2017-08-17 14:38:00

Familia ya Mungu Tanzania inamshukuru Mungu kwa zawadi ya Upadre


Kristo Yesu katika maisha na utume wake alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu na kusimika Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano. Akawachagua mitume wake kumi na wawili ili kusaidia mchakato wa uinjilishaji, huku wakisaidiwa na wafuasi wengine 72 waliotumwa kwenda kumwandalia Kristo Yesu, mazingira ya uinjilishaji. Alhamisi Kuu, siku ile iliyotangulizwa kuteswa kwake, Yesu aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu, kielelezo cha huduma makini inayomwilishwa katika Injili ya upendo na huduma.

Yesu aliwapatia mitume wake jukumu la kuwa ni: Manabii ili wahubiri Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa; Makuhani ili waweze kuwatakatifuza Watu wa Mungu kwa sala, sadaka na ushuhuda wa maisha yao; na Wafalme kwa kuwaongoza watu wa Mungu. Kimsingi, Padre ni ufunguo wa malango ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Miaka 100 iliyopita ilikuwa ni ndoto ya kufikirika kuweza kumpata Padre Mwafrika ambaye angeweza kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kama walivyofanya wamisionari!

Lakini, Kanisa Katoliki likawapatia hadhi Mapadre wa kwanza wazalendo, hapo tarehe 15 Agosti 1917 kama kilele cha hitimisho ya ndoto ya Askofu John Joseph Hirth alipowapata mapadre wanne wa kwanza wazalendo kutoka Tanzania na baadaye tarehe 7 Oktoba 1917 akawapata wawili kutoka Rwanda. Mashujaa hawa wa imani ni kama wafuatavyo:

PD. CELESTINE KIPANDA. Akitokea Kigunguli, Ukerewe Jimbo la Bunda.  

PD. ANGELO MWIRABURE Huyu alitokea Kome, Jimbo la Geita.

PD. OSCAR KYAKARABA   Alitokea Kashozi, Jimbo la Bukoba.

PD. WILLlBARD MUPAPI   Alitokea Kashozi, Jimbo la Bukoba.

PD. DONATUS REBERAHO Huyu alitokea Issavi Rwanda. Alipadrishwa Oktoba 7 1917,

PD. BALTHAZAR KAFUKO.  Alitokea Nsasa Rwanda alipadrishwa 7.10.1917

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Askofu Msaidizi Methodius Kilaini wa Jimbo Katoliki Bukoba, kama sehemu ya kilele cha maadhimisho ya Mwaka wa Padre, Tanzania, tarehe 15 Agosti, 2017, kwenye Kituo cha Hija Cha Mbwanga, Jimbo kuu la Dodoma, Kanisa lilipokuwa linaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa.

Askofu msaidizi Kilaini anaendelea kufafanua kwamba matunda ya sadaka na majitoleo ya Mapadre wazalendo ni kuanzishwa kwa Parokia ya Rubako kunako mwaka 1922 huko Jimbo Katoliki la Bukoba ambamo amezaliwa Kardinali Laurean Rugambwa, Askofu wa kwanza Mwafrika kutoka Tanzania na Kardinali wa kwanza Mwafrika bila kumsahau Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki Bukoba. Baadaye walifuatia Mapadre wengine waliendelea kupewa Daraja Takatifu ya Upadre sehemu mbali mbali za  Tanzania. Hii ni changamoto kwa Mapadre wa sasa kufuata nyayo za watangulizi wao daima wakiwa na furaha wanapojongea kwenye Altare ya Bwana, daima waendelee kupyaisha maisha na wito wao wa Kipadre, kwani wao wametwaliwa kati ya watu kwa ajili ya huduma ya mambo matakatifu na kwamba, hazina hii kubwa imehifadhiwa katika vyombo vya udongo!

Familia ya Mungu nchini Tanzania iendelee kuwaombea Mapadre wao ili wawe kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa; wawe mfano bora wa: upendo, umoja, udugu na mshikamano katika maisha na utume wa Kipadre, tayari kwenda sehemu mbali mbali za dunia kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Watambue kwamba, Kristo Yesu yuko pamoja nao hadi utimilifu wa nyakati!

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza anasema, huu umekuwa ni mwaka wa kumtolea Mwenyezi sifa na shukrani kwa zawadi, maisha, wito na utume wa Kipadre. Kanisa linamshukuru Mungu kwa uwepo wa kila Padre kwani kila Padre ni zawadi muhimu sana kwa maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho ya Mwaka wa Padre Tanzania imekuwa ni nafasi ya kwa familia ya Mungu Tanzania kuomba miito ya Kipadre, kwani mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache. Basi, waamini waendelee kumwomba Bwana wa mavuno ili aweze kupeleka watenda kazi wema, watakatifu na wachapakazi katika shamba lake.

Askofu mkuu Ruwaichi anakaza kusema, Mwenyezi Mungu ndiye anayeita, anayetoa zawadi hii kwa waja wake na hatimaye kuwaweka wakfu, ili taifa lake liweze kupata huduma linalohitaji wakati wote! Huu pia umekuwa ni mwaka wa kujitafakari, kujipima na kujichunguza katika maisha, wito, wakfu na utume wa Mapadre. Ili kuweza kumshukuru Mungu pale ambapo wametenda vyema; kuomba msamaha, toba na wongofu wa ndani, pale ambao mambo hayakwenda vyema, ili kuwa na ujasiri wa kuanza tena upya bila kukata tamaa. Maadhimisho ya Mwaka wa Padre Tanzania imekuwa ni fursa pia kwa familia ya Mungu kuangalia uhusiano wake na Mapadre wao, malezi na majiundo wanayowapatia Mapadre; jinsi wanavyojisadaka na kujitosa kwa ajili ya kuwaombea na kuwaenzi mapadre wao katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Ni nafasi pia kwa Kanisa zima kuthamini na kuendeleza zawadi ya wito wa upadre kutoka kwa Mwenyezi Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.