Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Makala

Askofu Msonganzila afafanua Jubilei ya Miaka 150, 100 na 60 ya Jimbo

Askofu Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma katika Barua yake ya kichungaji "Upendo kwa Utume" anafafanua maana na umuhimu wa maadhimisho ya Jubilei mbali mbali nchini Tanzania.

14/08/2017 14:53

Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, Miaka 100 ya Upadre Tanzania na Miaka 60 ya Jimbo Katoliki Musoma ameandika Barua ya kichungaji ”Upendo kwa Utume” akifafanua umuhimu wa matukio haya kwa familia ya Mungu Jimbo Katoliki Musoma. Anafafanua kwa kina hatua mbali mbali za uenezaji wa Injili Barani Afrika: Bagamoyo kama mlango wa uenezaji Injili Tanzaniza Bara na hatimaye mchakato wa uinjilishaji Jimbo Katoliki Musoma. Askofu Msonganzila anagusia kuhusu ukuaji wa Kanisa mahalia kwa kuwaangalia Mapadre wa kwanza wazalendo kutoka Tanzania. Kanisa mahalia, Jimbo la Musoma. Maadhimisho ya Jubilei hizi ni wakati muafaka wa kutathmin imani ya waamini mintarafu Sinodi ya kwanza ya Jimbo la Musoma; tathmini na utambulisho wa Mapadre.

Mwishoni anapembua kwa kina maana ya Jubilei katika Kanisa: mambo ya kuzingatia wakati wa madhimisho haya yaani: Matembezi ya Msalaba wa Jubilei, Hija, Huduma za kichungaji kwa waamini wenye vikwazo vya Kisakramenti; Ubatizo wa Msamaha kwa watoto wachanga na mwishoni, Askofu Msonganzila anahitimisha Barua yake ya kichungaji kwa sala ya maadhimisho ya kwanza ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika iliyofanyika mjini Roma kunako mwaka 1994.

Namna tutakavyoadhimisha Jubilei Jimboni Musoma

Jubilei ni wakati uliotengwa kwa ajili ya Mungu. Katika Agano la Kale Wayahudi walikuwa na utamaduni wa kuadhimisha mwaka ulioitwa “mwaka wa sabato”. Huu uliadhimishwa kila baada ya miaka saba. Mwaka huo ulikuwa ni mwaka wa kuipumzisha ardhi na mwaka wa kuwaweka huru wafungwa (Rej. Walawi 25:1-7). Pamoja na kuwaweka huru wafungwa, mwaka wa sabato ulikuwa pia ni mwaka wa kusamehe madeni, na haya yalifanyika kwa agizo la Mungu mwenyewe. Baada ya kuadhimisha mara saba mwaka wa sabato, yaani baada ya miaka arobaini na tisa, mwaka uliofuata ulitangazwa kuwa Mwaka wa Jubilei. Yale yaliyokuwa yakifanyika katika kila mwaka wa sababo yalikuzwa na kufanywa kwa namna ya pekee zaidi katika mwaka huo.

Katika Kanisa, Jubilei ndio ule “Mwaka uliokubaliwa na Bwana” (Lk. 4:19). Ni mwaka wa kupokea msamaha wa dhambi na adhabu zake, mwaka wa upatanisho kwa makundi au watu mbalimbali wenye migogoro na magomvi kati yao, mwaka wa kumrudia Mungu kwa njia ya wongofu na kwa kufanya toba ya kweli. Hii ndiyo sababu pia maadhimisho ya Jubilei katika Kanisa huambatana na kutolewa Rehema Kamili. Haya yote tunaalikwa kuyaadhimisha kwa furaha na shangwe kama ilivyo maana ya neno lenyewe Jubilei. Jubilei zetu za mwaka huu, kama zilivyo Jubilei nyingine zote, zitaadhimishwa kwa kujumuisha mazoezo yote hayo ya kiroho katika ngazi mbalimbali: mtu binafsi, familia, Jumuiya Ndogondogo za Kikristo, Parokia na Jimbo. Ndiyo maana nawaalika Mapadre kuweka msisitizo wa pekee katika homilia na katika huduma za kichungaji kwa ajili ya kuhamasisha toba, wongofu, msamaha, upatanisho na kukuza uchaji. Hata hivyo, nayaleta kwenu mambo yafuatayo ambayo yatakuwa alama mahsusi za maadhimisho ya Jubilei zetu kwa Mwaka huu.

Matembezi ya Msalaba wa Jubilei

Kumbukumbu za ukuu wa neema ya Mungu tulipata katika maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Mwaka 2000 bado ziko bayana katika mioyo yetu. Kati ya mengi yanayokumbukwa katika Jubilei hiyo ni zoezi la kiroho la kutembeza Msalaba wa Jubilei katika miji yetu, zoezi ambalo liliamsha imani na kuongeza mwamko wa watu kupokea msamaha wa dhambi na adhabu zake, kutafuta upatanisho, kufanya wongofu wa ndani na kupokea Rehema. Katika maadhimisho ya Jubilei hizi za mwaka huu ninaagiza Msalaba wa Jubilei Kuu uzunguke tena kote Jimboni kama alama hai inayobeba na kujumuisha maadhimisho yote ya mwaka huu wa Jubilei. Msalaba huu utaanza kuzunguka tarehe 31 Mei mwaka 2017, siku ya kumbukumbu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeti. Siku hiyo nitaadhimisha Misa katika Kanisa Kuu la Jimbo kwa heshima ya Bikira Maria na kuomba atusindikize kwenye matembezi hayo hadi tarehe 30 Juni 2018 tutakaporudi tena kwa shukrani Kanisa Kuu kuyahitimisha.

Ujio wa Msalaba wa Jubilei katika Parokia unapaswa kupewa uzito wa namna ya pekee katika Mwaka huu wa Jubilei. Ni muhimu yakafanyika maandalizi ya kutosha ili waamini wote wapate nafasi nzuri ya kushiriki. Ratiba ya mzunguko izingatie kwamba siku za dominika zote, wiki moja kabla ya Noeli, Oktava ya Noeli, Jumatano ya Majivu, wiki mbili kabla ya Pasaka na Oktava ya Pasaka zisiwe miongoni mwa siku za kuzungusha Msalaba. Lengo ni kuwapatia waamini nafasi ya kushiriki kikamilifu maadhimisho katika siku hizo husika. Kamati Maalumu niliyoiunda kuratibu Maadhimisho ya Jubilei hizi itatoa mapema mwongozo wa namna Msalaba huo utakavyozunguka ikiwa ni pamoja na ibada na mafundisho yatakazoambana na mzunguko huo.

Hija

Katika maadhimisho ya Jubilei yoyote, Hija ni sehemu muhimu ya mazoezi ya kiroho ya maadhimisho hayo. Kwa vile Jubilei yetu itaambatana na tendo kubwa la kuzunguza msalaba, katika nafasi ya kwanza naagiza hija zifanyike kiparokia. Ratiba ya kuzungusha Msalaba itatolewa hivi kwamba iwepo siku ya kuhitimisha mzunguko wa Msalaba kiparokia. Katika siku hiyo waamini wa parokia husika wafanye Hija kwenda Parokiani. Katika adhimisho la Misa Takatifu siku hiyo itolewe Rehema Kamili kwa wahujaji wote waliojiandaa kupokea Rehema Kamili. Aidha nasisitiza pia kuwa vikundi maalumu na hasa vyama vya kitume, vifanye hija katika vituo vyetu vya Hija, Kiabakari na Nyakatende. Wahifadhi wa vituo hivyo watoe mpango maalumu wa Hija katika mwaka huu wa Jubilei ili iwe nafasi nyingine ya watu kupokea Rehema Kamili.

Huduma za Kichungaji kwa waamini wenye vikwazo vya Kisakrameti

Mwaka uliokubaliwa na Bwana ni mwaka pia wa kuwaweka huru watu walio katika vifungo mbalimbali vya kimwili na kiroho. Kwa upendo wa kitume, ninawaalika mapadre wawe karibu zaidi na waamini ambao wana vikwazo mbalimbali vya kisakramenti. Kwa upendo wa Kristo mwenyewe ambaye hakumchukia mdhambi bali aliichukia dhambi, tutumie miongozo iliyopo ya Kanisa ili tuwasaidie katika kujikwamua kwenye vikwazo walivyomo.

Ubatizo wa Msamaha kwa watoto wachanga

Kuhusu ubatizo wa watoto wachanga, Sinodi yetu iliazimia kuwa “Isipokuwa kwa sababu maalumu na kwa kibali cha Baba Askofu, ubatizo wa watoto wachanga wasiotokana na ndoa za Kikristo uahirishwe hadi watakapokua na kupata mafundisho ya ukatekumeni”. Kwa mastahili ya maadhimisho ya Jubilei hizi, natoa kibali maalumu cha ubatizo wa watoto hawa kwenye maadhimisho ya Mwaka huu wa Jubilei. Ubatizo huu uhusishe watoto walio chini ya miaka saba ya kuzaliwa ufanyike mara moja tu katika parokia hasa wakati ambapo Msalaba wa Jubilei utakuwa katika Parokia husika. Ninawaomba maparoko watumie muda wa kutosha na wawe na uangalifu mkubwa katika kuwabaini watoto hawa wakiangalia hasa mazingira ya malezi yao. Ni muhimu wazazi au walezi wa watoto hawa wapewe mafundisho maalum walau kwa muda wa mwezi mmoja juu ya wajibu wao kwa watoto hawa ndipo ubatizo ufuate. Bila umakini na maandalizi ya kutosha watoto hawa, familia zao na jamii kwa ujumla itapokea ubatizo huu kwa mkumbo na hawatakuwa tayari kuyatwaa makukumu yanayoambatana nao.

Hitimisho

Katika kuhitimisha barua yangu, nawaalika tuyaelekeze macho na matumaini yetu kwa Bikira Maria Mama wa Mungu, Msimamizi wa Jimbo letu. Ndiye Nyota ya Uenezaji wa Injili ambaye Mt. Papa Yohane Paulo II aliiweka Afrika na utume wake wa kueneza Injili chini ya maombezi yake. Tuyakabidhi tena kwake maadhimisho ya Jubilei yetu na matunda yake kwa sala iliyotungwa na Maaskofu wenzangu wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Kwanza ya Afrika iliyofanyika mjini Roma mwaka 1994:

Ee Maria, Mama wa Mungu na Mama wa Kanisa, wanadamu wote katika tamaduni zao walifurahi kwa kuelewa kwamba Habari Njema ilikuwa imewajia, pale ulipopashwa habari ya kumzaa mkombozi, siku ya mwanzo wa kipindi kipya katika historia. Katika maandalizi ya Pentekoste mpya ya Kanisa la Afrika, Madagaska na visiwa vya karibu, waana wa Mungu pamoja na wachungaji wao wanakukimbilia na kuomba pamoja nawe ili Roho Mtakatifu alishukie Bara la Afrika na kulifanya mahali pa muungano kamili katika tofauti zetu, uwalete pamoja wana wa Bara hili kubwa wawe wana wakarimu wa Kanisa ambalo ni Familia ya Baba, undugu wa Mwana na mfano wa Utatu Mtakatifu: mbegu ya Ufalme wa Milele ianyoanza hapa duniani na kukamilika katika mji mtakatifu, mji wa haki, upendo na amani ambao Mungu ndiye mjenzi wake mkuu. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. AMINA.

+Michael Msonganzila.

ASKOFU WA MUSOMA.

Imetolewa Uaskofuni, Nyamiongo tarehe 10 Mei 2017.

14/08/2017 14:53