2017-08-14 08:37:00

Mwenyeheri Oscar Romero aliyezimishwa kama risasi ndani ya maji makuu


Mama Kanisa anaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 100 tangu alipozaliwa Mwenyeheri Osca Armulfo Romero, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la San Salvador, aliyeandika historia ya maisha yake kwa kuuwawa kikatili kunako mwaka 1980 wakati alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Kuanzia tarehe 11- 13 Agosti 2017, maadhimisho haya yamefanywa kwa maandamano makubwa, tafakari na Ibada ya Misa Takatifu na kilele cha maadhimisho haya ni wakati wa Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho yaani tarehe 15 Agosti 2017.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya anawakilishwa na Kardinali Richardo Ezzati Andrello, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Santiago de Chile. Kunako mwaka 1997 Mtakatifu Yohane Paulo II akaidhinisha mchakato wa kumtangaza kuwa Mwenyeheri, lakini ukasuasua. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akuvalia njuga na Papa Francisko akamtangaza kuwa Mwenyeheri kunako mwaka 2015. Mwenyeheri Osca Armulfo Romero, ni Askofu wa kwanza kuyamimina maisha yake kutoka El Salvador! Huo ukawa ni mwanzo wa kutoweka kwa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano nchini El Salvador na watu wakajikuta wakitumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Hivi ndivyo anavyoandika Askofu mkuu Josè Luis Escobar Alas wa Jimbo kuu la San Salvador katika kumbu kumbu ya miaka 100 tangu alipozaliwa Mwenyeheri Osca Armulfo Romero na miaka 40 tangu alipouwawa kikatiliki Padre Nelson Rutulio Lemus, Grande, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Imekwishagota miaka 25 tangu vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini El Salvador ilipositishwa na cheche za amani zikaanza kusikika tena!

Hata hivyo ghasia na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia bado ni changamoto kubwa sana nchini El Salvador na kwamba, Kanisa nchini humo ni shuhuda wa imani kutokana na watoto wake kuendelea kumwaga damu yao kama kielelezo cha ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Askofu mkuu Josè Luis Escobar Alas katika barua hii ya kichungaji anawakumbuka mashuhuda wa imani 24 waliouwawa kikatiliki, lakini kwa namna ya pekee kabisa anamkumbuka Padre Rutulio Grande aliyesimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu mintarafu kweli za Kiinjili, kiasi cha kuyamimina maisha yake, wakati Mama Kanisa alipokuwa anaingia kwenye mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo.

Aliwafundisha waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Kristo, kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii! Akawataka wawe ni raia wema na mfano bora wa kuigwa na jirani zao. Mifano bora ya mashuhuda hawa wa imani, iwe ni chachu ya kuchuchumilia utakatifu wa maisha unaoshuhudiwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Mashuhuda wa imani ni watu ambao walikuwa kweli ni mihimili ya uinjilishaji kwani kati yao walikuwemo: Makatekista, Viongozi wa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo na Viongozi wa kwaya!

Wote hawa walishutumiwa  na hatimaye kuuwawa kikatili kwa sababu walijihusisha na uinjilishaji dhana iliyokuwa ni tishio kwa utawala wa kikomunisti kwa wakati ule! Changamoto kwa waamini katika kumbu kumbu hii ni kuendelea kujikita katika utekelezaji wa dhamana na utume waliojitwalia wakati wa Sakramenti ya Ubatizo kwa kushiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo; dhamana inayopaswa sasa kumwilishwa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Walikuwa ni mashuhuda wa imani kwa vile walijiaminisha na kumtegemea Roho Mtakatifu katika maisha na utume wao.

Ni Mashuhuda waliosimama kidete kupinga uchu wa mali na madaraka; ukosefu wa haki na amani; mambo yaliyokuwa yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu. Haya ni mapambano endelevu hata kwa Wakristo wa nyakati hizi. Neema ya Sakramenti ya Ubatizo na nguvu inayobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, ziwaimarishe ili kweli wawe ni mashuhuda amini wa Kristo na Kanisa lake, daima wakiendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo, mafao ya wengi pamoja na wokovu wa watu wa Mungu. Vifo vya mashuhuda wa imani ni mwaliko wa kutambua kwamba, hata Wakristo wa nyakati hizi ni ushuhuda kwamba, hata wao wanaweza kumfuasa Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao na Bikira Maria katika huduma makini kwa jirani zao!

Kwa upande wake Kardinali Gregorio Rosa Chavez, Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la  San Salvador anasema, Mwenyeheri Osca Armulfo Romero alikuwa kwa hakika: Askofu aliyefundisha, ongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu; kiongozi na shuhuda wa Injili; mtetezi wa Kanisa, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Alikuwa ni sauti ya kinabii kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii! Alikuwa ni chombo na shuhuda wa huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake! Kama Padre na Askofu akasimama kidete kutetea haki, amani na upatanisho. Alijikita katika majadiliano kati ya Kanisa na walimwengu, changamoto endelevu hata kwa watu wa nyakati hizi.

Kardinali Gregorio Rosa Chavez anawataka vijana wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho kati ya watu wa Mataifa. Watumie kipaji cha ujana na ubunifu katika mchakato wa maboresho ya maisha yao na ushiriki wao katika maisha na utume wa Kanisa. Vijana wajisikie kuwa ni sehemu muhimu sana ya Kanisa, kama kielelezo cha ushuhuda wao Kanisa linapomkubuka Mwenyeheri Osca Armulfo Romero, miaka 100 tangu kuzaliwa kwake! Waamini watambue kwamba, wanafanya hija ya imani kwa Kristo na Kanisa lake! Huyu ndiye Kristo Yesu: Njia, Ukweli na Uzima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.