2017-08-15 14:55:00

Mwenyeheri Oscar Romero ni "Jembe" lililokatika kabla ya wakati wake!


Katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, iliyotangazwa na Papa Pio XII hapo tarehe 1 Novemba 1950 kama sehemu ya mafundisho ya Imani tanzu ya Kanisa kwamba, Bikira Maria aliyekingiwa na kila doa la dhambi ya asili, baada ya kuhitimisha maisha yake hapa duniani alipalizwa mbinguni mwili na roho akatukuzwa na Bwana kama Malkia wa ulimwengu ili aweze kufananishwa zaidi na Mwanaye, aliye Bwana wa mabwana. Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni wanasema Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican anang’aa duniani kama alama ya hakika ya matumaini na faraja kwa taifa la Mungu lililo safarini, mpaka siku ile Bwana atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu! Hii ni kati ya Sherehe kongwe kabisa zinazoadhimishwa na Kanisa la Mashariki kama “Dormitio Virginis” au “Kulala kwa Bikira Maria” na Makanisa ya Magharibi yanaiadhimisha Sherehe hii kama “Assunta” yaani “Kupalizwa kwa Bikira Maria”.

Wakristo wanaposherehekea Siku kuu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, wakimbilie tunza na maombezi ya Bikira Maria aliyeusaidia mwanzo wa Kanisa kwa maombezi yake na sasa ametukuka mbinguni awaombee watoto wake umoja na mshikamano katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Familia yote ya Mungu idumu katika: haki, amani na maridhiano kwa utukufu wa Ufumbo la Utatu Mtakatifu.

Sherehe hii ni kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Mwenyeheri Oscar Armulfo Romero alipozaliwa. Kwa hakika alijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake kama Askofu kwa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Alikuwa ni kiongozi na shuhuda wa Injili ya Kristo; mtetezi wa maisha na utume wa Kanisa; aliyesimama kidete kulinda na kutetea: utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Alikuwa ni sauti ya kinabii kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii! Alikuwa ni chombo na shuhuda wa huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake! Kama Padre na Askofu akasimama kidete kutetea haki, amani na upatanisho kiasi hata cha kumgharimu maisha yake. Alijikita katika majadiliano kati ya Kanisa na walimwengu, changamoto endelevu hata kwa watu wa nyakati hizi.

Kardinali Richardo Ezzati Andrello, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Santiago de Chile, mwakilishi wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya anasema, huu ndio urithi endelevu na amana ya Kanisa kutoka kwa Mwenyeheri Oscar Armulfo Romero, Kanisa linapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 100 tangu alipozaliwa! Kardinali Richardo Ezzati ameyasema haya wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kama kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu Mwenyeheri Oscar Romero alipozaliwa. Hii ni changamoto ya kujizatiti kikamilifu katika kukuza na kudumisha mchakato wa amani na utulivu duniani. Katika maadhimisho haya, waamini wametembea kilometa 150 kwa muda wa siku tatu huko San Salvador na hatimaye, Kardinali Gregorio Rosa Chàvez, Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la San Salvador, huko El Salvador, akawaunga mkono.

Kardinali Richardo Ezzati Andrello amewapongeza na kuwashukuru waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwa kushiriki kwa wingi katika kuenzi yale mambo msingi yaliyosimamiwa kwa dhati kabisa na Mwenyeheri Oscar Armulfo Romero. Anakaza kusema, huu ni ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo; kielelezo cha ndoto ya Kanisa la Baba Mtakatifu Francisko anayelitaka Kanisa kutoka kifua mbele ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu: aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa watu, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo. Hili ni Kanisa linalotaka kujikita katika msingi kwa kutambua kwamba, linalo dhamana na utume wa kimisionari wa kuwatangazia watu wa Mataifa Furaha ya Injili, Imani, Matumaini na Amani!

Amewataka vijana wa kizazi kipya, walioshiriki kwa wingi kuiga mfano wa maisha na utume wa Mwenyeheri Oscar Romero kwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani; kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Amewataka vijana kuondokana na uchu wa mali na madaraka; rushwa na ufisadi, saratani inayopekenyua na kuharibu misingi ya haki, amani na mafungamano ya kijamii na badala yake, wawe ni vyombo na wajenzi wa: haki, amani, udugu na mshikamano wa kitaifa. Mwenyeheri Oscar Romero alikuwa ni shuhuda makini wa maisha na utume wa Kanisa; kiongozi mwaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, aliyetambua na kuthamini utamaduni wa kusikiliza kwa makini wale wote waliomwendea kutaka ushauri kutoka kwake! Ibada hii ya Misa Takatifu imeongozwa na Askofu mkuu Josè Luis Escobar Alas wa Jimbo kuu la San Salvador.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.