2017-08-16 14:00:00

Yaliyojiri kilele cha maadhimisho ya Mwaka wa Padre Tanzania!


Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka wa Padre nchini Tanzania yamekuwa ni muda maalum wa kumwimbia Mwenyezi Mungu na Kanisa utenzi wa sifa na shukrani kwa kulizawadia Mapadre wa kwanza wazalendo kunako tarehe 15 Agosti 1917 na tangu wakati huo, kumekuwepo na umati mkubwa wa Mapadre wa Majimbo na Mashirika kutoka Tanzania wanaoendelea kujisadaka sehemu mbali mbali za dunia kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha kwa watu wa Mataifa.

Kanisa linaendelea kujitahidi kutafakari kwa kina na mapana ukuu na utakatifu wa Fumbo la wito, maisha na utume wa Kipadre, ili kuweka bayana thamani yake isiyoweza kupimika kwa mizani ya kibinadamu, ili kulinda, kuhifadhi na kudumisha usafi na utakatifu wake kama wahudumu wa Mafumbo matakatifu ya Kanisa. Jambo la msingi kwa Mapadre ni kutambua kwamba, Kanisa linawahimiza kuwa kweli ni watumishi waaminifu, watakaomuakisi Kristo fukara, Kristo mtii na Kristo msafi katika useja! Huyu ni Kristo Yesu aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa kuwaondolea watu dhambi zao; kuwaganga na kuwaponya pamoja na kuwakirimia mahitaji yao msingi; mambo yanayofumbatwa katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima!

Kwa kutambua thamani, ukuu na utakatifu wa Daraja Takatifu ya Upadre, ndiyo maana Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania liliamua kuadhimisha Mwaka wa Padre Tanzania ambao umehitimishwa rasmi, tarehe 15 Agosti 2017, huko Jimbo kuu la Dodoma kwa kuhudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Tanzania! Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa na mahubiri kutolewa na Askofu msaidizi Methodius Kilaini wa Jimbo Katoliki Bukoba ambaye kimsingi ni bingwa wa historia ya Kanisa!

Askofu mkuu Marek Solczyński ametumia fursa ya kilele cha maadhimisho ya Mwaka wa Padre Tanzania ili kuweza kujitambulisha rasmi kwa familia ya Mungu nchini Tanzania baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa  Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapo tarehe 1 Agosti 2017. Barua ya utambulisho kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko iliyoandikwa kwa lugha ya Kilatini, ilisomwa na Askofu Damian Kyaruzi na baadaye kutafsiriwa kwa lugha ya kiswahili, ili kuwawezesha watu wa Mungu kuelewa ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko.

Katika maadhimisha haya, Askofu mkuu Marek Solczyński amebariki Pango la Bikira Maria lililoko kwenye Kituo cha Hija cha Mbwanga, Jimbo kuu la Dodoma na Askofu mkuu Protase Rugambwa amebariki Jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu Mapya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania yanayotarajiwa kujengwa Dodoma, baada ya Serikali ya awamu ya tano kuamua kuhamia Dodoma kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa maamuzi yaliyofanywa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, miaka zaidi ya 50 iliyopita!

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya, Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ambaye pia ndiye aliyekuwa mwenyeji wa maadhimisho ya kilele cha Mwaka wa Padre Tanzania amesema kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limeamua kuhamishia Makao yake Makuu kutoka Kurasini, Dar es Salaam kwenda Dodoma, Makao Makuu ya Tanzania. Kutokana na uamuzi huu, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bwana Jordan Rugimbana, kwa niaba ya Serikali ya Mkoa wa Dodoma ameamua kuchangia mifuko 100 kwa ajili kuharakisha ujenzi wa Kikanisa cha Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Katika kipindi cha siku 14, kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kinapaswa kuwa kimepatikana.

Maadhimisho ya kilele cha Mwaka wa Padre Tanzania yamehudhuriwa na Maaskofu 22, zaidi ya Mapadre 400 na kundi kubwa la watawa pamoja na familia ya Mungu katika ujumla wake. Itakumbukwa kwamba, kilele cha maadhimisho haya kilizinduliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Josep Mlola, Mlezi wa Umoja wa Mapadre Tanzania, UMAWATA. Katika mahibiri yake, aliwataka Wakleri nchini Tanzania kuimarisha upendo kati yao na familia ya Mungu nchini Tanzania katika ujumla wake, ili Tanzania iweze kuwa kweli ni nchi ya amani, upendo na mshikamano kati ya watu wake; kichocheo madhubuti cha maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili. Ibada hii ya Misa Takatifu, imeadhimishwa hapo tarehe 14 Agosti 2017, Kanisa lilipokuwa linafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe, Padre na Mfiadini aliyeacha chapa ya kudumu katika nyoyo za watu kama Padre Mkatoliki!

Askofu Msaidizi Methodius Kilaini wa Jimbo Katoliki Bukoba anasema, ndoto ya Askofu John Joseph Hirth ilitimia tarehe 15 Agosti 1917, miaka 100 siku ya leo, alipowapata mapadre wanne wa kwanza wazalendo kutoka Tanzania na baadaye tarehe 7 Oktoba 1917 akawapata wawili kutoka Rwanda. Mashujaa wetu ni hawa:

  1. PD. CELESTINE KIPANDA. Akitokea Kigunguli, Ukerewe Jimbo la Bunda.  
  2. PD. ANGELO MWIRABURE Huyu alitokea Kome, Jimbo la Geita.
  3. PD. OSCAR KYAKARABA   Alitokea Kashozi, Jimbo la Bukoba.
  4. PD. WILLlBARD MUPAPI   Alitokea Kashozi, Jimbo la Bukoba.
  5. PD. DONATUS REBERAHO Huyu alitokea Issavi Rwanda. Alipadrishwa Oktoba 7 1917,
  6. PD. BALTHAZAR KAFUKO.  Alitokea Nsasa Rwanda alipadrishwa 7.10.1917

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.