Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Changamoto mamboleo: fursa za ajira na huduma makini kwa wakimbizi!

Taarifa zinaonesha kwamba, kuna wakimbizi na wahamiaji wanaozamishwa baharini ili kufuta ushahidi dhidi ya wafanyabiashara ya binadamu! - REUTERS

11/08/2017 13:45

Baba Mtakatifu Francisko anasema, maskini ni kito cha thamani sana katika maisha na utume wa Kanisa! Ni amana na utajiri wa Kanisa kama ambavyo ulishuhudiwa na Shemasi mkuu Laurent, shahidi, mwanzo kabisa mwa madhulumu ya Kanisa. Umaskini wa hali na kipato ni matokeo ya mambo mengi yanayowasibu watu. Kanisa lina dhamana na wajibu wa kuwasaidia na kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kusaidiwa na Yesu wa Ekaristi Takatifu. Mama Kanisa ameadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Laurenti Shemasi mkuu na Shahidi, tarehe 10 Agosti 2017.

Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Laurenti Shemasi mkuu na Shahidi, anasema, kuna mambo makuu mawili yanayotishia amani, usalama na mafungamano ya kijamii: kwanza kabisa ni ukosefu wa fursa za ajira unaowakumba wafanyakazi na familia zao pili ni hali mbaya ya maisha ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi, lakini wanakumbana na kuta za uchoyo na ubinafsi! Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya fursa za ajira na familia, kwani kazi ni sehemu ya utimilifu wa maisha na utu wa binadamu.

Kazi inawawezesha wafanyakazi kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao, kwa kuhakikisha kwamba, familia zinapata mahitaji msingi. Pale mfanyakazi anapokosa fursa za kazi kutokana na sababu mbali mbali, utu, heshima, wajibu na dhamana yake kwenye familia na jamii iko mashakani na pole pole, familia inaanza kupoteza matumaini ya maisha! Huo unakuwa ni mwanzo wa magonjwa ya sonona! Kardinali Bassetti ambaye ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Perugia, kuhusu wahamiaji na wakimbizi anakaza kusema, hii ni changamoto pevu na endelevu katika ulimwengu mamboleo.

Hii nii changamoto inayohitaji uwajibikaji unaomwilishwa katika Injili ya upendo kwa watu wanaohitaji: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete dhidi ya biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo kwa kujikita katika: kanuni maadili na utu wema; uwajibikaji, sheria na taratibu za nchi husika. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu bila kujitumbukiza katika ushirikiano na wafanyabiashara ya binadamu na utumwa mamboleo.

Hapa kuna haja ya kukuza utamaduni na kujenga madaraja ya kukutana na watu, ili kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kama binadamu. Jumuiya ya Kimataifa ina wajibu na dhamana ya kujenga utandawazi wa mshikamano na upendo, dhidi ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; utandawazi unaojikita katika ubinafsi, uchoyo na mkono wa “birika”. Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anahitimisha mahubiri yake kwa kusema kuna haja ya kutekeleza dhamana ya huduma kwa Injili ya familia na Injili ya upendo kwa wakimbizi na wahamiaji kwa kuwajibika na kuzingatia sheria, kanuni, maadili nautu wema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

11/08/2017 13:45