2017-08-15 14:24:00

Papa Francisko awakumbuka na kuwaombea waathirika wa majanga asilia


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 15 Agosti 2017 wakati Kanisa linaadhimisha, Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho, amewakumbuka, akawaombea na kuwahifadhi katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa amani, watu wote wanaoteseka kutokana na athari za majanga asilia sehemu mbali mbali za dunia. Watu wanaoteseka kutokana na vita, ghasia, kinzani na mipasuko ya kijamii, ili wote hawa waweze kupata amani, utulivu na usalama wa maisha yao!

Taarifa kutoka Sierra Leone zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu 312 wanaohofiwa kupoteza maisha kutokana na mvua kubwa iliyonyeesha, Alfajiri siku ya Jumatatu tarehe 14 Agosti 2017 na hivyo kusababisha mafuriko na maporomoko ya udongo. Zaidi ya watu 6,000 hawana makazi na kwamba, hadi sasa juhudi za kuwaokoa watu walionaswa na mafuriko pamoja na maporomo ya udongo zinaendelea na kwamba, pengine, idadi ya watu waliofariki dunia, ikaongezeka maradufu. Hali ya maafa ni kubwa kiasi kwamba, kuna watu wameanza kukata tamaa kutokana na machungu wanayokumbana nayo mbele yao kwa wakati huu. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF  linasema kwamba, vyanzo vikuu vya maji safi na salama vimeharibiwa hali inayotishia kuzuka kwa magonjwa ya milipuko!

Mafuriko na maporomoko ya ardhi ni jambo la kawaida kwa Nchi za Afrika ya Magharibi, kutokana na ukosefu wa mipango miji na ujenzi usiozingatia ubora na viwango vinavyotakiwa! Uharibifu mkubwa wa misitu ni kati ya mambo yanayoendelea kuchangia kwa athari za mabadiliko ya tabianchi. Mji wa Free town unakaliwa na watu zaidi ya milioni 1.2 na umekuwa ukikumbwa na mafuriko mara kwa mara kiasi cha kuharibu miundo mbinu na hivyo kupelekea kuzuka kwa magonjwa ya milipuko! Kunako mwaka 2015, watu 10 walipoteza maisha baada ya Mto kufurika na kusababisha maelfu ya watu kukosa mahali pa kuishi. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 2014, Sierra Leone, ilikuwa ni kati ya nchi ambazo zilikumbwa vibaya sana na ugonjwa wa Ebola na hivyo kupelekea watu zaidi ya 4, 000 kupoteza maisha na madhara yake kusikika katika medani mbali mbali za maisha ya wananchi wa Sierra Leone.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.