wazi wazi? Pili kama kweli amekuja kumkomboa mwanadamu ni vipi wengine awalinganishe na mbwa?

Tukijisumbua kidogo na kusoma mahali pengine tutaona mazingira yanayokinzana. Katika Injili ya Mathayo sura ya 8 aya ya 7 Kristo anamponya mtumishi wa Akida wa Kapernaum ambaye alikuwa si Myahudi. Pia ni lazima kuelewa utamaduni wa mahali ambapo Kristo alikuwepo, yaani katika nchi za upagani ambapo mbwa alikuwa ni rafiki wa wanadamu na anakaa na watu nyumbani. Hivyo kusema kutupia chakula cha watoto mbwa ilieleweka kwa yule Mama mkananayo kwamba chakula kinaandaliwa kwa ajili ya watoto hakiwezi kupelekwa kwa mbwa hata kama ni rafiki wa binadamu.

Hivyo lipo linalopaswa kuangaliwa zaidi na kujifunza katika Injili ya dominika hii. Hii ni imani kwa Kristo kama Masiha. Mama mkananayo ni kielelezo kwetu kwa imani thabiti. Anaitambua haiba ya Kristo kwamba ni Masiya na hakuna chochote ambacho kilimtenganisha naye. Mama huyu anakuwa kinyume na Wayahudi ambao kwao walimtaka Kristo mwenyewe ajithibitishe kwa ishara na miujiza. Yeye anamthibitisha Kristo akisema: “Unirehemu, Bwana Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo”. Hivyo kwa imani yake binti yake akaponywa. Hapa anatuambia kwamba si lazima kukaa ndani ya maji ndipo utakate. Tunapaswa kuyafanya maji hayo yapite mwilini mwetu na kututakasa.

Pengine bado tunaweza kubaki kujiuliza kwa nini Kristo alitumia njia ngumu hivi hadi kumkubalia ombi lake? Hii ni mbinu mahsusi ya kupima uthabiti wa imani yake. Kristo anataka kumwona mama huyu kama anamkimbilia kwa sababu tu amesikia anafanya miujiza na uponyaji na hivyo anamchukulia kama mganga wa kienyeji vile au anayo imani kweli juu ya uwezo wake wa kimasiha. Mbinu hii ya kumngejelesha ilinuia katika kumkatisha tamaa; alitaka kuona kama anautambua ukuu wa Mungu ambao unapita mipaka ya fikra na tamaduni za kibinadamu. Imani yake kubwa na thabiti inamfungulia hazina za neema ya Mungu.

Nabii Isaya anaonesha nia hiyo ya Mungu ya kuwakomboa watu wote hata kwa wale walioonekana kuwa wageni. Neno la Mungu linatuambia kupitia kinywa cha Nabii Isaya kwamba: “Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabiu zao zitakubaliwa juu ya madhabau zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote”. Ahadi wanayoipokea wana wa Israeli ya kutoka utumwani haiishii kwao tu bali kwa mataifa yote na ukweli huu unathibitika wakati huu wa Yesu.

Hivyo, tunaweza kuielewa sentensi hii: “kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli” kuashiria jamii nzima ya waamini ambao kwa imani wanampokea Kristo kama Masiha. Imani yao kwa Kristo ndiyo inawastahilisha kupokea Baraka zote za mbinguni zinazofunguliwa kwa njia yake. Jumuiya hii mpya ya Waisraeli ambao msingi wake si wa damu au kuzaliwa katika Yerusalemu bali ni imani kwa Kristo mfufuka ndiyo jamii nzima ya waamini. Imani ya Kanisa ndiyo ambayo inalifanya kusonga mbele na kuwa sababu ya baraka na neema kwa watu wote. Hii inamaanisha kwamba uthabiti wako kiimani ndiyo unakupeleka katika wokovu.

Mtume Paulo anaonesha wazi jinsi ambavyo Wayahudi walivyoichezea nafasi ya dhahabu na kuwapelekea watu wa Mataifa kupata neema na baraka za Mungu. Ni onyo kwetu ambao tumefanywa wana warithi wa Mungu kwa njia ya Ubatizo na kuimarishwa na mapaji ya Roho Mtakatifu kuitambua hadhi yetu. Matendo yetu maovu ni sababu ya kumkataa Kristo na kumsukumia kwa wale tunaodhani wamepotea. Tunaweza kujikinai kuwa katika nafasi mbalimbali ndani ya jumuiya ya Kanisa, tunaweza kujidai na ujuzi wa elimu ya dini lakini matendo yetu hayamuakisi Mungu. Tunaendekeza ugomvi, unyonyaji, dhuluma, ugomvi na matusi na matendo mengine mengi yanayopingana na Kristo Masiha.

Tujitafiti nafsi zetu na tuepuke kuipoteza nafasi hii adhimu ya dhahabu tunayokuwa nayo. Tumefanyika kuwa wana wa Mungu hivyo basi tudumu katika imani thabiti kwake ili kuendelea kuchota neema na baraka zake kila siku za maisha yetu.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.

17/08/2017 15:18