2017-08-16 15:29:00

Kilele cha Mwaka wa Padre Tanzania: Ukuu, Utakatifu na Wito wa Upadre


Bwana ameapa, Wala hataghairi, Ndiwe kuhani hata milele, Kwa mfano wa Melkizedeki. (Zab.110:4) Huu ndio ujumbe Mkuu wa leo kwetu ndugu zangu mapadre, na ndugu zangu waamini wapendwa. Tumekuja hapa kuadhimisha na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa zawadi ya upadre Tanzania. Miaka 100 iliyopita siku ya leo ndipo Kanisa Katoliki Tanzania tulipata makuhani wa kwanza wazawa, mapadre wa kwanza wazawa. Tushangilie na kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Bwana wetu Yesu Kristo, Nafsi ya Pili ya Mungu alijifanya mwanadamu ili atukomboe. Duniani alihubiri Ufalme wa Mungu na kwa ajili ya hilo aliwatayarisha kwa karibu sana mitume 12 na vile vile wafuasi 72 ili waendeleze kazi aliyoianza na aliyoitegemeza. Siku ya Alhamisi Kuu aliwapa uwezo, aliwaweka wakfu akiwapa majukumu ya kuwa Manabii, Makuhani na Wafalme. Kuwa Padre ni kuwa hayo mambo makuu matatu. Manabii ili wahubiri Habari njema. Aliwatuma akisema Nendeni Duniani Kote mkawafanye wote wawe wanafunzi wangu. Makuhani ili watakatifuze. Kilele chake ni pale alipochukua mkate  akaubariki na kuwapa wafuasi wake akisema: “Twaeni mle nyote huu ndiyo Mwili wangu”, na divai hivyo hivyo alisema “Twaeni mnywe nyote hii ni damu yangu......akamalizia na maneno  FANYENI HIVI KWA UKUMBUSHO WANGU. Tangia hapo Padre siyo tu humwakilisha Kristo bali hufanya kwa nafsi ya Kristo mwenyewe. Ni Kristo mwingine. Hasemi huu ni Mwili wa Kristo bali husema “Huu ni Mwili wangu”, husema “Nakuondolea dhambi zako”, nk.  Anakuwa mfalme atawale na kuamua kwa jina la Bwana Wetu Yesu Kristo.”Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni” (Mt.18:18 )

Wapendwa huu wadhifa anaoupata Padre ni mkubwa mno na unaogopesha. Hakuna anayestahili ila kwa nguvu zake Mungu. Mt. Paulo kwa Waebrania anatuambia kwamba “Na hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni. (Heb. 5:4)”  Mtakatifu Yohana Maria Vianney Msimamizi wa Mapadre anaandika akisema “ni ukubwa ulioje upadre! Kama Padre angelitambua ukubwa wake angelikufa kwa mshtuko wa upendo; Mungu anamtii na kushuka toka mbinguni kwa wito wa sauti yake katika Ekaristi Takatifu”.

Padre ndiye ufunguo wa ukombozi kwa sababu bila yeye milango yote imefungwa na hazina zote zilizomo, kwa sababu anaingiza binadamu katika ushirika wa ukombozi kwa Ubatizo, anamtibu anapougua kwa dhambi kwa Sakramenti ya Kitubio, anampa chakula cha uzima ambaye ni Bwana wetu Yesu Kristo katika Ekaristi Takatifu, anaunda familia kwa kushuhudia na kubariki pingu za Ndoa Takatifu, anampa tumaini na nguvu mgonjwa kwa Sakramenti ya Mpako na mwishoni anamfungia pamba ya njiani au viatiko ya mwisho anapokufa na kwenda kwa Baba mbinguni. 

Miaka 100 iliyopita sehemu kubwa ya Afrika ilikuwa chini wa wakoloni. Wakoloni wengine walitia mashaka hata utu wa Mwafrika na kwa mantiki hiyo walimdhalilisha sana. Ni wakati huo Kanisa Katoliki liliwapa hadhi kubwa sana waafrika kuwafanya mapadre sawa kama wazungu. Hili halikuwa rahisi. Tumshukuru Askofu wa Vikariati ya Nyanza ya Kusini John Joseph Hirth ambaye aliamini sana katika uwezo wa Mwafrika. Wakati huo siyo tu wakoloni lakini hata wamisionari wenzake hawakukubaliana naye. Kwa mfano hata gambera wa seminari yaani mwalimu na mlezi mkuu akiandika nyumbani alisema “Tuko tunashughulika kupanda na kutunza mbegu seminarini, mwisho wa siku tukiwapata makatekista wazuri wa kuwasaidia wamisionari  tutafurahi na kuridhika.”

Mwaka 1909, vijana wa kwanza walipomaliza masomo ya sekondari, na Askofu Hirth alipotaka kufungua seminari Kubwa hapo Rubya alipata upinzani mkubwa.  Mkuu wa misioni (Provincial Pd. Leonard) alilipoti hivi makao makuu “Kwangu mimi sasa iko wazi kabisa kwamba Askofu Hirth anakosea juu ya vijana hawa, mimi sioni chochote ndani yao. Mungu tu ndiye anajua ni mbegu gani ya wito Askofu anaona ndani ya vijana hawa.” Lakini Askofu Hirth akiwa na nguvu zake Roho Mtakatifu alijikaza akaendelea mbele. Alifurahi mwaka 1910 vijana wake 9 wa kwanza walipopata tonsura na baadaye vazi la kanzu la Uklero, ni hapo mmojawapo Celestine Kipanda kutoka Kagunguli, Ukerewe alipomwandikia mfadhili wake kupitia kwa Mkuu wa Shirika akisema: “Hili vazi la ukleri tulilolipata linatuhamasisha na kututia nguvu kwamba Mungu Mwema ameliweka Kanisa lake siyo tu kwa ajili ya watu weupe lakini hata kwetu watu weusi maskini na wengine wote aliowaita katika utukufu wake.” Askofu Hirth alipoisoma barua hii alitokwa machozi ya furaha.

Ndoto ya Askofu John Joseph Hirth ilitimia tarehe 15 Agosti 1917, miaka 100 siku ya leo, alipowapata mapadre wanne wa kwanza wazalendo kutoka Tanzania na baadaye tarehe 7 Oktoba 1917 akawapata wawili kutoka Rwanda. Mashujaa wetu ni hawa:

  1. PD. CELESTINE KIPANDA. Akitokea Kigunguli, Ukerewe Jimbo la Bunda.  
  2. PD. ANGELO MWIRABURE Huyu alitokea Kome, Jimbo la Geita.
  3. PD. OSCAR KYAKARABA   Alitokea Kashozi, Jimbo la Bukoba.
  4. PD. WILLlBARD MUPAPI   Alitokea Kashozi, Jimbo la Bukoba.
  5. PD. DONATUS REBERAHO Huyu alitokea Issavi Rwanda. Alipadrishwa Oktoba 7 1917,
  6. PD. BALTHAZAR KAFUKO.  Alitokea Nsasa Rwanda alipadrishwa 7.10.1917

Bahati nzuri mapadre hawa wa kwanza walikuwa shupavu, watauwa na watenda kazi. Kwa mfano Padre Angelo Mwilabure, Mzinza wa ukoo wa Wazigaba kutoka Kome, Geita ndiye alikuwa paroko wa kwanza mzawa hapa Tanzania. Akishirikiana na Padre Oscar Kyakaraba, mwaka 1922 alifungua Parokia ya Rutabo. Hii parokia imeendeshwa na mapadre waafrika na ni parokia yenye ufanisi mkubwa sana jimboni Bukoba. Pamoja na kuzaa mapadre wengi na watawa, parokia hii ilimzaa Laurean Rugambwa, Askofu wa kwanza Mwafrika Tanzania na Kardinali wa kwanza Afrika na vile vile  Askofu Desiderius Rwoma wa jimbo la Bukoba. Mapadre wa kwanza walionesha kwamba Askofu Hirth hakukosea, walidhihilishia ulimwengu uwezo wa mwafrika na kumletea heshima na hadhi kubwa.

Mapadre hawa mashujaa waliwafungulia milango mapadre wengine wazalendo siyo tu Vikariati ya Nyanza Kusini lakini Tanzania nzima.

Mapadre wapendwa tufuate nyayo za hawa watangulizi wetu na kila siku tuje mbele ya Bwana tukifurahi na kuimba: “Nitajongea altare yako, Furaha yangu na heri yangu siku zote”. Miaka 45 iliyopita nikiwa na miaka 23 niliandika hilo juu ya kumbukumbu yangu ya upadre. Na sasa miaka 45 baadaye, nikiwa nimepigika, kichwa cheupe, kasi imepungua, bado naimba kwa furaha kubwa “Nitajongea altare yako.... Mapadre wapendwa hiyo ndiyo furaha yetu kubwa kama ilivyokuwa kwa maelfu ya mapadre kabla ya yetu na itakuwa hivyo kwa watakaokuja baada yetu. Hakuna anayeweza kukunyanganya kama tunaishika kwa nguvu na utashi wetu wote, hautachoka. Utabaki fresh daima.

Mtakatifu Paulo anatukumbusha kwamba “Maana kila kuhani mkuu alitwaliwa katika wanadamu na amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi; aweze kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu”. (Heb. 5:1-2). Padre hadondoki kutoka mbinguni bali hutoka kati ya binadamu, hutoka katika familia, hutoka ulimwenguni. Padre ni kiumbe dhaifu aliyewezeshwa na Mungu. Kwa maneno ya Mt. Paulo kwa Wakorinti  “Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu.” (2 Kor. 4:7) Padre si malaika. Hivyo lazima asaidiwe, ategemezwe, aombewe na kupendwa. Padre akijikwaa na kuanguka apate nguvu tena za kuamka na kumtumikia Bwana. Leo sisi mapadre kama Baba Watakatifu walivyofanya: ni siku licha ya kushangilia na kushukuru ni siku ya kuomba msamaha kwa Mungu, kwa waamini na watu wote pale ambapo tumekosea, ambapo tumekwaza na ambapo hatukutimiza wajibu wetu ipasavyo. Tuaahidi kuafanya juhudi zote kutimiza wajibu wetu kwa msaada wa neema yake Mwenyezi Mungu.

Tuombee na kutegemeza miito. “Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache.  Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake”. (Mt. 9:37-38) Hivyo wapendwa, tumwombe Mungu atume watendakazi tena wazuri katika shamba lake. Vile vile waamini wapendwa tuwategemeze mapadre wetu kwa sala na ibada, kwa hali na mali, kwa upendo na ushauri na kwa ushirikiano na umoja. Watawa wapendwa, kwa namna ya pekee dada zetu masista, tunajua kwamba mnatuombea sana, endeleeni kutuombea tuongezeke na tuwe watakatifu, tuwe chumvi ya kukoleza dunia na tuwe taa ya kuangaza ulimwengu. Mtuombee tuwe na umoja,  tupendane na kushirikiana kati yetu karibu katika kufanya kazi ya Bwana.  “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma”. (Jn. 17:21) Leo Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho,umwombe huyu Mama wa Mapadre atuombee na kutubeba kama alivyowabeba mitume. Huyu ndiye Mama yako, alituasa Bwana kupitia Mtume Yohana.

Mwishowe ,tukiwa tunaadhimisha miaka mia moja ya mapadre wa kwanza, Bwana wetu Yesu Kristo anatutuma tena “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.  Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;  na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” (Mt. 28:18-20) Kila mmoja wetu Bwana anatuuliza kama alivyomwuliza nabii Isaiya “Nimtume nani” tumjibu bila kusita hata siku moja “Mimi hapa, nitume mimi”. Lije jua, ije mvua, safari tambarare au ya milima, lazima kila mara kujibu “Mimi hapa, nitume mimi”. Mapadre wapendwa kama asemavyo Mt. Paulo “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Ni nini kitatutenga na utumishi wa Bwana? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?   Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. (Rm. 8:35).

Katika Kristo aliyeshinda mauti, mauti ya Msalaba tunapata nguvu. Bwana yuko pamoja nasi hata ukamilifu wa dahari. Tunapoanza miaka mingine mia moja ni wakati wa kuamsha ari na hamasa yetu katika wito wetu. Ni wakati wa kutazama mbile na kuitikia upya wito wake wa kwenda kuwafanya wote wanafunzi wa Kristo. Hivyo sote tunaitikia na kuimba kwa sauti moja kwamba tuko tayari. “Nimtume Nani” “Unitume mimi nitume Bwana, Nitakwenda kutangaza Neno lako wewe, Mataifa yasikie yakufuate wewe, unitume mimi nitume Bwana”.

Na Askofu Method Kilaini.

Jimbo Katoliki Bukoba, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.