2017-08-14 08:55:00

Mtakatifu Maximilian Kolbe mfano bora wa utume na upendo kwa jirani


Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Agosti, anafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe, Padre na Mfiadini. Ni Padre aliyependa kwa dhati, akalimwilisha pendo hili kwa matendo na katika ukweli kama Padre na shahidi wa mwanga angavu wa imani inayomwilishwa katika matendo. Ni shahidi aliyeongozwa na Mwanga wa Kristo Mfufuka, kiasi cha kuyatoa maisha yake kwa ajili ya Mungu na jirani. Ni chachu ya majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi; msamaha, upatanisho na amani ya kudumu. Hii ndiyo changamoto inayofanyiwa kazi na vijana huko Varsavia, nchini Poland na vijana kutoka katika nchi kumi na tatu duniani, kati yao zikiwemo: Marekani, Russia, Ujerumani na Poland. Kanisa ni Sakramenti ya wokovu ndiyo maana linapenda kujibidisha katika mchakato mzima wa haki, amani na upatanisho duniani.

Kongamano hili ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ulioanza miongoni mwa vijana hao kuanzia tarehe 11 Agosti na unahitimishwa, tarehe 16 Agosti 2017. Vijana wanapaswa kuifahamu historia, ili kuwajengea uwezo na nguvu ya kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Haki, amani na upatanisho ni changamoto endelevu katika maisha ya watu anasema Askofu mkuu Ludvig Schick, kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani. Misingi ya haki na amani inapaswa kumwilishwa miongoni mwa vijana, ili wawe tayari kusimama kidete kuilinda, kuitangaza na kuidumisha, dhidi ya dhana ya udini, ukabila, utaifa na umajimbo unaohatarisha mshikamano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe, Padre na Mfiadini ni mfano thabiti katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kwa njia ya ushuhuda wa maisha, changamoto petu kwa vijana wa kizazi kipya!

Itakumbukwa kwamba, wakati wa madhulumu ya Kinazi, alitupwa kizuizini na kuonja mateso na madhulumu ya utawala wa kinazi kwenye kambi ya mateso ya Auschwitz, wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Akiwa gerezani akaamua kutoa sadaka ya maisha yake kama Padre ili kuokoa maisha ya Baba wa familia, aliyekuwa mwenza pale gerezani, ushuhuda wa hali ya juu wa imani inayomwilishwa katika matendo. Akafariki dunia kwa njaa hapo tarehe 14 Agosti 1945. Huu ni mwanga wenye nguvu na uwezo wa kumwangazia mwanadamu katika maisha yake yote, kwani ni Mwanga unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, aliye hai, Mungu ambaye ni upendo mkalimifu, unaomchangamotisha mwamini kujenga maisha thabiti.

Kutokana na ukweli huu, Baba Mtakatifu Francisko katika waraka wake wa kitume “Lumen Fidei” yaani “Mwanga wa Imani” anasema, Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani kwani unafumbata upendo wa Mungu, ushuhuda na tafakari ya kina, ili kila mtu anayemwangalia Yesu pale Msalabani aweze kuamini na kuokoka. Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe alizaliwa kunako mwaka 1894, akajiunga na Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Francisko kama mtawa. Akakuza na kuimarisha Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, kiasi hata cha kuanzisha "Jeshi la Bikira Maria". Ni Padre aliyetekeleza utume wake kwa njia ya mahubiri ya kina yaliyokuwa yanabubujika kutoka katika Neno la Mungu. Alikuwa ni mwandishi mahiri aliyetumia taaluma yake kuendeza Habari Njema ya Wokovu na Kweli za Kiinjili. Alionesha ari na mwamko mkubwa wa shughuli za kimissionari Barani Ulaya na Asia, leo hii ni mfano bora wa kuigwa si tu katika maisha, wito na utume wake kama Padre, bali kama mfuasi amini wa Kristo aliyejitahidi kuyasadaka maisha yake, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda wa upendo kwa jirani zake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.