2017-08-16 14:20:00

Uchaguzi Mkuu Nchini Kenya: Ponyeni makovu ya utengano, jengeni umoja


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, KCCB, katika tamko lake mara baada ya kukamilika mchakato wa uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo tarehe 8 Agosti 2017 na Rais Uhuru Kenyatta kuibuka kidedea, wanawawataka wanasiasa pamoja na wananchi wote wa Kenya katika ujumla wao: kuchukuliana kwa unyenyekevu, upole, uvumilivu na upendo na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa roho katika kifungo cha amani. Wanawashukuru na kuwapongeza wananchi wote walioonesha uvumilivu na ustahilimivu wa kushiriki katika zoezi la kupiga kura kwa kujipanga mistari mirefu ili kutekeleza wajibu wao wa kikatiba wa kuwachagua viongozi wanaowataka. Wanawapongeza wananchi walioshiriki kulinda na kudumisha amani na utulivu, kielelezo makini cha uzalendo na demokrasia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linapenda kuchukua fursa hii kumpongeza Rais mteule Uhuru Kenyatta kwa kuchaguliwa tena kuwaongoza wananchi wa Kenya katika awamu ya pili. Wanawapongeza pia viongozi waliojitokeza kuwania kiti cha Urais wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu. Kwa namna ya pekee, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linapenda kuipongeza Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya, IEBC pamoja na kukazia mambo kadhaa ili kuhakikisha kwamba, inazivalia njuga changamoto zinazoendelea kujitokeza mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu.

Maaskofu wanamwomba Rais mteule na Serikali yake kuhakikisha kwamba, inajizatiti zaidi katika kuganya na kuponya madonda ya mpasuko wa kijamii yaliyojitokeza wakati wa zoezi zima la uchaguzi, ili kuanza mchakato wa umoja wa kitaifa na mafungamano ya kijamii na kwamba, kila Jumuiya itapewa uzito inayostahili na wala haitaweza kutengwa kutokana na mchakato wa uchaguzi mkuu au kuwashughulikia watu kadiri ya maeneo wanamotoka! Wanawataka wanasiasa kwa namna ya pekee kabisa kuwa makini kwa maneno wanayotumia na jinsi ya kuwasiliana na wananchi ili kweli waweze kuwa ni sehemu ya mchakato wa umoja wa kitaifa, amani na maridhiano.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linavipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri vilivyofanya katika kulinda na kudumisha: ulinzi, amani na utulivu wakati wa zoezi zima la uchaguzi mkuu. Wanavitaka kuwa makini ili visitumie nguvu kubwa vinapokabiliana na makundi ya watu, kwa kuheshimu utakatifu wa maisha wanapotekeleza dhamana na wajibu wao kwa jamii ya Kenya. Maaskofu wanasikitishwa sana na taarifa za vifo vya wananchi wasiokuwa na hatia pamoja na uhribifu mkubwa wa mali za watu. Maaskofu wanavitaka vyombo vya ulinzi na usalama kulinda maisha ya wananchi na mali zao na kamwe kusiwepo tena vifo vya watu kutokana na uchaguzi mkuu uliopita!

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika tamko lake lililotiwa mkwaju na Askofu Philip Anyolo, Rais wa Baraza hili anakaza kusema, uchaguzi umekwisha na Tume huru ya uchaguzi na mipaka imetangaza matokeo ya uchaguzi mkuu! Wanasikitishwa sana na hali tete ambayo imezuka baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu kutangazwa. Maaskofu wanawataka wanasiasa ambao hawakuridhishwa na matokeo kutumia sheria ili kuhakikisha kwamba,  haki yao inapatikana kadiri ya Katiba ya nchi. Wanawakumbusha wananchi wote wa Kenya kwamba, uchaguzi umekwisha na kwamba, sasa wanapaswa kurejea katika maisha yao ya kila siku na kuviachia vyombo vinavyohusika na uchaguzi mkuu kutekeleza dhamana na wajibu wake. Maaskofu wanahitimisha tamko lao kwa kusema wanapenda kuwahakikishia wananchi wote wa Kenya uwepo wao wa karibu kwa njia ya sala.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.