Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Makala

Mwaka wa Padre Tanzania: Uchambuzi wa malezi, maisha na utume wake!

Mwaka wa Padre Tanzania: Malezi: awali na endelevu; maisha, wito na utume pamoja na mambo msingi wanayopaswa kuzingatiwa na Mapadre.

12/08/2017 12:36

Kanisa nchini Tanzania linaadhimisha Mwaka wa Padre, yaani Jubilei ya Miaka 100 tangu Tanzania ilipopata Mapadre wa kwanza wazalendo kunako tarehe 15 Agosti 1917, kilele cha maadhimisho haya ni tarehe 15 Agosti 2017, huko Jimbo kuu la Dodoma. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inakuletea makala maalum kuhusu: malezi, maisha na utume wa Mapadre kama unavyochambuliwa na: Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri; Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki Bukoba pamoja na Askofu Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki Shinyanga.

Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, hapo tarehe 8 Desemba 2016 lilipitisha Mwongozo mpya wa Malezi na majiundo ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre”. Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri anasema, malezi na majiundo ya kipadre yanapaswa kupyaishwa, kuendelezwa na kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Mama Kanisa. Hizi ndizo sababu msingi ambazo zimepelekea kuchapishwa kwa Mwongozo wa Malezi ya Kipadre yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre” baada ya miaka arobaini na sita, tangu mwongozo wa mwisho ulipotolewa na Mama Kanisa. Mwongozo wa sasa unazingatia na kukidhi mahitaji msingi ya malezi na majiundo ya Kipadre ili kuweza kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni mwongozo unaotoa mwelekeo na uwiano sahihi wa malezi: kiutu, kiroho, kiakili na kichungaji kwa njia ya safari ya malezi na majiundo makini ya Kipadre, taratibu, lakini kila jandokasisi akiangaliwa kwa jicho la pekee.

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican kuhusu malezi, maisha na utume wa Padre anasema, Padre ni mhudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa. Anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya miito ya Kipadre ambayo analijalia Kanisa la Tanzania. Lakini, kuna baadhi ya majimbo ambayo “yamekaukiwa na miito”. Jambo ambalo anapenda kukazia ni kuhusu malezi na majiundo makini ya Majandokasisi seminarini na katika nyumba za malezi. Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa anawataka walezi kuwa na moyo wa kujisadaka bila ya kujibakiza, daima wakijitahidi kuiga mfano wa Kristo Mchungaji mwema, ili kweli Mapadre waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Mapadre wasaidie kazi ya ukombozi, ili Mwenyezi Mungu apewe sifa na mwanadamu apate wokovu! Mapadre wajitahidi kuwa ni wachungaji wema, watakatifu na wachapakazi, ili waweze kuendeleza huduma ya Kanisa ulimwenguni.

Naye Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma katika Barua yake ya kichungaji “Upendo kwa Utume” kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, Miaka 100 ya Upadre Tanzania Bara na Miaka 60 ya Jimbo Katoliki Musoma anasema Jubilei ya miaka 100 ya upadre katika Tanzania inatupa kwa namna ya pekee zaidi sisi mapadre wasaa wa kujitathmini. Hapa tunaliona bayana mbele yetu swali ambalo Kristo aliwauliza wanafunzi wake “watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?” (Mt. 16:13). Katika swali hii ni sisi tunasimama mbele ya wanafunzi wetu na kuwahoji “watu husema sisi mapadre ni akina nani?” Swali hili la msingi kwetu kujitathmini linagusa undani wa utambulisho wetu kama mapadre.

Katika Mausia ya Kitume Pastores Dabo Vobis, Mt. Papa Yohane Paulo II anaelezea dhana ya  Utambulisho wa Mapadre kwa maneno haya: “Mapadre ni wawakilishi wa kisakramenti wa Yesu Kristo - kiongozi na mchungaji ambao kwa mamlaka waliyopewa hutangaza neno lake na huendeleza kazi yake ya ukombozi hasa kwa njia ya sakramenti za ubatizo, Kitubio na Ekaristi wakiyatolea mapendo yao kama zawadi ya nafsi zao nzima kwa kundi walilokabidhiwa ili walikusanye na kulipeleka kwa Baba kwa njia ya Kristo katika Roho Mtakatifu”

Wengi wetu tunaifahamu simulizi inayovutia sana kumhusu Mtakatifu Maximilian Kolbe, Padre na Mfiadini. Katika siku ya kifo chake alipokuwa gerezani Auschwitz, Poland  alijitolea auawe badala ya  mfungwa ambaye angeacha mke na watoto. Katikati ya kilio cha mfungwa huyo ghafla Mt. Kolbe anasema “Mimi hapa najitolea kuuawa badala yake”. “Wewe ni nani?” aliuliza Askari. Mt. Kolbe alijibu bila kusita “Mimi ni Padre Mkatoliki”, akakipokea kifodini. Utambulisho alioukiri Padre mwenzetu, Mtakatifu Maximilian Kolbe, ni utambulisho anaopaswa kuushuhudia kila Padre, kila siku ya maisha yake. “Dhana hii” kama anavyofundisha Papa Mstaafu Benedikto wa XVI “ni ya msingi katika kutekeleza wajibu wetu wa kipadre sasa na hata baadaye”. Nawaalika mapadre kuhuisha utambulisho huu katika tathmini ya Upadre wetu mwaka huu wa Jubilei. Fikra zetu, maneno yetu, kazi zetu na maisha yetu yote kwa ujumla yawe ni ungamo la utambulisho wetu - sisi ni mapadre wakatoliki.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki Bukoba anasema katika safari ya maisha yake ya kipadre alikumbana na changamoto nyingi lakini hakukata tamaa! Daima alipata ushirikiano mzuri kutoka kwa wazazi na walezi wake, waliomtia shime hata pale ambapo mbele yake kulionekana kuwa na giza nene, kutokana na hali ya familia, uwezo na karama ambazo amekirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya sifa na utukufu wa watu wake. Anakiri kwamba, wosia aliopewa na Baba yake mzazi tangu siku ile ya kwanza alipoanza safari ya malezi na majiundo ya kikasisi kwa kumtaka “kuinamisha shingo” yaani kuonesha utii ni changamoto ambayo imemwezesha kusonga mbele katika safari ya maisha yake ya Kipadre na kiutu, hadi ukamilifu wa Daraja ya Upadre, kwa kuwekwa wakfu kuwa ni Askofu.

Jambo la msingi kwa Padre anasema, ni kuhakikisha kwamba, anaupenda, anauthamini na kuulinda Upadre wake kwa hali na mali: kwa akili zake zote, kwa moyo wake wote na kwa nguvu zake zote! Mambo mengine wanaweza kumnyang’anya, lakini daima ajitahidi kuukumbatia Upadre wake. Adhabu yoyote anaweza kuipokea na kuifanya, ili kuboresha maisha, wito na utume wake kama Padre. Hii inatokana na ukweli kwamba, zawadi ya wito na maisha ya kipadre imehifadhiwa katika chombo cha udongo kinachopaswa kuboreshwa kwa njia ya: Sala, tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Mapadre waupende sana wito wao!

Askofu Desiderius Rwoma anasema, Jambo la pili ambalo Mapadre wanapaswa kuzingatia ni kushinda uovu kwa wema, kauli mbiu aliyoitumia wakati wa maaadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 40 ya Upadre wake uliotukuka. Anatambua kwamba, fadhila ya unyenyekevu na uvumilivu zimemsaidia sana katika safari ya maisha na utume wake. Amekutana na changamoto nyingi, lakini akaweza kuzivuka kwa njia ya unyenyekevu na uvumilivu; kwa kutenda wema na kushinda ubaya. Na kwa njia hii, Mwenyezi Mungu akamkirimia neema na baraka katika maisha na utume wake.

Askofu Desiderius Rwoma anawataka Mapadre kuwa wanyenyekevu, wavumilivu na watiifu kwa Kristo na Kanisa lake. Daima wajitahidi kumwiga Kristo Mtumishi wa watu na wala siyo Kristo Mfalme huko wanaweza kuelemewa na ubinafsi, wakashindwa kutekeleza dhamana hii nyeti; wawe tayari kuwa ni mashuhuda amini kwa kumwiga Kristo Nabii wa ukweli na huruma ya Mungu kwa waja wake. Kristo Yesu, Mtumishi, ni kielelezo makini cha Padre katika ulimwengu mamboleo; ni sura ya mvuto na mashiko kwa watu wa Mungu, hasa wakati huu Kanisa nchini Tanzania linapoadhimisha Mwaka wa Padre. Daraja takatifu ni zawadi na neema ya Mungu kwa waja wake, kwa ajili ya huduma kwa mambo matakatifu. Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki Bukoba, anawataka Mapadre kuwa na kiasi katika maisha; waheshimu na kuthamini wito na maisha yao ya Kipadre. Wawe na  busara na hekima katika kufikiri, kuamua na kutenda, daima wajitahidi kujiweka chini ya ulinzi na maongozi ya Mwenyezi Mungu kama udongo wa mfinyanzi, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwatumia kadiri ya mahitaji ya Kanisa kwa kuzingatia: karama, uwezo na nafasi katika maisha na utume wa Kanisa.

Kwa upande wake, Askofu Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki Shinyanga anasema, kimsingi Mapadre wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Katika maisha na wito wao, wakuze moyo wa sala, tafakari ya Neno la Mungu, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Mapadre wawe ni chachu ya upendo ambao unafumbatwa katika: umoja, amani na mshikamano wa kweli. Mapadre wawe ni mashuhuda wa kutenda wema, kwa kutambua kwamba, hii ni changamoto kwa binadamu wote kutendeana wema, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Bila upendo, yote ni bure anasema Askofu Liberatus Sangu.

Katika Makala haya maalum kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 ya Upadre Tanzania, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inapenda pia kukushirikisha mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na Mapadre katika maisha na wito wao kama yanavyofafanuliwa na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican. Anasema, Mapadre wanapaswa kumtambua na hatimaye kumuiga Kristo Yesu: kiongozi na mchungaji mwema, mwaminifu, mtiifu kwa Baba yake wa mbinguni na mwenye upendo usiokuwa na mipaka. Mapadre waoneshe na kushuhudia: uaminifu, upendo, unyofu, unyenyekevu na huruma inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake! Wawe ni watu wenye mvuto na mashiko kutokana na maisha na utume wao kwa familia ya Mungu. Wawe ni mfano bora wa kuigwa, daima wakijitahidi kumfuasa Kristo Yesu; mwalimu na mlezi wa Mapadre katika huduma takatifu kwa watu wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

12/08/2017 12:36