2017-08-11 14:09:00

Kilele cha Mwaka wa Padre Tanzania: Vigogo kutoka Vatican kushiriki


Bikira Maria aliyekingiwa na kila doa la dhambi ya asili, baada ya kukunja kilago cha maisha yake hapa duniani, aliinuliwa katika utukufu wa mbinguni: mwili na roho. Akatukuzwa kama Malkia wa ulimwengu, kwa sababu alikuwa amefanana sana Mwanaye, Yesu Kristo, mshindi wa dhambi na mauti. Kupalizwa kwa Bikira Maria mbinguni ni kushiriki kwa namna ya pekee Fumbo la Ufufuko wa Mwanaye mpendwa Yesu Kristo na ni utangulizi wa ufufuko wa waamini wengine. Bikira Maria ni mfano wa imani na mapendo thabiti kwa ajili ya Kanisa.

Ilikuwa ni tarehe Mosi, Novemba 1950 Papa Pio XII katika Waraka wake wa Kitume “Munificentissimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kwamba, Bikira Maria alipalizwa mbinguni mwili na roho. Hili ni fundisho la imani linalopaswa kupokelewa na waamini kwa moyo wa unyenyekevu na shukrani kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Sherehe hii inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 15 Agosti. Sherehe hii inachukua uzito wa pekee sana kwa Kanisa Katoliki nchini Tanzania, kwani hii ni siku ambayo, familia ya Mungu nchini Tanzania, inahitimisha Jubilei ya Mwaka wa Padre, Kanisa linapomshukuru na kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya Daraja Takatifu ya Upadre.

Miaka 100 iliyopita, Tanzania ilibahatika kupata Mapadre wa kwanza wazalendo. Hawa ni Padre Angelo Mwirabure wa Jimbo la Geita, Padre Oscar Kyakaraba wa Jimbo Katoliki Bukoba, Padre Celestine Kipanda wa Jimbo la Katoliki la Bunda pamoja na Padre Wilibard Mupapi wa Jimbo la Bukoba. Kilele cha maadhimisho haya ni huko Jimbo kuu la Dodoma, kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 15 Agosti, 2017. Askofu Joseph Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kuelekea kilele cha Jubilei ya Mwaka wa Padre Tanzania. Taarifa inaonesha kwamba, Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki Bukoba na Padre Titus Amigu wa Jimbo Katoliki Lindi, watatoa semina.

Kilele cha Jubilei ya Mwaka wa Padre Tanzania ni hapo tarehe 15 Agosti 2017, Kanisa linapoadhimisha Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni, mwili na roho! Ibada hii itaongozwa na Askofu mku Protase Rugambwa, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa. Baada ya Misa atabariki jiwe la msingi la Kikanisa cha Makao makuu mapya  ya Baraza la Maaskofu Tanzania, Jimboni Dodoma.

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya, Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema, maadhimisho haya yatakuwa pia ni fursa kwa Askofu mkuu Marek Solczyński kujitambulisha rasmi kwa familia ya Mungu nchini Tanzania baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa  Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapo tarehe 1 Agosti 2017. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alimteua, mwezi Aprili, 2017 Askofu mkuu Marek Solczyński kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Tanzania, baada ya Askofu mkuu Francisco Padilla kuhamishiwa nchini Kuwait pamoja na kuwa ni Mwakilishi wa Kitume wa Visiwa vya Kiarabu.

Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Marek Solczyński alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Georgia, Armenia na Azerbaijan. Askofu mkuu Marek Solczyński alizaliwa tarehe 7 Aprili 1961 huko Stawiszyn, nchini Poland. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 28 Mei 1987 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Baada ya kufanya utume wake katika masuala ya kidiplomasia ya Vatican sehemu mbali mbali za dunia na tarehe 26 Novemba 2011, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu na kumwekwa wakfu tarehe 6 Januari 2012. Askofu mkuu Marek Solczyński ameshiriki kikamilifu katika maandalizi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Georgia, Armenia na Azerbaijan aliyoitekeleza kunako mwaka 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.