2017-08-14 09:19:00

Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni na Mwaka wa Padre Tanzania


Mataifa mengi hapa duniani yametenga siku ya mapumziko kwa raia wake. Kwa Waitalia siku hiyo inaitwa Ferragosto yaani mapumziko ya mwezi wa Agosti yanayoangukia tarehe 15 ya mwezi huo. Ferragosto ni kama weekend ndefu ya mwezi mzima wa Agosti. Mapumziko ya Ferragosto yalianzishwa na mfalme Augusto mwaka wa 18 kabla ya Kristo. Tarehe hiyo hiyo Kanisa Katoliki linasherehekea sikukuu ya kutwaliwa Bikira Maria mbinguni. Siku hiyo ni mapumziko ya kitaifa na kikanisa. Mwaka huu Kanisa Katoliki nchini Tanzania, limechagua tarehe 15 Agosti, 2017 kusherekea Jubilei ya miaka 100 kutoka pale alipopata ukasisi padre mzalendo wa kwanza wa Tanzania. Kwa hiyo mwaka huu tunabahatika kusherekea sikukuu mbili kwa siku moja, yaani kupalizwa mbinguni kwa Mama yetu Bikira Maria, mwili na roho pamoja na kufunga mwaka wa Jubilei ya miaka mia moja ya mapadre wazalendo nchini Tanzania.

Kulikoni sikukuu mbili  kwa siku moja? Matendo makuu ya Mungu kwa waja wake!

Tunaweza kujihoji endapo kuna uhusiano na maana yoyote ile kwa waumini wa kanisa la Tanzania hususani kwa mapadre wenyewe kusherekea siku moja sikukuu hizi mbili. Ndugu zangu, kwa harakaharaka tunaweza kusema:  Bikira Maria ni mama wa Yesu Kristo aliye Kuhani (padre), Nabii na Mfalme. Vyeo hivyo vya Yesu anavipata kila mkristo anapobatizwa na anapopewa Sakramenti ya kipaimara. Hapo mkristu anapakwa mafuta ya Krisma na kurithi cheo cha Kristo: Kuhani, Nabii na Mfalme. Kadhalika mapadre waliowekewa mikono na kupakwa tena Krisma wanakuwa Kristo mwingine. Ikumbukwe pia kwamba, zamani wafalme walipakwa mafuta. Kwa hiyo Mama wa Yesu ni Mama wa Wakristo wote, na ni Mama wa mapadre wote, hata mama wa viongozi wote.

Kuhani amekabidhiwa na Yesu kazi zile zile za Yesu yaani, kuhubiria ulimwengu habari njema ya Mungu. Kuwepo karibu na watu wote kutoka wanapozaliwa hadi wanapokufa. Kuhani ameitwa na kutumwa kufanya kazi hizo na Mwana wa Maria pale aliposema: “Kama Baba alivyonituma mimi, nami pia nawatua ninyi.” Yoh. 20:21). “Siyo ninyi mlionichagua mimi, bali mimi ndiye niliyewachagua ninyi, na nimewaweka ili mwende mukazae matunda, na matunda yenu yadumu… Kama ulimwengu unawachukia, mjue kwamba ulimwengu ulinichukia mimi kwanza kabla ya kuwachukia ninyi. Kama ninyi mngekuwa wa ulimwengu, basi ulimwengu ungewapenda, lakini kwa vile ninyi siyo wa ulimwengu, kwa vile nimewachagua kutoka ulimwenguni, kwa hoja hiyo ulimwengu unawachukia.” (Yoh. 15:16…). “Haya mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa mwitu. Muwe basi wenye busara kama nyoka na wanyofu kama njiwa.” (Mt. 10:16). “Anayewasikiliza ninyi, ananisikiliza mimi, anayewadharau ninyi, ananidharau mimi.” (Lk 10:16).

Uchungu wa Mwana aujua Mama

Ndugu zangu, hata kama kuhani angeinuliwa katika hadhi ya juu namna gani, huyo anabaki daima kuwa Mwana wa Adam, mwenye kurithishwa dhambi ya asili. Kadhalika ibilisi anayo hasira na wivu mkali sana dhidi ya Makuhani hao. Anafanya juu chini kuwazuia Makuhani wasiziokoe roho za watu. Kwa hiyo Kuhani anahitaji msaada wa pekee ili aweze kutekeleza na kutimiza vyema majukumu yake ya kikuhani. Mama Maria anatambua vizuri sana mahitaji ya Kuhani hao wa Mwanae. Anawaombea neema nyingi ili waweze kuokoa roho na kuzitakatifuza; anawatunza kwa namna ya pekee, kama alivyokuwa anafanya kwa mitume wa kanisa la awali. Bikira Maria anamwona Mwanaye Yesu katika kila padre na anaitunza roho ya kila padre kama mboni ya jicho lake. Maria anajua hatari iliyolala mbele ya Padre, hasahasa wakati wetu huu wa maovu yaliyo mbele yao na hila za shetani dhidi yao. Lakini Mama mpendwa hawaachi watoto wake katika mapambano hayo na anawalinda na kuwafunika kwa bushuti lake. Kadhalika Mapadre kwa maombezi ya Mama Maria, wanawalinda waumini dhidi ya udanganyifu na ulaghai wa maadui wa Mungu.

Mama ni tumaini la Wakristo

Sikukuu ya kupalizwa Bikira Maria mbinguni, inatukumbusha watu wote, kwamba kwa njia ya Maria Mungu anatudhihirishia umaana wa uwepo wetu hapa duniani na kwamba sisi siyo akina “kufa basi” bali tunayo maisha zaidi. Aidha tunayo maisha yaliyotukuka kwa sababu kutukuzwa kwa Mama wa Yesu siku ya leo kunatuhakikishia kutukuzwa kwetu pia, yaani kwa kuchukuliwa Bikira Maria mbinguni mwili na roho hata sisi tunapata matumaini kwamba kuna umilele unatusubiri. Kwamba kuna Paradisi ambako Mama wa Mungu na Mama yetu anatusubiri akiwa pamoja na Mwanae tunayempigania hapa duniani.

Ushindi katika Mungu

Lakini ushindi na kutukuzwa huko kwa Mama kulimtegemea Mungu. Kama tunavyosoma katika somo la kwanza kutoka Ufunuo wa Yohane. Mwanamke aliyevikwa jua, na wezi miguuni pake, kichwani aliveshwa taji la nyota kumi na mbili zilizo alama ya jumuia ya wakristu waliozungukwa na Joka jekundu ambalo ni alama ya ubaya na uovu. Kwa vile Wakristu wa awali waliokuwa wanadhulumiwa sana, walipata kitulizo na matumaini katika imani yao. Mwanamke huyo anaokolewa na Mungu na kwenda jangwani. Kwa hiyo, Mama huyo anatoa mwanga kwa maisha na matumaini mapya. Picha hii ya mwanamke anayeokolewa kutoka kwenye mdomo wa joka inatukumbusha kuokoka kwetu kutokana kwa mama wa kwanza Eva na tunakabidhiwa sasa kwa Mama Eva mpya. Hii ndiyo picha ya mapokeo ya kihistoria ya Wakristu juu ya Maria. Katika Maria unapata picha ya ushindi wa ubinadamu. Kwamba utu wa mtu uliokandamizwa na ukiritimba wa Watawala dhalimu wa ulimwengu huu, sasa utu huo umepata tena hadhi yake. Lakini ushindi huo unatoka kwa Mungu ndiye anayetupigania kama alivyompigania Mwanae na Mama yake.

Maria ni Balozi wetu Mbinguni

Somo la pili linatoka Barua ya Kwanza ya Paulo kwa Wakorinto, ambayo inatangaza imani ya mkristu juu ya maisha: “Kama vile katika Adamu wote tunakufa, ndivyo katika Kristu sisi sote tunapokea maisha.” (IKor. 15:22). Kwa hiyo kifo ni tamthilia ambayo kila mtu wa kila nyakati aliyeishi hapa duniani amekikataa kabisa kukikubali. Hata Warumi waliokuwa watafiti wakuu wa maisha walijaribu kukikana kifo waliposema: “Non omnis moriar.” Sitakufa moja kwa moja. Lakini haina budi kueleweka kwamba, wakristo hata makuhani hawana majibu kwa maswali yote yahusuyo uzima na kifo, kuishi na kufa. Sisi sote tunashuhudia kwa macho yetu jinsi kifo kinavyotumaliza. Tunaona binadamu anakufa na kutoweka machoni petu na tunabaki kulia na kutikisa vichwa tukisema: “Mapenzi ya Mungu yatimizwe.” Lakini imani ya mkristo iliyojengwa juu ya imani ya ufufuko wa Kristo, ndiyo inayoibua pia utukufu wa Maria. Maria aliyeinuliwa kwenye utukufu wa mbinguni mwili na roho, anawakilisha siku ya leo kama mfano na nembo ya kutukuka kwetu dhidi ya kifo. Kwa kweli, Maria ni kama balozi wetu huko mbinguni pamoja na Kristu, na ni alama ya tutakavyokuwa hata sisi siku moja hapo baadaye. Kristo alikuwa anatufundisha kuwa na matumaini hayo ya baada ya kifo.

Kubali yaishe:

Katika Injili unamkuta Elizabeti anamsalimia Maria kimila kabisa cha wakati wake anaposema: “Amebarikiwa yeye aliyesadiki kwamba yatakamilika yale yaliyonenwa na Bwana.”  Ama kweli hapa Elizabeti amenena, kwamba ukuu wa Maria siyo hasa ule wa umama wa kimungu, yaani kuwa Mama wa Mungu, bali hasa katika imani yake isiyolegea kabisa juu ya utimilifu wa Neno la Mungu. Hilo Neno ambalo kutokana na kule kuitikia kwake “Nitendewe.” Kama vile angesema “Nimekubali” hapo Neno hilo likawa mwili katika Yesu Kristu, Mwana wa Mungu, anayeokoa na kufanya upya maisha moja kwa moja. Kumbe neno linaweza kuwa kitu. Padre wa kwanza mzalendo aliitikia Neno la mwito wa upadre, “Nimekubali” na Neno hilo limezaa matunda ya uwepo wa upadre uliodumu hadi leo katika Tanzania.

Imani inaongoza kwenye furaha ya Injili!

Imani ni pamba ya safari wa kuelekea kwenye furaha. Furaha aliyokuwa nayo Elizabeti inamkuna Maria hadi anamwimbia Elizabeti wimbo mtamu unaoitwa “Moyo wangu wamtukuza Bwana” kwa kilatini ni Magnificat. Kutokana na wimbo huo, Maria anathibitisha kwamba heri ile ambayo Mungu ameitoa, siyo imeidhihirika kwake peke yake, bali inatakiwa pia iwe ukumbusho wa kihistoria unaotakiwa kuhifadhiwa na kudhihirika daima pale anapoendelea kuimba kwamba: “Tokea sasa vizazi vyote wananiita mwenye heri. Kwa sababu Mwenyezi amenitendewa makuu, na jina lake ni Takatifu.” Ama kweli hata makuhani wake wote wanapaswa kuimba maneno hayo, kwani wamebahatika kutendewa makuu na Mwana wake hasa kwa kule kuwa makuhani wake, na kushirikishwa cheo na kazi zake. Maria ni nembo ya uwepo wa Mungu katika historia na katika yeye mwenyewe. Kadhalika kuhani ni nembo uwepo wa Kristu katika historia na katika padre mwenyewe.

Hapo tu ndipo unaweza kuona ukweli huu kwamba Mungu amebadilisha vigezo vya mivuvumko ya maisha. Kwamba ya “Kale hayakoo”. Kwamba utawala wa mabavu uliotamba ulimwenguni kwa karne nyingi sasa umepinduliwa pale Maria anapoimba: “Amewaangusha wenye vyeo katika viti, na kuwakweza wanyenyekevu”. Hivi ndivyo Mungu alivyomfanyia msichana huyu Maria. Leo Mama akiwa mbinguni anafurahiana na Mwanae Yesu, anafurahiana pia na wanae Wakristu walioko hapa duniani pamoja na  Makuhani wao, kutokana na  mambo makuu waliyotendewa na Mwenyezi Mungu. Heri sana kwa Jubilei ya miaka mia moja ya Ukuhani Tanzania.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.