2017-08-16 15:08:00

Mshikamano wa upendo na wananchi wa Afrika ya Kati!


Askofu mkuu Ludwig Schick, Mwenyekiti wa Tume ya Kanisa Ulimwengu, Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani, kuanzia tarehe 16 hadi tarehe 23 Agosti 2017 anafanya ziara ya upendo na mshikamano nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, ili kuweza kujionea mwenyewe shida na mhangaiko ya wananchi ambao kwa sasa wanakabiliwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe kutokana na uchu wa mali na madaraka. Wananchi wengi wamekumbwa na baa la njaa kutokana na ukame wa kutisha na ukosefu wa usalama, amani na utulivu. Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watu 180, 000 wameikimbia miji ya Bria, Alindao na Baungassou kutokana na vita na ghasia kupamba moto kwa siku za hivi karibuni!

Askofu mkuu Ludwig Schick akiwa nchini Jamhuri ya watu wa Afrika ya Kati, atawasilisha msaada wa mshikamano na upendo kutoka kwa familia ya Mungu nchini Ujerumani, dhamana inayotekelezwa na familia pamoja na vyama mbali mbali vya kitume, vinavyoguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wananchi hao. Anakutana na viongozi wa Kanisa pamoja na viongozi wa waamini wa dini ya Kiislam nchini Jamhuri ya watu wa Afrika ya kati. Hii itakuwa ni fursa pia ya kukutana na kuzungumza na Jukwaa la Viongozi wa Kidini nchini Jamhuri ya watu wa Afrika ya Kati ambalo linakutana kwa mara ya kwanza, tangu mwaka 2013 baada ya kufumuka tena mapigano na mkataba wa amani, kuwekwa ghalani! Itakuwa ni nafasi pia ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya watu wa Afrika ya kati, mabalozi wanaowakilisha nchi zao pamoja na baadhi ya wabunge.

Askofu mkuu Ludwig Schick anaianza safari hii kwa kutembelea kwanza nchini Cameroon, ili kukutana na kuzungumza na Kardinali Christian Tumi pamoja na viongozi wawakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon, ili kuzungumzia hali tete ya machafuko inayoanza kujitokeza huko Cameroon kutokana na wananchi kugawanywa kwa misingi ya lugha wanayozungumza yaani: kifaransa, kielelezo cha watu walioendelea zaidi na kiingereza ni “kwa akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.