2017-08-11 12:50:00

Papa Francisko: Sitisheni mara moja zoezi la kifo laini!


Baba Mtakatifu Francisko analitaka Shirika la “Ndugu wa Upendo” lililoanzishwa kunako mwaka 1899 huko Ubelgiji na sasa linamiliki na kuendesha hospitali 15 za wagonjwa wa afya ya akili, kuhakikisha kwamba, linasitisha mara moja kutekeleza sera na mikakati ya kifo laini, kinachofumbatwa katika utamaduni wa kifo. Zoezi hili ni kinyume kabisa cha Mafundisho Jamii ya Kanisa na Injili ya uhai inayojikita katika utu, heshima na hadhi ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kutunzwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Taarifa zinaonesha kwamba, Ubelgiji na Nchi za Scandinavia, ndiko mahali ambapo sheria inawaruhusu wafanyakazi katika sekta ya afya kutekeleza mpango wa kifo laini au “eutanasia”. Mheshimiwa  Raf  De Rycke, Mkuu wa Shirika la Ndugu wa Upendo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alisikika akisema, sera hii ilikuwa inatumiwa kwa ajili ya kuwasaidia waliokuwa wanateseka sana, kazi ambayo imetendwa kwa uangalifu mkubwa; kwa kuheshimu uhuru wa madaktari na wafanyakazi katika sekta ya afya mintarafu sheria na taratibu za nchi ya Ublegiji.

Shirika la “Ndugu wa Upendo” ambalo lina makao yake makuu mjini Roma, nchini Italia, mwezi Mei, 2017 lilikiri kwamba kwa kutekeleza sera na mikakati ya kifo laini lilikuwa linakwenda kinyume cha Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kwa mara ya kwanza katika historia, Shirika la kitawa ndani ya Kanisa Katoliki linathubutu kutangaza wazi wazi kwamba, kifo laini ni sehemu ya utekelezaji wa huduma kwa wagonjwa, dhamana inayotekelezwa kwa dhamiri nyofu ya madaktari wanaohusika na zoezi hili.

Wachunguzi wa kanuni maadili na Mafundisho Jamii ya Kanisa, wanasema, hapa Shirika la “Ndugu wa Upendo” limekengeuka na kwenda kinyume kabisa cha mafundisho, kanuni na maadili ya Kanisa Katoliki, hatari kubwa hasa nchini Ubelgiji. Baraza la Maaskofu Katoliki Ubelgiji liliijulisha Vatican kuhusu “sakata hili” na hapo uchunguzi wa awali ukafanywa na Vatican. Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuridhishwa na ukweli huu kuhusu kifo laini, ameamuru kwamba, Shirika hili kuanzia mwezi Agosti, 2017 lisijihusishe tena na zoezi ya kifo laini katika hospitali zake, kwani mwelekeo huu unaweza kulitumbukiza shirika katika adhabu mbali mbali kiasi hata cha kutengwa na Kanisa.

Takwimu zinaonesha kwamba, wagonjwa wengi wanaokimbilia msaada wa kifo laini nchini Ubelgiji ni wale wanaosumbuliwa na ugonjwa wa Saratani au magonjwa ya kurithi. Kuna idadi ndogo sana ya wagonjwa wanaoomba kifo laini, hawa ni sawa na asilimia 3% kiasi cha wagonjwa 4, 000 kwa mwaka. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, utamaduni wa kifo umeanza kuingia kwa kasi sana, kiasi kwamba, Injili ya uhai iko mashakani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.