Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Kanisa linatumwa na Kristo kuwa ni shuhuda wa Injili ya matumaini!

Kanisa litambuna na dhoruba pamoja na mawimbi makali katika historia, maisha na utume wake, lakini Kristo Yesu, ataliokoa kwa wakati muafaka na kulifikisha bandari salama! Jambo la msingi ni imani kwa Kristo Mwana wa Mungu aliye hai! - AP

12/08/2017 09:45

Ninapenda kuchukua fursa hii kukukaribisha katika kipindi cha Liturujia ya Neno la Mungu, Kanisa linapoadhimisha Jumapili ya XIX ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa. Kwa ufupi tunajulishwa kwamba, Mwenyezi Mungu anapatikana katika Ibada, historia ya maisha ya mwanadamu; katika: ukimya, utulivu na amani ya ndani na wala si katika vurugu, makeke na fujo, kwani Mwenyezi Mungu ni asili ya amani na furaha ya kweli. Imani ni zawadi na fadhila ya Kimungu na kwamba, imani hai hutenda kazi kwa upendo. Ni jukumu la mwamini kujitahidi kuimwilisha imani hii katika matendo: kwa kuiungama, kwa kuishuhudia na kuineza.

Ikumbukwe kwamba, huduma na ushuhuda ni muhimu sana kwa wokovu wa binadamu. Injili ya leo, ni mwendelezo wa miujiza iliyotendwa na Yesu! Baada ya kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili, Yesu anajidhihirisha kwa mitume wake, akitembea kwa miguu juu ya maji! Petro anamwomba ruksa ili aweze kuungana naye, lakini kwa bahati mbaya, akaingiwa na shaka kwa sababu ya imani haba na hapo akaanza kuzama na huo ukawa ni mwisho wa muujiza! Miujiza iliyotendwa na Kristo Yesu ilipania kuimarisha imani ya watu wake!

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Mwinjili Mathayo kwa ufupi kabisa anapenda kutushirikisha matukio ambayo yameacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za Wakristo wa Kanisa la mwanzo. Anawaonesha mitume wanaosafiri peke yao bila ya kuambatana na Kristo Yesu, ambaye anajitenga nao ili kwenda kusali faraghani, kuteta na Baba yake ya mbinguni. Katika mazingira yote haya, chombo walichokuwa wanasafiria mitume kilikumbwa na misuko suko, kiasi cha kutaabika baharini kutokana upepo mkali. Yesu anawatokea huku akitembea kwa miguu juu ya bahari, kiasi cha kuwafanya mitume kuingiwa na hofu! Petro mwenye imani haba anataka naye kutembea juu ya bahari, lakini anaanza kuzama kama “nanga majini”, na hatimaye kuokolewa na Kristo Yesu!

Jumuiya ya Wakristo wa Kanisa la mwanzo, waliliona Kanisa katika mfano huu kwa Petro mtume, kupewa dhamana ya kuliongoza na hatimaye kulivusha Kanisa katika historia yenye mawimbi mazito. Kanisa lilikuwa linapitia kipindi kigumu sana cha nyanyaso na madhulumu. Mitume walitiwa pingu, wakatupwa gerezani na wengine wakakatwa vichwa vyao! Hao ndiyo akina Stefano Shahidi, aliyetwangwa kwa mawe hadi kufa! Kanisa likasambaratika na kuanza kuenea Palestina. Roma, kulikuwa kunawaka moto! Nerone, akatembeza upanga dhidi ya Wakristo! Kilio cha Wakristo kikaenea sehemu mbali mbali za dunia kwani Kanisa lilikuwa linakumbana na mawimbi mazito ya bahari. Wakristo wakagundua kwamba, hapa dawa si kukimbia na kuliacha Kanisa, bali walipaswa kusimama kidete: kuimwilisha, kuiungama, kuishuhidia na hatimaye, kuieneza imani hiyo kwa Kristo na Kanisa lake.

Hii ndiyo sehemu ya Injili ya matumaini katika shida na magumu; katika nyanyaso na dhuluma, kamwe Wakristo wasikate wala kukatishwa tamaa! Waendelee kujikita na kujiaminisha kwa Kristo Yesu kwa njia ya sala, kama alivyofanya Petro mtume, akapiga kelele, kuomba msaada wa Kristo! Kwa njia hii, Kristo mwenyewe atawainua, atawafufua na kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo. Injili ya matumaini iwasaidie waamini kupambana na magumu na changamoto za maisha ya imani na utu wema! Kamwe wasijiamini kipumbavu! Watazama ndani ya maji kama risasi! Hayo ndiyo yaliyompata Petro Mtume, aliyetaka kujitafuta na kujiamini mwenyewe, akadhani kwamba, yote alikuwa anayatenda kwa nguvu na jeuri yake binafsi! Ni Petro huyu huyu, atakaye mkana Yesu mara tatu; leo anaanza kwa kuzama kutokana na hofu na imani haba “imani kiduchu”. Anakosa imani, dira na mwelekeo sahihi wa maisha.

Mwinjili Mathayo anawakumbusha waamini kwamba, katika shida, mahangaiko na changamoto za maisha, hawana sababu ya kulikimbia Kanisa, bali kushikamana na Kristo Yesu, ili kushuhudia na kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kwani kwa njia ya imani yao, wataweza kuokolewa na Kristo Yesu katika pilika pilika na majanga ya maisha! Ndiyo maana walipoona matendo makuu ya Mungu anayeokoa, anayesamehe na kusahau wote waliokuwa ndani ya chombo wakamsujudia wakisema kwa hakika Yesu ni Mwana wa Mungu aliye hai!

Ndugu yangu, bahari leo hii ni ulimwengu mzima ambamo Wakristo wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Chombo cha wokovu ni Kanisa la Kristo! Litakumbwa na dhoruba na mawimbi mazito ya kashfa na utepetevu wa imani kutokana na ubinadamu, hata hivyo Kanisa bado litazidi kusonga mbele! Katika toba na wongovu wa ndani, Kristo atakuja katika hali ya ukimya; yaani “Usiku wa manane” ili kuwaokoa! Huu ndio mzani wa kupima imani ya kweli kwa Kristo na Kanisa lake na wala si imani ya miujiza ya kujitafutia ujiko na umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko wa kutaka kutembea kwa miguu juu ya bahari.

Tunakumbushwa tena umuhimu wa sala katika maisha ya mwamini, alama ya kujiaminisha na kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu anayepatikana katika hali ya utulivu, amani na kimya kikuu na wala si katika matetemeko ya ardhi, moto mkali, miamba kuvunjika na kuyeyuka kama nta! Mwenyezi Mungu anapatika katika: Ibada, historia, maisha, amani na utulivu wa ndani. Tumwombe Mwenyezi Mungu ujasiri wa kumwita kila wakati katika safari yetu ya maisha, ili tuweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Habari Njema ya Wokovu sanjari na Injili ya matumaini, kwa wale waliokata tamaa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

12/08/2017 09:45